Jumamosi, 15 Juni, 2024
Leo ni Jumamosi 8 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1445 Hijria mwafaka na 15 Juni 2024 Miladia.
Leo tarehe 8 Dhul-Hija ni siku ya Tarwiya. Siku hii imepewa jina la siku ya Tarwiya kwa maana ya kujitosheleza kwa maji kwa sababu katika zama za Nabii Ibrahim (as) maji hayakuwa yakipatikana katika jangwa na Arafa na kwa msingi huo watu walikuwa wakipeleka maji eneo la Arafa kutoka Makka tarehe 8 Dhul-Hija wakijitayarisha kwa ajili ya mahitaji ya maji ya kesho yake yaani tarehe tisa Dhulhija. ***
Katika siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Imam Hussein bin Ali (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad SAW aliondoka Makka na kuelekea Kufa nchini Iraq baada ya kukataa kumbai na kutoa kiapo cha utiifu kwa Yazid bin Muawiya. Miezi minne kabla ya hapo, Imam Hussein alikuwa amewasili mjini Makka akiwa pamoja na familia yake na alikitumia kipindi cha kuweko waumini waliotoka pembe mbalimbali za dunia kwa ajili ya kufanya ziara katika Nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu, kuwaamsha na kuwabainishia dhulma na ufisadi mkubwa uliokuwa ukifanywa wa utawala wa Yazid mwana wa Muawiya. Wakati huo huo kutokana na wito wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na njama za utawala wa Yazidi za kutaka kumuuwa, Imam Hussein aliondoka Makka na kueleka Kufa. ***
Tarehe 15 Juni miaka 316 iliyopita katika siku kama ya leo harakati ya wapigania uhuru wa Scotland ilikandamizwa vikali na Uingereza. Uingereza daima imekuwa ikifanya jitihada za kuiunganisha Scotland na ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo. Hata hivyo harakati za mapambano za Wascotland zilipinga vikali suala hilo. Hata hivyo mwaka 1707 mabunge ya nchi hizo mbili yaliunganishwa. Suala hilo liliwakasirisha sana Wascotland walioanzisha harakati nyingine ya mapambano mbayo ilikandamizwa vikali katika siku kama ya leo hapo mwaka 1708. ***
Siku kama ya leo miaka 176 iliyopita sawa na tarehe 15 Juni 1848, Otto von Bismarck Kansela wa Ujerumani aliuchagua mji wa kihistoria na maarufu wa Berlin, kuwa mji mkuu wa nchi hiyo. Kuteuliwa mji wa Berlin kuwa mji mkuu wa Ujerumani, kulitokana na utekelezaji wa mpango wa kuziunganisha Ujerumani mbili, uliobuniwa na Kansela Bismarck. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Ujerumani iligawanyika katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi. Mwezi Septemba 1990 baada ya kuvunjwa ukuta wa Berlin, kuliandaliwa mazingira ya kuunganishwa pande hizo mbili, na hatimaye Berlin kurejea tena na kuwa mji mkuu wa Ujerumani. ***
Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, alifariki dunia Ayatullahil-udhma Sheikh Muhammad Fadhil Lankarani alimu na marjaa mkubwa wa Kiislamu baada ya kuugua. Allamah Fadhil Lankarani alizaliwa mnamo mwaka 1310 Hijria Shamsia katika mji wa kidini wa Qum huko kusini mwa Tehran na kuanza kujifunza masomo ya dini akiwa kijana mdogo. Aidha alipata kustafidi na mafunzo ya walimu wakubwa wa zama zake kama vile Ayatullahil udhma Burujerdi na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu awarehemu. Ayatullahil Udhma Sheikh Muhammad Fadhil Lankarani katika kipindi kifupi aliweza kufikia daraja ya ijtihad. ***