Aug 30, 2016 09:57 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (135)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza sehemu ya 135 ya kipindi chenu hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho hukujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Kipindi cha juma hili tutaendelea kujali swali ambalo tumekuwa tukilijadili katika vipindi viwili vilivyopita ambalo linasema: Je, ni kwa nini Mtume Mtukufu alisisitiza katika hadithi ya Thaqalain kwamba wokovu na kuepuka upotovu wa kiitikadi hakuthibiti ila kwa njia ya kushikamana kwa pamoja na Qur’ani Tukufu na Ahlu Beit wake watoharifu?

Katika vipindi viwili vilivyopita tulipata jibu la swali hili kwa kutegemea aya mbili za Qur’ani Tukufu ambazo ni aya za 43 na 44 za Surat an-Nahl. Aya hizo zinasema wazi kwamba kama alivyofanya kuhusiana na kaumu za kale, Mwenyezi Mungu aliteremsha vitabu vya mbinguni ambavyo aliwakalifisha watu wa kiume ambao ni Manabii na mawasii wao watukufu jukumu la kubainisha na kufafanua mambo yaliyotajwa humo. Kwa msigi huo jukumu la Mtume Mtukufu (saw) halikuwa tu ni kufikisha ujumbe wa wahyi alioteremshiwa na Mwenyezi Mungu bali pia alikuwa na jukumu la kuwafafanulia watu walioteremshiwa kitabu hicho makusudio ya mambo yaliyoandikwa katika kitabu kitakatifu cha Qur’ani.

Hivyo ni katika rehema kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake kwamba amewajaalia marejeo maasumu ambayo hayafanyi dhambi wala kukosea katika kufahamu makusudio ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu ambayo wanapasa kuyarejea katika lile wasilolijiua, na watukufu hao ndio wanaotajwa na Mwenyezi Mungu kuwa wenye ukumbusho. Watukufu hao wanaokusudiwa katika aya tulizotangulia kuzijadili katika vipindi vilivyopita ni Mtume Muhammad na Aali zake watoharifu (as) kama ilivyopokelewa katika riwaya za madhehebu zote mbili za Shia na Suni.

Katika kipindi cha juma hili tutaendelea kuzungumzia suala hili ambapo leo tutazungumzia jibu la pili la Qur’ani kuhusiana na swali tunalolijadili kwa kuashiria aya ya 7 ya Surat Aal Imran, endeleeni kuwa nasi.

*********

Mwenyezi Mungu anasema katika aya hiyo tukufu: Yeye ndiye aliyekuteremshia Kitabu hiki. Ndani yake zimo Aya zilizo waziwazi ambazo ndizo msingi wa Kitabu hiki na nyingine za mifano. Ama wale ambao nyoyoni mwao mna upotovu wanafuata zile za mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake; na wala hapana anayejua maana yake ila Mwenyezi Mungu na waliozama katika elimu. Husema tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu. Lakini hawakumbuki hayo isipokuwa wenye akili.

Qur'ani; hayana shaka yaliyomo ndani yake

 

Ndugu wasikilizaji aya hii tukufu inabainisha sifa tatu muhimu za Qur’ani Tukufu ambazo ufahamu wake humpelekea muumini kufahamu moja ya hekima na neema kubwa za Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Ufahamu huo ndio humuwezesha mwanadamu kufahamu moja ya siri za Mtume Mtukufu (saw) kusisitiza kwamba kuepuka upotovu hutimia tu kwa kushikamana kwa pamoja na Qur’ani na Ahlul Beit wake watoharifu (as).

Sifa ya kwanza ni kwamba Mwenyezi Mungu aliwateremshia wanadamu kitabu kitakatifu cha Qur’ani kikiwa na aina mbili za aya ambazo ni zile zilizo wazi na nyingine za mifano. Na maana ya aya zilizo wazi hapa ni zile ambazo zina maana iliyo wazi na ya moja kwa moja kadiri kwamba hakuna uwezekano wa kuzifasiri kwa maana inayozidi moja. Nazo ni mama wa Kitabu yaani ni marejeo ya asili ambayo tafsiri zote za aya za mifano hurejeshwa kwake.

Imam Ridha (as) amenukuliwa katika kitabu cha Uyun Akhbar ar-Ridha akisema: ‘Mtu anayerejesha (aya za) mifano ya Qur’ani kwenye (aya zake) zilizowazi huongozwa kwenye njia iliyonyooka……Hakika kwenye hadithi zetu kuna mifano kama ilivyo mifano ya Qur’ani, basi zirejesheni zile za mifano kwenye zile zilizo waziwazi na wala msifuate za mifano msije mkapotea.’

Ama aya za mifano ni zile ambazo kuna uwezekano wa kufasiriwa dhihiri zake kwa zaidi ya maana moja. Nazo ni aya za maana kadhaa kama alivyozisifu Imam Ali (As) katika kulalamikia uasi uliofanywa na Makhawarij dhidi yake. Ufahamu sahihi wa aya hizi na maana inayokusudiwa na Mwenyezi Mungu hutimia kwa kuzirejesha kwa aya zilizo wazi na kuzifasiri kwa msingi wa aya hizo ambazo zinasifiwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni mama wa Kitabu.

*********

Hiyo ni sifa ya kwanza, ama sifa ya pili ni ya wale watu ambao nyoyoni mwao mna upotovu, yaani wale ambao wameyafanya matamanio kuwa mungu wao. Hao ni wale watu ambao hufuata aya za mifano katika Qur’ani kwa lengo la kutafuta fitina yaani kuwapotosha watu na kuwafanya kuwa wafuasi wao na vilevile kwa lengo la kufasiri Qur’ani kama wanavyotaka wao na kuzuia isifasiriwe au kufafanuliwa na watu wengine.

Ama sifa ya tatu ni kwamba kitabu hiki kitakatifu cha Mwenyezi Mungu kina dhahiri, asili, batini na hakika ambayo katika ulinganishaji wa dhahiri ni mfano wa roho iliyo ndani ya mwili. Na hii ndiyo siri iliyofichika kwenye Qur’ani na chemichemi safi na ya kuvutia ambayo huashiriwa na dhihiri ya aya za kitabu hicho kitakatifu. Siri hii ndiyo hupenya kwenye moyo wa mwanadamu na kuuhuisha kama ambavyo dhihiri ya Qur’ani huzungumza na akili ya mwanadamu na kuihuisha.

Na tafsiri na maana hii ni katika elimu ya gheib ambayo haijui isipokuwa Mwenyezi Mungu na wale aliowaridhia katika waja wake wema ambao huwa hawaitumii katika kuwapotosha watu na kuwafanya kuwa watumwa wao bali huitumia kama njia na chombo cha kuwaongoza kuelekea kwa muumba na Mola wao. Wao ndio wale waja wema ambao wamebobea na kuzama kwenye elimu, na Mwenyezi Mungu huwajuza na kuwafahamisha baadhi ya mambo ya gheib ambayo hawafafanuliwi wanadamu wengine. Wao ni watukufu ambao wamepewa isma na Mwenyezi Mungu yaani kinga ya kutotenda dhambi ambayo huwakinga na matamanio ya kutumia Qur’ani kama njia ya kuwafanya wanadamu wengine kuwa watumwa wao kama wanavyofanya wale ambao kwenye nyoyo zao mna maradhi na upotovu.

Qur'ani; kitabu pekee isicho na makosa

 

Ndugu wasikilizaji, kwa kufahamu sifa tatu hizi za kitabu kitakatifu cha Qur’ani, tunatambua vyema hekima na rehema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake ambapo amefungamanisha Qur’ani yake tukufu na watu wajuzi waliobobea kwenye elimu na maasumu ambao amewajaalia neema ya kufasiri na kufafanua maana halisi ya kitabu chake hicho. Mwenyezi Mungu amewajaalia wema hao kuwa mwanga wa kuwaongoza waja wake katika kuzirejesha aya za mifano kwenye aya zilizo wazi ili wapate kuongoka na kuepuka fitina, kufuata aya za mifano na kutumbukia kwenye upotovu. Vilevile Mwenyezi Mungu aliwajaalia kuwa mwanga ili wapate kukinga na kuepusha waja wake kuwafuata watu ambao wana maradhi na upotevu kwenye nyoyo zao na maimamu wa upotevu ambao hufanya juhudi za kuwafanya wenzao kuwa watumwa wao na hivyo kuwazuia kuelekea kwenye njia nyoofu na ya kumpwekesha Muumba wao. Na vilevile ili wapate kuingiza kwenye nyoyo za waja hakika za Qur’ari kadiri ya uwezo wa kila mja na hivyo hilo kuwa nishati na masurufu yao katika njia nyoofu. Kwa njia hiyo waja hao hawatatengana na Qur’ani kwa sababu Maimamu wao pia hawatengani na Qur’ani wala Qur’ani kutengana nao, kama inavyosisitiza hilo hadithi ya Thaqalain ambayo imepokewa kwa wingi katika madhehebu zote mbili za Shia na Suni.

Kwa msingi huo inabainika wazi kwamba hadithi ya Thaqalain ni maneneo ya Mtume Mtukufu (saw) yanayobainisha maana ya aya tukufu tuliyotangulia kuisoma ambayo inabainisha kile ambacho kimeashiriwa katika sifa za Kitabu cha Mwenyezi Mungu ambazo zinasisitiza udharura wa kushikamana na kitabu hicho sambamba na maasumina wa Ahlul Beit wa Mtume Mtukufu (saw). Maasumina hao ni wale wema ambao wamebobea kwenye elimu ambao huwa hawatafuti jambo jingine katika kufundisha mafundisho ya Qur’ani Tukufu isipokuwa ridhaa ya Mwenyezi Mungu.

Ama kuhusiana na ufafanuzi zaidi wa jibu la swali hili kwa kutegemea hadithi, tutalijadili hilo katika kipindi kichacho cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain, Inshaallah. Huku tukikushukuruni nyote kwa usikilizaji wenu wa kipindi hiki, kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hatuna la ziada isipokuwa kukuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi wa Barakatuh.