Ijumaa, 16 Oktoba, 2026
-
Leo Katika Historia
Leo ni Ijumaa mwezi 5 Mfunguo Nane, Jumada al-Ula 1448 Hijria, sawa na tarehe 16 Oktoba, 2026 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 1443 iliyopita, yaani mwezi 5 Mfunguo Nane mwaka wa tano Hijria, alizaliwa Bibi Zainab SA binti mtukufu wa Imam Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatimatu Zahraa AS.
Bibi Zainab alikuwa mashuhuri miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo.
Katika tukio la Karbala, Bibi Zainab AS alisimama kidete na kukabiliana na dhulma za watawala madhalimu na ujahili wa watu wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (as). Bibi Zainab alipelekwa Sham pamoja na mateka wengine wa Nyumba Tukufu ya Mtume SAW baada ya mapambano ya Imam Hussein (as) huko Karbala. Hotuba za Bibi Zainab mbele ya majlisi ya Ibn Ziyad, mtawala wa Kufa na katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko Sham zilikuwa na taathira kubwa katika kufichua dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya na kuonesha jinsi Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume walivyodhulumiwa.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa nchini Iran siku ya kuzaliwa Bibi Zainab AS huadhimishwa kama 'Siku ya Wauguzi'.
&&&
Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita, mnamo mwezi 5 Jumada al-Ula mwaka wa 8 Hijria vilipiganwa vita vya Mu'tah, baina ya jeshi la Waislamu na jeshi la Roma na waitifaki wake.
Vita hivyo vilitokea baada ya mjumbe aliyekuwa ametumwa na Mtume SAW huko Sham kwenda kulingania Uislamu, kuuliwa shahidi na kamanda wa ulinzi wa mpakani wa eneo hilo.
Baadhi ya wanahistoria wanasema, kuuawa shahidi wasomeshaji 14 wa Qur'ani Tukufu waliokuwa wakielekea maeneo ya mpakani ya Sham ni moja ya sababu za Bwana Mtume SAW kutuma jeshi la wapiganaji 3,000 katika eneo hilo lililokuwa likidhibitiwa na utawala wa Roma. Katika vita hivyo Bwana Mtume alimteua Ja'far bin Abi Twalib, mwana wa ami yake, kuongoza jeshi la Kiislamu, na akawateua Zaid bin Haritha na Abdullah bin Rawaha kukaimu nafasi hiyo.
Waislamu ambao hiyo ilikuwa mara yao ya kwanza kukata masafa marefu kama hayo ili kwenda kupambana na maadui, walikabiliana na jeshi la Warumi na makabila ya eneo hilo lililokadiriwa kufikia wapiganaji laki moja. Vita hivyo visivyo na mlingano vilipiganwa katika eneo la Mu'tah magharibi ya Jordan ya leo. Jeshi la Waislamu lilipigana kwa ushujaa mkubwa kiasi kwamba majemadari wake wote watatu pamoja na Mujahidina wengi waliuawa shahidi katika vita hivyo. Hatimaye Waislamu walimkabidhi ujemadari wa jeshi Khalid Bin Walid ambaye alikuwa ndio kwanza amesilimu, ambaye alitoa amri ya jeshi kurudi nyuma.
Japokuwa Waislamu hawakushinda vita vya Mu'tah, lakini waliweza kusoma mbinu na mikakati ya kijeshi ya Warumi, hatua ambayo ilikuwa utangulizi wa ushindi dhidi ya jeshi hilo katika vita vya baadaye.
&&&
Siku kama ya leo miaka 233 iliyopita, yaani tarehe 16 Oktoba mwaka 1793, aliuawa kwa kukatwa kichwa kwa shoka, malikia wa Ufaransa, Marie Antoinette, kwa amri ya Baraza la Katiba la nchi hiyo na kwa amri ya Maximilien Robespierre pia.
Miezi 10 kabla ya hapo, Louis wa 16 aliyekuwa mume wa Antoinette, alitangulia kufikwa na hatma hiyo hiyo iliyomkuta mkewe. Marie Antoinette alikuwa binti wa Maria Theresa Walburga, mtawala wa Austria na Ufaransa. Antoinette aliolewa na Louis, mrithi wa kiti cha ufalme wa Ufaransa, mnamo mwaka 1770 akiwa na umri wa miaka 14. Hatua ya Louis ya kumuoa mwanamke huyo ilikuwa na nia ya kuzikurubisha pamoja nchi za Austria na Ufaransa ambazo wakati huo zilikuwa zikishindana barani Ulaya.
Hata hivyo Wafaransa wengi hawakuridhia ndoa hiyo kiasi cha kuwafanya waendelee kumwita ‘Muaustria’ hata kipindi alipokuwa tayari ni malkia wa Ufaransa.
&&&
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita liliasisiwa Shirika la Chakula Duniani (FAO).
Hati ya kuasisiwa shirika hilo ilipasishwa Oktoba 16 mwaka 1945 katika mji wa Québec nchini Canada. Lengo ya kuasisiwa shirika la FAO ni kuzisaidia nchi wanachama kukusanya taarifa, ripoti na takwimu zinazohusiana na chakula, kilimo, utunzaji wa misitu na uvuvi na kufanya tathmini kuhusu uzalishaji wa chakula, ugavi wake na juhudi za kuboresha uzalishaji, masoko ya chakula, kulinda maliasili, kupanga sera zinazohusiana na kilimo na chakula na kadhalika.
&&&
Na siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, yalitokea maafa makubwa kwenye Msikiti Mkuu wa Kerman, magharibi mwa Iran baada ya polisi na askari usalama wa utawala wa mfalme Muhammad Reza Pahlavi kuwashambulia kwa risasi wananchi waliokusanyika kwenye eneo hilo la msikitini kwa shabaha ya kuwaenzi na kuwakumbuka mashahidi waliouawa tarehe 17 Shahrivar mjini Tehran.
Shambulio hilo la askari usalama wa Shah liliamsha hasira na wimbi jipya la harakati za wananchi za kupinga utawala kibaraka wa Mfalme Muhammad Reza Pahlavi.
&&&