Sep 09, 2016 13:37 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (53)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji wa kuwa nanyi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Kwa hakika kufuata matakwa haramu ya nafsi ni kizingiti na kizuizi kikubwa katika njia ya kufikia katika saada na ufanisi na ni miongoni mwa mambo yanayohesabiwa kuwa chimbuko la masaibu, shida na taabu kwa mwanadamu. Matamanio ya nafsi ni kama moshi mzito ambao umeifanya nyumba kuwa na kiza  na kwa hakika moyo wa aina hii hauwezi kuwa na ustahiki wa kupata mwanga msafi wa kimaanawi. Imam Ali bin Abi Talib AS anasema kuhusiana na hili kwamba: Katu si dini wala akili ambayo inaweza kuwa pamoja na hali ya kuabudu matamanio ya nafsi. Wapenzi wasikilizaji kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 53 kitazungumzia matamanio ya nafsi na hadithi zinazohusiana na hilo. Karibuni.

********

Matamanio ya nafsi huambiwa kila amali na nia ambayo inafanyika kinyume na matakwa na irada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kufuata matamanio ya nafsi ni kikwazo kikubwa katika njia ya saada na ufanisi wa mwanadamu. Kusalimu amri bila ya masharti mbele ya matamanio ya nafsi na matakwa haramu ya nafsi ni adui mkubwa wa saada na ufanisi wa mwanadamu. Katika Qur'ani Tukufu Mwenyezi Mungu amewaonya Mitume wake AS kuhusiana na jambo hili. Aya ya 26 ya Surat Saad inamhutubu Nabii Daud AS kwa kusema:

Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya wewe uwe Khalifa katika nchi. Basi wahukumu watu kwa haki, wala usifuate matamanio yakakupoteza kwenye Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika wanao ipotea Njia ya Mwenyezi Mungu wakaiacha, watapata adhabu kali kwa sababu ya kusahau kwao Siku ya Hisabu.

Aidha katika aya ya 23 ya Surat al-Jaathiya, matamanio ya nafsi yanatajwa kuwa ni sanamu hatari. Aya hiyo inasema:

Je! Umemwona aliye fanya matamanio yake kuwa ndiye mungu wake, na Mwenyezi Mungu akamwacha apotee pamoja na kuwa ana ujuzi, na akapiga muhuri juu ya masikio yake, na moyo wake, na akambandika vitanga machoni mwake? Basi nani atamwongoa huyo baada ya Mwenyezi Mungu? Hamkumbuki?

Kwa hakika kufuata matamanio ya nafsi hupofusha macho, huyafanya masikio kuwa na uziwi, huifanya akili na fikra za mtu kutofanya kazi na katika hali hii humfanya mhusika ashindwe kuainisha masuala madog kabisa ya maisha. Imam Ali bin Abi Talib AS anasema: Mtu mwenye matatizo kabisa ni yule ambaye amehadaika na matamanio ya nafsi na ghururi zake.

 

Mtume SAW anayataja matamanio ya nafsi kuwa ni moja ya masanamu mabaya kabisa.

Mbora huyo  wa viumbe anasema: Hakuna sanamu chini ya mbingu mbele ya Mwenyezi Mungu ambalo ni kubwa zaidi kwa ajili ya kulifuata kama matamanio ya nafsi.

Imam Ali AS anasema kuwa, adui wa akili ni kuabudu matamanio ya nafsi.

Ukweli ni kuwa, wakati matamanio ya nafsi yanapowekwa nafasi ya akili na mtu akawa anaabudu na kufuata matamanio ya nafsi, jambo hilo halina natija nyingine bighairi ya kupataa, taabu, mashaka na majanga.

Mintarafu hiyo ndio maana sio jambo la kushangaza kusikia Mtume SAW akimwambia Imam Ali AS kwamba: Sehemu hatari zaidi ya kutupwa saada na ufanisi wako ni kuabudu matamanio ya nafsi; kwani kufuata matamanio ya nafsi  hukufanya usiifuate haki na husahaulisha matarajio ya muda mrefu ya akhera.

Kwa hakika matamanio ya nafsi ni chimbuko la madhambi yote na mtu mwema na mcha Mungu ni yule ambaye hajatumbukia katika mtego wa matamanio ya nafsi. Mtume SAW anawataja watu wanaoweza kuyakimbia na kuyapinga matamanio ya nafsi zao kwamba ni mashujaa wa umma wake. Anasema, watu mashujaa zaidi ni wale ambao wanaweza kuyashinda matakwa ya nafsi.

Ukweli wa mambo ni kuwa, kwa kadiri mtu anavyofuata matamanio ya nafsi yake ni kwa kiwango hicho hicho anapokuwa mbali na nguvu na irada ya akili. Kwa maana kwamba, uwezo wake wa kutumia akili hudhoofika kadiri mtu anavyokuwa ni mwenye kufuata na kuabudu matamanio ya nafsi yake.

 

Watu ambao wamezama na kuchupa mipaka katika kuabudu matamanio ya nafsi hukosa irada na nguvu ya kufanya mambo, kwa maana kwamba, huwa hawana irada katika kufanya mambo. Imam Ja'afar Sadiq AS anasema kuhusiana na hili kwamba: "Usiiache nafsi katika mikono ya matamanio ya nafsi; kwani matamanio ya nafsi ni sababu ya kifo cha nafsi; na kuipa uhuru nafsi katika matamanio ya nafsi husababisha maradhi na kuizuia na matamanio ya nafsi ndio tiba yake. "

Kwa hakika Aya za Qur'ani Tukufu zinazozungumzia matamanio ya nafsi zinaweka wazi msisitizo wa hali ya juu wa Uislamu kuhusiana na kukabiliana na matamanio ya nafsi. Aya za 40 na 41 za Surat Naaziat zinaeleza kwamba, kumuogopa Mwenyezi Mungu na kupambana na matamanio ya nafsi ni ufunguo wa kuingia peponi. Aya hizo zinasema:

Na ama yule anaye ogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuilia nafsi yake na matamanio, Basi huyo, Pepo itakuwa ndiyo makaazi yake!

Aghalabu matamanio ya nafsi na hali ya kutaka kumfuata Mwenyezi Mungu ni vitu viwili ambavyo haviwezi kukusanyika pamoja. Hii ni kutokana na kuwa, matakwa ya nafsi iliyokengeuka hayana mpaka wala mwisho. Lakini endapo mwanadamu atamtanguliza Mwenyezi Mungu mbele ya matakwa ya nafsi, basi Allah humpa izza na heshima mja huyu ya kutokuwa mhitaji kwa mtu yeyote yule.

Hivyo basi ili mwanadamu aweze kuyashinda matamanio ya nafsi anapaswa kufungamana kikamilifu na mafundisho ya Uislamu. Aidha ili aweze kutatua mikinzano na vile vile kubadilisha matamanio yake binafsi na kuyaelekeza katika vitu au mambo yanayostahiki anapaswa kumtanguliza Allah mbele ya matamnio ya nafsi. Kwa maneno mengine ni kuwa, mja asikubali kuburuzwa na matamanio ya nafsi, kama vile bendera inavyofuata upepo, bali achuje na kutia katika mizani kila jambo analotaka kulifanya ambalo nafsi imelitamani. Kipimo cjake kiwe ni hili swali kwamba, je hili ninalotaka kulifanya ambalo nafsi imelitamani linaridhiwa na Mwenyezi Mungu au la?

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha Hadithi ya Uongofu umefikia tamati kwa leo. Tukutane tena juma lijalo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh