Jumanne, Septemba 10, 2024
Leo ni Jumanne, mwezi 06 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hijria, sawa na tarehe 10 Septemba, 2026.
Miaka 110 iliyopita yaani tarehe 10 Septemba mwaka 1914 kulitokea vita baina ya majeshi ya Ujerumani na Russia kando kando ya Ziwa ya Masurian.
Vita hivyo vilianza kufuatia kuzuka Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kujiunga Russia na kambi ya nchi Waitifaki. Katika vita hivyo vya Masurian, Wajerumani wakiongozwa na kamanda Paul Von Hindenburg walifanikiwa kupata ushindi na kuwaua takribani wanajeshi 20,000 wa Russia na kuwateka nyara wengine 45,000.
Hatimaye mwaka 1917 baada ya kutokea mapinduzi nchini Russia, nchi hiyo ilijiondoa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi ulitokea katika eneo la Orleansville kusini magharibi mwa Algeria.
Janga hilo la mtetemeko wa ardhi lilisababisha mji mmoja uliokuwa na wakazi 30,000 kuangamia na watu 10,000 kupoteza maisha yao.
Fauka ya hayo, makumi ya maelfu ya wananchi wa kusini magharibi mwa Algeria walibaki bila ya makazi. Mtetemeko huo vilevile ulitoa pigo kubwa kwa miundombinu ya uchumi wa nchi hiyo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita inayosadifiana na tarehe 20 Shahrivar 1360 Hijria Shamsia, aliuawa Shahidi Ayatullah Sayyid Asadullah Madani, Imamu wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran wakati wa kuswalisha Swala ya Ijumaa.
Shambulio hilo la kigaidi lilifanywa na kikundi cha kigaidi cha Munafiqin. Ayatullah Madani alipatia elimu kwa maulamaa kadhaa katika mji wa Qum na kisha kuelekea Najaf Iraq, ambako aliweza kujipatia daraja ya juu ya kielimu ya Ijitihad.
Msomi huyo alikamatwa na kuteswa mara kadhaa na askari wa utawala wa mfalme wa Iran kutokana na misimamo yake ya kuupinga utawala huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini MA alimteua Ayatullah Madani kuwa Imam wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz.
Tarehe 10 Septemba mwaka 1990 yaani miaka 34 iliyopita, Samuel Kanyon Doe aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Liberia aliuawa na kundi la waasi.
Samuel Doe alishika madaraka ya nchi mwaka 1980 akiwa sajenti mwenye umri wa miaka 29 tu baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akitumia umaskini, kupanda kwa gharama za maisha na hali mbaya ya wananchi. Hata hivyo utawala wa kidikteta wa Samuel Doe haukufanikiwa kupunguza machungu na mashaka ya Waliberia bali kinyume chake alipanua zaidi hitilafu za kikabila na kuzidisha matatizo ya kiuchumi na kijamii.
Vilevile alitayarisha uwanja wa kuporwa zaidi utajiri wa madili ya almasi ya nchi hiyo kupitia njia ya kupanua zaidi uhusiano wa Liberia na Marekani na utawala haramu wa Israel. Mauaji ya Samuel Doe yalifuatiwa na vita vya ndani nchini Liberia ambavyo viliendelea kwa kipindi cha miaka 15 na kusababisha vifo vya watu karibu laki mbili na nusu.
Ni leo ni "Siku ya Kuzuia Kujiua Duniani". Mwaka 2003, siku hii ilipewa jina la Siku ya Kuzuia Kujiua Duniani kutokana na pendekezo la Chama cha Kimataifa cha Kuzuia Kujiua kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), ili kuifahamisha dunia kuhusu suala hili muhimu linalosababisha takriban vifo watu 700,000 kila mwaka na matokeo yake ya kutisha katika dunia ya kisasa.