Oct 01, 2016 04:12 UTC
  • Jumamosi, Oktoba Mosi, 2016

Leo ni Jumamosi tarehe 29 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja 1437 Hijria mwafaka na tarehe Mosi Oktoba 2016 Miladia.

Tarehe Mosi Oktoba huadhimishwa kote duniani kwa anuani ya Siku ya Wazee Duniani. Siku hii ilitengwa kwa ajili ya kuwakirimu na kuwaenzi watu wa tabaka hilo. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa hapa nchini Iran na kutokana na mabadiliko yaliyotokea baada ya Mapinduzi ya Kiislamu na ada na utamaduni unaotawala hapa nchini wazee na watu wazima wanapewa nafasi maalumu katika jamii. ***

Miaka 67 iliyopita katika siku kama ya leo, kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China kulitangazwa rasmi na Mao Tse Tung akachaguliwa kuwa kiongozi wa jamhuri hiyo. China yenye ustaarabu mkongwe, ilikuwa chini ya udhibiti wa madola ya Ulaya kuanzia mwishoni mwa karne ya 16. Mara kadhaa Wachina walianzisha vita dhidi ya mkoloni hasa Muingereza ili kuikomboa nchi yao lakini hawakufanikiwa. ***

Katika siku kama ya leo miaka 56 iliyopita nchi ya Nigeria ilipata uhuru. Wareno waliwasili Nigeria katika karne ya 15 na mkoloni Mwingereza naye akawasili katika nchi hiyo katika karne ya 16. Katika karne ya 17 Miladia ardhi ya Nigeria iligeuzwa na kuwa moja kati ya vituo muhimu vya biashara ya utumwa. Mwishoni mwa karne ya 19 vikosi vya Uingereza, viliidhibiti kikamilifu ardhi ya Nigeria. Mwaka 1914 Uingereza uliziunganisha nchi mbili za Nigeria ya Kaskazini na Kusini zilizokuwa chini ya udhibiti wake na kuunda koloni moja la Nigeria. Miaka 40 baadaye nchi hiyo ikajitangazia mamlaka ya ndani. Hatimaye baada ya kupitia misukosuko mingi, Nigeria ikajipatia uhuru katika siku kama ya leo. ***

Na miaka 31 iliyopita sawa na tarehe Mosi Oktoba mwaka 1985 ndege za kijeshi za utawala haramu wa Israel ziliyashambulia makao ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Tunisia. Watu wapatao 70 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa kufuatia mashambulio hayo. PLO ilikuwa imehamishia makao yake Tunisia kutoka Lebanon baada ya mashambulio ya kijeshi ya utawala haramu wa Israel nchini humo mwaka 1982. Hata hivyo uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo ulilifanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushindwa kuchukua hatua zozote za maana dhidi ya Tel Aviv.