Feb 18, 2025 08:56 UTC
  • Jumanne, 18 Februari, 2025

Leo ni Jumanne 19 Shaaban 1446 Hijria sawa na 18 Februari 2025.

Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, kulijiri vita vya Bani Mustaliq. 

Bani Mustaliq ni moja ya koo za kabila la Khuza'a ambao uliohamia katika viunga vya mji wa Makka, muda mrefu katika historia. Viongozi wa kaumu hiyo walieneza ibada ya kuabudu masanamu.

Baada ya Waislamu kusimamisha dola ya Kiislamu mjini Madina, ukoo huo wa Bani Mustaliq ambao uliendelea kuabudu masanamu, ulitangaza utayarifu wake kwa ajili ya kupigana na Waislamu. Kwa sababu hiyo Mtukufu Muhammad (saw) akiwa na kundi la wafuasi wake, alilazimika kupambana na kaumu hiyo na hatimaye kuishinda vibaya.

Miaka 461 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Michelangelo di Lodovico Buonarroti, mchongaji wa sanamu, msanifu majengo na malenga mkubwa wa Kiitalia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 89.

Michelangelo alizaliwa mwaka 1475 na kuanza kujishughulisha na uchoraji na kuchonga sanamu licha ya upinzani wa baba yake. Malenga huyo wa Kiitalia alionyesha kipaji chake haraka katika uwanja wa uchoraji, uchongaji sanamu na usanifu majengo.

Uchongaji wa sanamu za Manabii Isa na Musa huko Italia ni moja kati ya kazi kubwa za kisanaa zilizofanywa na Michelangelo katika zama zake hizo.

Michelangelo di Lodovico Buonarroti

Siku kama ya leo miaka 191 iliyopita, vikosi vya utawala wa kikoloni wa Ufaransa ambavyo vilianza kuikalia kwa mabavu Algeria mwaka 1830, vilishindwa vibaya na wapiganaji wa Amir Abdelkader al-Djezairi, kiasi kwamba theluthi moja ya askari wa Ufaransa waliuawa na nusu nyingine ya waliobakia hai walikamatwa mateka.

Wakati huo Wafaransa ambao ndio ilikuwa mara yao ya kwanza kupata hasara kubwa ya namna hiyo barani Afrika, waliamua kuomba suluhu ili kujipanga upya na kukusanya nguvu. Hata hivyo Amir Abdelkader al-Djezairi alikataa ombi hilo, hadi baada ya kupita karibu miaka miwili na kuikomboa ardhi yote ya Algeria kutoka mikononi mwa Wafaransa hao wavamizi.

Miaka kadhaa baadaye Ufaransa iliweza kuidhibiti tena nchi hiyo baada ya kuongeza askari na zana za kijeshi sambamba na kuwatumia baadhi ya viongozi wasaliti wa makabila ndani ya Algeria.

Katika siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, askari wa Ufaransa na Uhispania, walivunja mapambano ya wapiganaji wa Morocco chini ya uongozi wa Abdel-Karim Rifi, na shujaa huyo Muislamu akapelekwa uhamishoni kusini mwa Afrika. 

Abdel-Karim Rifi alianzisha mapambano yake sambamba na kuanza uvamizi wa Uhispania katika sehemu ya ardhi ya Morocco hapo mwaka 1912. Hata hivyo na licha ya mkoloni huyo kuwa na nguvu kubwa na kutekeleza mauaji ya umati dhidi ya raia wa Morocco wasio na hatia, mwaka 1921 wapiganaji wa Abdel-Karim Rifi walipata ushindi mkubwa kiasi cha kuyafanya baadhi ya maeneo ya nchi hiyo kutangaza Jamhuri.

Wafaransa nao ambao walikuwa wakiyadhibiti baadhi ya maeneo ya nchi hiyo walipatwa na hofu kufuatia ushindi wa wananchi dhidi ya Wahispania na mwanzoni mwa mwaka 1924 walianzisha hujuma kubwa dhidi ya wanamapambano hao. Jeshi la Ufaransa chini ya Jemadari Philippe Pétain ambalo mwanzoni lilishindwa vibaya na wanamupambano wa Morocco, mwezi Februari 1926 katika siku kama ya leo liliwashinda wapiganaji wa Abdel-Karim Rifi baada ya kupata msaada wa kijeshi na kutekeleza jinai kubwa dhidi ya raia wa Morocco. Kwa utaratibu huo Ufaransa ikaweza kuendeleza ukoloni wake nchini Morocco.

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita yaani mnamo tarehe 18 mwezi Februari mwaka 1965, Gambia ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza.

Uingereza ilianza kuikoloni Gambia mwaka 1588 na kupora maliasi za nchi hiyo kwa karibu karne nne.

Mwaka 1963, Uingereza iliipatia Gambia mamlaka ya ndani baada ya kudhoofika kisiasa na kiuchumi kutokana na Vita vya Pili vya Dunia na kushindwa kuendesha makoloni yake. Hatimaye ilipofika mwaka 1965 Gambia ilipatia uhuru wake.

Miaka 58 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mwanafizikia na mtengenezaji wa bomu la atomiki wa Marekani, Robert Oppenheimer.

Kabla ya Vita vya Pili vya Dunia mtaalamu huyo alifanya utafiti kuhusiana na jinsi ya kupasua atomu na kupata nishati ya nyuklia. Wakati wa vita hivyo alipewa wadhifa wa kusimamia kitengo cha utafiti katika Wizara ya Vita ya Marekani na chini ya usimamizi wake yakatengenezwa mabomu matatu ya kwanza ya nyuklia.

Hata hivyo, wakati Marekani ilipoishambulia Japan kwa mabomu ya nyuklia mwaka 1945, makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia waliuawa katika kipindi kifupi, hali iliyomfanya Oppenheimer kujutia kitendo chake hicho na akatoa wito wa kutumiwa nishati ya atomiki katika masuala ya amani. 

Robert Oppenheimer

Miaka 15 iliopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 30 Bahman 1388 Hijiria Shamsia, manowari ya kwanza ya kivita ya Iran inayojulikana kwa jina la Jamaran ilianza kufanya kazi.

Jamaran ni manowari ya kijeshi yenye uwezo wa kubeba aina kadhaa za makombora ya kuhujumu meli na kutungua makombora na ndege za adui. Pia ina rada za kisasa na uwezo wa kushiriki katika vita vya kielektroniki.

Meli hiyo inayoenda kwa kasi kubwa pia ina eneo la kutua helikopta. Baadhi ya teknolojia iliyotumia kutengeneza manuwari hiyo inamilikiwa na nchi kadhaa tu dunia na wataalamu wa Jamhuri ya Kiislamu wamefanikia kuvunja mzingiro huo na kuiwezesha Iran kuwa miongoni mwa nchi zenye utaalamu wa kubuni na kuzalisha teknolojia hiyo.

Jamaran