Jul 01, 2024 06:03 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (56)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 56 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 56 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 49.

احْذَرُوا صَوْلَةَ الْکَرِیمِ إِذَا جَاعَ، وَ اللَّئِیمِ إِذَا شَبِعَ

Jihadharini na shambulio la mtu karimu anapokuwa na njaa, na la mtu duni anaposhiba

Katika hikma hii ya 49, Imam Ali AS anatumia busara na hikma zake kubwa kutangaza tofauti iliyopo baina ya watu wenye heshima na watukufu kwa upande mmoja na watu wakorofi, dhalili na wasio na thamani kwa upande wa pili. Anasema jihadharini na shambulizi la watu wenye heshima na utukufu wakati wanapokuwa na shida na njaa na jihadharini pia na shambulio la watu duni, wasio na thamani na wakorofi wakati wanapokuwa wameshiba na wanapokuwa hawana shida.

 

Historia ya mwanadamu imejaa matukio ya watu waungwana na pia watu waovu na wakorofi. Matukio ya watu waungwana daima yamekuwa yakijenga hamasa za kupigania haki na ukombozi na kutokubali kudhulumiwa wala kuwa chini ya utii wa yeyote isipokuwa Allah tu kiasi kwamba matukio hayo daima ni mapya na hayachakai kwa kupita muda na zama. Wakati watu wakarimu wanapotumbukia kwenye hali nzito na ngumu bila ya wao wenyewe kutaka na kuingia kwenye shida kutokana na matendo ya watu duni na waovu, na wakati heshima yao inapotiwa majaribuni, hawakai wakafunga mikono, bali hujitokeza kwenye medani ya mapambano kwani wakati huo huwa ni wajibu kulinda heshima yao ambayo ni kito adhimu na ni rasilimali kubwa kwao. Wakati heshima ya mja mwema, mwenye heshima na mtukufu inapoingizwa hatarini kwa hali ambayo hakuna namna nyingine yoyote ila kusimama ni kupigania heshima na haki yake, hapo hutumia ujudi na uwepo wake wote kulinda hadhi na heshima yake. 

 

Katika hekima hii, Imam Ali AS anatoa matamshi mazuri kuhusu watu watukufu na waungwana akisema: احْذَرُوا صَوْلَةَ الْکَرِیمِ إِذَا جَاعَ Jihadharini na shambulio la mtu karimu anapokuwa na njaa. Neno njaa hapa si kwa maana yake maarufu ya tumbo kuhitaji chakula bali ni kinaya hapa kwa maana ya kuvunjiwa heshima mtu muungwana na karimu na kufikishwa katika kiwango ambacho si cha kuvumilika tena. Ni jambo lililo wazi kwamba mtu karimu na muungwana ni mvumilivu sana na ni mtu wa kujitolea mno na sifa hiyo inashuhudiwa mara zote kwa Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW ambao walivumilia shida na njaa kwa ajili ya wengine. Hivyo ni wazi hapa kwamba makusudio ya Imam Ali ni shambulio kali la mtu muungwana na karimu pale inapokuwa hakuna njiia wala namna nyingine isipokuwa kusimama kidete kulinda na kupigania haki na heshima yake. 

Amma katika matamshi ya sehemu ya pili ya hikma hii yanayosema: وَ اللَّئِیمِ إِذَا شَبِعَ na ogopeni shambulio la mtu duni na mkorofi anaposhiba. Hapa pia ni vivyo hivyo wakati mtu duni, mkorofi asiye muungwana anapokuwa ameshiba huwa ni hatari sana kwa wanadamu wengine. Kuna mifano mingi katika historia ya mwanadamu inayoonesha maafa na mabalaa yaliyosababishwa na watu waovu, duni na mataghuti ambapo wengine walifikia hata kujiita waungu na kuwalazimisha watu wawaabudu wao bali wengine ijapokuwa hawajiiti waungu lakini matendo yao ni kama ya kujiona wao ni waungu watu. Hivyo Imam katika hikma hii anatoa tahadhari pia kwa madhara na mashambulio ya watu wa namna hiyo. 

 

Aya za 6 na 7 za Surat al Alaq zinasema: کَلَّا إِنَّ الْإِنْسَانَ لَیَطْغَى/ أَنْ رَآهُ اسْتَغْنَى Kwani! Hakika mtu bila ya shaka huwa jeuri. Akijiona katajirika. Aya hizo za Qur'ani Tukufu zinaonesha kwa uwazi namna watu duni wanapopata utajiri wanapokuwa waovu, waliojaa ghururi, jeuri na majivuno ambayo hayawaachi salama watu wengine. 

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags