Jumamosi, Julai 30, 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 25 Mfunguo Mosi Shawwal 1437 Hijria sawa na tarehe 30 Julai mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1289 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Imam Ja'far Swadiq (a.s) mjukuu wa Mtume Mtukufu (s.a.w) aliuawa shahidi kwa kupewa sumu kwa amri ya Mansur Dawaniqi mtawala dhalimu wa Bani Abbas. Imam Ja'afar Swadiq (a.s) alizaliwa mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina na kulelewa na baba yake mtukufu Imam Muhammad Baqir (a.s) pamoja na mama yake mtoharifu. Imam Sadiq (a.s) alibeba jukumu la uimamu na kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Muhammad Baqir (a.s). Kipindi chake kilisadifiana na zama za migogoro na mapigano makali kati ya Bani Umayyah na Bani Abbas ambapo mashinikizo yalipungua kwa Ahlul Bayt wa Mtume (saw). Imam alitumia fursa hiyo kueneza mafundisho sahihi ya Uislamu na kulea wanafunzi hodari katika taaluma mbalimbali kama kemia, hisabati, nujumu na kadhalika. Jabir bin Hayyan ambaye anatambuliwa kuwa baba wa elimu ya kemia pia alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa Imam Jaafar Swadiq (as).***
Katika siku kama ya leo miaka 69 iliyopita alifariki dunia mvumbuzi wa Kimarekani anayejulikana kama baba wa sekta ya utengenezaji magari wa nchi hiyo Henry Ford. Alizaliwa tarehe 30 Julai 1863 katika familia ya kimaskini na tangu utotoni alikuwa na hamu kubwa ya masuala ya mekaniki. Siku moja Ford aliona gari likitembea barabarani bila ya kuvutwa na farasi na akaamua kutengeneza gari lake mwenyewe. Henry Ford alifanyia majaribio mkokoteni wa kwanza usiotumia farasi akiwa na umri wa miaka 12 tu. Mvumbuzi huyo aliboresha zaidi mkokoteni huo na mwaka 1896 alifanikiwa kutengeneza gari lake la kwanza. Mwaka 1895 alipewa haki ya kutengeneza magari licha ya kwamba watu wengine pia walikuwa wanatengeneza chombo hicho na mwaka 1903 aliasisi kampuni ya magari ya Ford Motor. Ford aliwapiku watengeneza magari wengine kwa kutengeneza magari mengi ya bei rahisi.***
Miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo, alama za bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambazo hapo kabla zilikuwa zimepasiswa zilitangazwa rasmi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Imam Khomeini MA alitoa amri ya kutengenezwa bendera ya Iran ambayo itaendana na mafuhumu na malengo ya mfumo wa Kiislamu. Bendera hiyo yenye rangi tatu za kijani, nyeupe na nyekundu, katikati ina jina la Allah huku pembeni ikiwa imezungukwa na neno Allah Akbar ambalo limeandikwa mara 22 ambayo ni nembo ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyopata ushindi tarehe 22 mwezi Bahman. ***