Jul 09, 2024 02:21 UTC
  • Jumanne, tarehe 9 Julai, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 3 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria sawa na 09 Julai mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 1439 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, inayosadifiana na tarehe 3 Muharram mwaka wa 7 Hijria, Mtume Muhammad SAW aliwatumia barua wafalme wa tawala mbalimbali duniani, na kwa hatua hiyo akawa ameanza rasmi kuwalingania watu Uislamu kimataifa.

Baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani kati ya Mtume SAW na washirikina wa Makka huko Hudaibiya, Mtume wa Mwenyezi Mungu alipata fursa ya kuwalingania dini ya Uislamu viongozi wa tawala kubwa duniani bila wasiwasi.

Wanahistoria wanasema kuwa, Mtume aliandika barua 12 hadi 26 kwa watawala mbalimbali katika kipindi hicho wakiwamo watawala wa Roma, Iran, Uhabeshi, Bahrain, Yemen na maeneo mengine makubwa katika zama hizo ambapo kila mmoja kati ya watawala hao alitoa jibu lake. Hatua hiyo ya Mtume ilionesha wazi kuwa dini ya Uislamu inalingania haki kwa kutumia mantiki na hoja madhubuti.

Miaka 1385 iliyopita yaani tarehe 3 Muharram mwaka 61 Hijria, jeshi la Umar bin Saad liliwasili katika ardhi ya Karbala.

Baada ya Hurr bin Yazid kumzingira Imam Hussein AS na maswahaba wake katika ardhi ya Karbala na kuwazuia wasisonge mbele, Ubaidullah bin Ziyad aliyekuwa kibaraka wa mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya huko Kufa, alikabidhi jukumu la ukamanda wa jeshi la Yazid kwa Umar bin Saad. 

Siku kama ya leo miaka 617 iliyopita, alizaliwa Ibn Khallouf mtaalamu wa fasihi, mwandishi na malenga mkubwa wa Kiislamu.

Akiwa kijana mdogo alifanya safari mjini Makkah na baadaye Quds, Palestina huku akisafiri pia mjini Cairo, Misri baada ya kuwa ni kijana. Lengo la safari hizo ilikuwa ni kwa ajili ya kutafuta elimu kiasi kwamba, akiwa na umri wa miaka 26 alihesabika kuwa mmoja wa wasomi wakubwa katika vyuo vikubwa vya nchini Misri.

Mbali na hayo ni kwamba Khallouf alikuwa akisoma pia mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad (saw) na watu wa familia yake. Hadi leo turathi za msomi huyo zipo katika maktaba za Bairut, Lebanon na Damascus, Syria. 

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita na baada ya usitishaji vita wa mwezi mmoja, vita kati ya Waarabu na utawala haramu wa Israel vilianza tena.

Vita hivyo vilianza baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu mwezi Mei 1948. Vita hivyo vilisimama mwezi Juni mwaka huo kufuatia ombi la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Vita kati ya utawala wa Kizayuni na Waarabu vilipelekea kukaliwa kwa mabavu asilimia 78 ya ardhi ya Palestina na Wapalestina 750,000 kuwa wakimbizi.   

Miaka 22 iliyopita mwafaka na tarehe 9 Julai mwaka 2002 Umoja wa Afrika (AU) ulichukua nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) baada ya kuidhinishwa na wakuu wa nchi za Kiafrika.

OAU iliundwa mwaka 1963 ili kusaidia juhudi za kupigania uhuru wa nchi za Kiafrika na kutatua hitilafu miongoni mwa nchi hizo. Hata hivyo siku baada ya siku kulijitokeza hisia kwamba katika mazingira ya ulimwengu wa leo kuna udharura wa kuundwa taasisi yenye nguvu za utendaji na yenye malengo mapya zaidi. Kwa msingi huo katika siku kama ya leo mwaka 2002 wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) waliunda Umoja wa Afrika (AU) katika mji wa Durban, Afrika Kusini.

Taasisi kama vile bunge, kamisheni ya utendaji, benki kuu, mfuko wa fedha na mahakama zimezingatiwa katika umoja huo kwa ajili ya kuratibu mawasiliano na kusaidia ustawi wa kiuchumi wa nchi za Kiafrika. 

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita Sudan Kusini ilitangazwa rasmi kuwa nchi huru inayojitawala.

Nchi mpya ya Sudan Kusini iliundwa baada ya kujitenga na Sudan. Raia wa Sudan Kusini tarehe Tisa mwezi Julai mwaka 2011 walishiriki kwenye kura ya maoni kwa ajili ya kuainisha mustakbali wa eneo la kusini mwa Sudan na lile la kaskazini, kura ambayo hatimaye ilipelekea eneo la kusini mwa Sudan kujitenga na lile la kaskazini na kuundwa nchi inayojitawala ya Sudan Kusini.