Jumatano, 21 Januari, 2026
Leo ni Jumatano tarehe Mosi Shaaban 1447 Hijria mwafaka na tarehe 21 Januari 2026.
Mwezi wa Shaabani ulioanza leo ni mwezi wa ibada, kujipinda na kuomba maghufira.
Mtume Muhammad (saw) aliutukuza mno mwezi huu na kuuita kuwa ni mwezi wake. Mtume na maimamu watoharifu katika kizazi chake wamewausia mno Waislamu kufanya ibada hususan kufunga swaumu katika mwezi huu wa Shaabani kwa sababu ndio unaotayarisha uwanja mzuri wa kuingia kwenye mwezi wa ugeni wa Mwenyezi Mungu na wenye baraka tele wa Ramadhan.
Katika mwezi huu wa Shaabani kumetukia mambo mengi muhimu kama kuzaliwa Imam Hussein bin Ali (as) mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw) na pia tukio la kuzaliwa Imam wa Zama, Mahdi (as) Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake.

Siku kama ya leo miaka 754 iliyopita Ghiathuddin Abu Madhaffar Abdul Karim bin Ahmad anayefahamika kwa lakabu ya Ibn Taus, alifariki dunia huko Kadhimain, moja kati ya miji ya Iraq.
Ibn Taus alikuwa faqihi na mwandishi mashuhuri wa karne ya saba Hijria. Alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa na umri wa miaka 11. Baada ya hapo alijifunza fasihi ya lugha ya Kiarabu na kupata elimu kwa wanazuoni wakubwa kama Khajah Nasiruddin Tusi.
Ibn Taus ameandika vitabu kadhaa kwa lugha ya Kiarabu.

Siku kama ya leo miaka 290 iliyopita kulitokea kimbunga kikali katika Ghuba ya Bengal, mashariki mwa India na kupelekea watu laki tatu kufariki dunia.
Tufani hiyo inatajwa kuwa ndiyo kubwa na iliyosababisha maafa makubwa zaidi hadi sasa katika eneo hilo. Eneo la Ghuba ya Bengal lililoko kaskazini mwa Bahari ya Hindi na kusini mwa Asia ni miongoni mwa maeneo yanayokumbwa na vimbunga na mafuriko makubwa ya mara kwa mara ambayo aghlabu husababisha hasara na maafa makubwa.

Siku kama ya leo miaka 233 iliyopita Mfalme Louis XIV wa Ufaransa alinyongwa.
Alichukua hatamu za uongozi mwaka 1774 na kuathiriwa mno na mkewe Marie-Antoinette. Mwaka 1789 wananchi wa Ufaransa walianzisha mapambano dhidi ya Mfalme Louis XIV kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii na miaka mitatu baadaye serikali ya kifalme ilifutwa rasmi nchini Ufaransa.
Hata hivyo kutokana na kuwa mfalme Louis alikuwa ameomba msaada wa nchi za kigeni kwa siri alituhumiwa kuwa amefanya uhaini na kuhukumiwa kifo. Watu kadhaa wa familia ya Mfalme Louis XIV akiwemo mkewe Marie-Antoinette pia walinyongwa.

Tarehe Mosi Shaabani miaka 181 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad Hassan Najafi maarufu kwa lakabu ya Sahibul Jawahir.
Sahibul Jawahir alifanya uhakiki mkubwa wa masuala ya fiqhi na kusajili fikra zake katika taaluma hiyo kwa njia ya kuvutia na nyepesi. Kitabu kikubwa zaidi cha mwanazuoni huyo ni "Jawahirul Kalam" ambacho kina thamani na umuhimu mkubwa sana kati ya wataalamu wa taaluma hiyo.
Katika kitabu hicho Sheikh Muhammad Hassan Najafi ameandika masuala ya kifiqhi na sheria za Kiislamu kwa kutumia hoja madhubuti na umakini mkubwa. ****
Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, alifariki dunia Vladimir Ilyich Lenin, kiongozi wa mapinduzi ya Kikomonisti wa Urusi ya zamani.
Lenin alizaliwa mwaka 1870 ambapo alianza kupambana na utawala wa kifalme wa wakati huo nchi humo tangu akiwa chuo kikuu na hadi mwaka 1900 alielekea uhamishoni nje ya nchi. Baada ya kurejea nchini alifungwa jela na wakati mwingine akabaidishwa, ambapo alikuwa akijishughulisha na kazi ya uandishi wa vitabu mbalimbali.
Mwezi April 1917 alirejea Russia kwa lengo la kuongoza kwa karibu mapinduzi ya Kikomonisti nchini humo. Baada ya ushindi wa mapinduzi alikuwa kiongozi wa Urusi ya Zamani ambapo alifariki dunia katika siku kama ya leo mwaka 1924. ****
Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, mamluki wa utawala wa kidikteta wa Shah nchini Iran walishambulia Chuo Kikuu na Tehran na na kuwajeruhi wanafunzi wengi.
Wanachuo hao walikuwa wakiandamana kudai haki za wanafunzi waliokuwa wameandamana na kisha kukabiliwa na vitendo vya kikatili vya maafisa usalama. Askari hao waliwapiga vibaya makumi ya wanachuo na wahadhiri na kuharibu nyenzo za masomo kama vitabu na maabara.
Baada ya tukio hilo, serikali ya wakati huo kwa kuhofia kuenea malalamiko ilikifunga Chuo Kikuu cha Tehran kkwa muda wa miezi miwili na nusu.

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita sambamba na kuanza kutetereka nguzo za utawala wa Shah nchini Iran mkabala wa wimbi kubwa la mashinikizo ya wananchi na harakati za Mapinduzi ya Kiislamu, serikali ililazimika kuwaachia huru wafungwa waliokuwa katika jela za Shah na wananchi Waislamu wa Iran wakawapokea watoto wao waliokuwa wakiteseka kwa miaka mingi katika jela hizo.
Alasiri ya siku hiyo maafisa wa Jeshi la Anga la Iran walifanya maandamano na kutangaza uungaji mkono wao kwa harakati ya taifa la Kiislamu la Iran. Siku hiyo hiyo pia magazeti ya Iran yaliandika habari iliyokuwa na kichwa kilichokolezwa wino kwamba: "Imam Khomeini Kurejea Iran Siku Kadhaa Zijazo".
Habari hiyo ilizusha wimbi la hamasa na furaha kubwa kati ya wananchi wanamapinduzi wa Iran na kila mtu alianza kujitayarisha kwa ajili ya kwenda kumpokea kiongozi wa kihistoria wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini. *****