Jumamosi, 8 Novemba, 2025
Leo ni Jumamosi 17 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1447 Hijria mwafaka na 8 Novemba 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1155 iliyopita, alifariki dunia Abul-Abbas Ahmad Ibn Yahya Tha’lab, msomi mashuhuri wa lugha na nahau. Tha’labi aliyekuwa na asili ya Iran ya alizaliwa mwaka 200 Hijiria mjini Baghdad. Kutokana na kumbukumbu yake nzuri alijifunza kwa haraka elimu ya nahau, lugha ya Kiarabu, kusoma Qur’ani na hadithi mbele ya walimu wa zama hizo. Akiwa kijana mdogo tayari alikuwa amehifadhi fasihi ya lugha ya Kiarabu ambapo alilipa umuhimu suala hilo huku akifikia daraja ya juu katika uga huo. Miongoni mwa athari zilizosalia hii leo kutoka kwa Abul-Abbas Ahmad Ibn Yahya Tha’lab ni kitabu cha ‘Majaalisu Tha’lab’ ‘Kitabul-Faswiih’ na ‘Qawaidu al-Shi’r.’
Miaka 997 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa mmoja wa wasomi na wanafalsafa wakubwa wa Kiislamu na Kiirani, Abu Hamid Muhammad Ghazali, maarufu kwa jina la Imam Muhammad Ghazali. Ghazali alisoma elimu ya fiq'hi kutoka kwa Abu Nasri Ismail na baada ya kufikia umri wa miaka 28 alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo. Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati huo Khoja Nidham al-Mulk kumwalika msomi huyo kwenda mjini Baghdad kwa ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na masuala ya ualimu. Kabla ya kurejea Iran, Imam Muhammad Ghazali alipata kuandika vitabu vya thamani kama "Ihyau Ulumuddin," "Kemia ya Saada" na "Nasaha za Wafalme".
Siku kama ya leo miaka 369 iliyopita, alizawa Edmond Halley, mtaalamu wa nyota wa nchini Uingereza. Halley alisoma katika kitengo cha Queen kilicho chini ya chuo kikuu cha Oxford, nchini humo na kuanza kujishughulisha na masuala ya utafiti wa nyota akiwa kijana mdogo, huku akifanya safari kuelekea kusini mwa dunia kwenye kisiwa kilichoko Bahari ya Atlantic. Edmond Halley alichukua muda mwingi katika kutalii nyota ambapo aligundua kwamba, kama ilivyo kwa sayari, nyota nazo zina obiti za duara dufu na kwa msingi huo wakati wa kurudi kwao unaweza kuhesabika. Mwaka 1704 alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Oxford. Mnamo 1720, aliteuliwa kuwa mnajimu katika Royal Observatory huko Greenwich. Halley alifariki dunia mwaka 1742.
Katika siku kama ya leo miaka 351 iliyopita, alifariki dunia John Milton, malenga wa Kiingereza. Kazi za kwanza za ushairi za John Milton zilijulikana kwa majina ya Roho ya Huzuni na Roho ya Furaha. Kazi nyingine ya uandishi ya John Milton ni ile aliyoipa jina la Paradise Lost. Malenga Milton alikuwa akitetea suala la kutenganishwa serikali na kanisa, kuweko uhuru wa kuabudu na wakati huo huo aliunga mkono uchujaji wa taarifa uliokuwa ukifanywa na serikali.
Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita sawa na tarehe 8 Novemba mwaka 1895, miale ya X iligunduliwa na Wilhem Conrad Rontgen, mwanafizikia na mwanasayansi maarufu wa Ujerumani. Mtaalamu huyo mwaka 1901 alitunukiwa tuzo ya Nobel kwa kufanikiwa kugundua miale hiyo. Kwa kuwa hakutambua miale aliyoigundua, Rontgen aliamua kuipa jina la X. Miale hiyo hupenya kwa urahisi katika mwili wa mwanadamu na kwa ajili hiyo ni njia nzuri zaidi ya kuchukua taswira ya viungo au picha ya X-ray inayotumiwa kujua sehemu za ndani ya mwili zilizodhurika au kuvunjika.
Siku kama ya leo miaka 125 iliyopita alizaliwa Bi Margaret Mitchell mwandishi wa Kimarekani huko Atlanta katika jimbo la Georgia nchini humo. Baba yake Bi Mitchell alikuwa wakili wa mahakama. Kwa muda fulani alisomea fani ya udaktari, lakini baadaye alilazimika kukatisha masomo hayo kutokana na majonzi aliyokuwa nayo kufuatia kifo cha baba yake. Margaret allianza kazi ya uandishi akiwa na miaka 22. Alizidi kupata umashuhuri baada ya kuchapisha riwaya yake aliyoiita kwa jina la "Gone with The Wind."