Muharram, Mwanzo wa Historia
Assalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh. Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi katika kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kuanza mwezi mtukufu wa Muharram na harakati ya Bwana wa Vijana wa Peponi Imam Hussein bin Ali (as). Ni matarajio yangu kuwa mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Tumo katika siku za mwanzoni mwa mwezi wa Muharram ambao ni mwezi wa kwanza wa mwaka wa Hijria. Katika zama za utawala wa Khalifa Umar bin Khattab Waislamu na kwa pendekezo lililotolewa na Imam Ali bin Abi Twalib (as), walijaalia hijra na kuhama kwa Mtume Muhammad (saw) kutoka Makka kwenda Madina kuwa ndio mwanzo wa kalenda ya Kiislamu. Baadaye mwezi wa Muharram ulichaguliwa kuwa mwezi wa kwanza wa mwaka wa Kiislamu kutokana na sifa zake za kipekee. Kwa Waislamu wengi duniani hususan Waislamu wa madhehebu ya Shia, kuanza kwa mwaka mpya wa Hijria na mwezi wa Muharram hukumbusha harakati itakayodumu milele ya Imam Hussein bin Ali (as). Katika historia ya Uislamu mwezi wa Muharram huambatana na tukio la Ashuraa yaani tarehe 10 mwezi huu; tukio ambalo licha ya kupita karne kadhaa sasa tangu litukie, bado linaangaza na kuwamulikia njia wapigania haki, ukweli na uadilifu.
Sababu ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa Hijria Qamaria kupewa jina la Muharram ni kwamba, katika zama za ujahilia ilikuwa haramu na marufuku kupigana vita katika mwezi huu. Kwa utaratibu kwamba, watu walikuwa wakisimamisha na kuacha kupigani vita katika mwezi wa Muharram na amani na usalama ulitawala katika maeneo yote. Baadhi ya wafasiri wa Qur'ani Tukufu wanasema kuwa, suna na ada ya kukataza vita katika miezi minne ukiwemo huu wa Muharram, ilianza katika zama za Nabii Ibrahim (as). Suna na kanuni hiyo iliendelezwa katika zama za ujahilia na ikadumishwa na kuungwa mkono na Uislamu.

Kuharamishwa vita katika miezi hiyo ilikuwa mojawapo ya njia za kukomesha vita vya muda mrefu kati ya makabila ya Waarabu na wenzo wa kulingania amani, suluhu na utulivu. Kwani wakati wapiganaji walipokuwa wakiweka chini silaha zao kwa kipindi cha miezi minne walipata fursa ya kutafakari vyema, suala ambalo lilitayarisha mazingira ya kufanyika juhudi za upatanishi na kukomeshwa vita. Hata hivyo inasikitisha kuwa watawala waovu na madhalimu wa kizazi cha Bani Umayyah walivunja heshima na utukufu wa mwezi huu wa Muharram kwa kumwaga damu ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein bin Ali (as) katika mwezi huu na kusababisha maafa makubwa ya Karbalaa. Imam Ali bin Mussa al Ridhaa ambaye ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) amesema: Heshima ya mwezi huu ililindwa katika kipindi cha ujahilia na Waarabu hawakuwa wakipigana vita ndani yake. Lakini katika mwezi Muharram mwaka 61 damu yetu wana wa Muhammad (saw) ilimwagwa na heshima yetu ikavunjwa; watoto na wanawake wetu walichukuliwa mateka, mahema makachomwa moto, mali zikaporwa na heshima ya Mtume katika kizazi chake ikavunjwa."
Katika mwaka 61 Hijria Qamariya miaka 50 baada ya kuaga dunia Mtume Muhammad (saw), wakati hofu ya kutoweka Uislamu na Qur'ani ilipotanda ulimwengu wa Kiislamu kutokana na dhulma, ufuska na maovu ya watawala wa Bani Umayya, Imam Hussein bin Ali (as) alianzisha harakati ya mapambano ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu na mafundisho ya babu yake. Hussein bin Ali bin Abi Twalib ni mwana wa Fatima bint Muhammad (saw) na mjukuu wa Mtume wetu mtukufu ambaye daima alikuwa akisema: "Hussein anatokana na mimi, na mimi ninatokana na Hussein." Imam Hussein alitoa somo la ushujaa, uungwana na ujasiri kwa wanadamu wote na akaziamsha nyoyo zilizokuwa zimelala katika usingizi mzito kwa harakati yake katika medani ya Karbalaa. Kwa hakika Hussein (as) alihuisha mti wa Uislamu kwa kuunyesheleza kwa damu yake na masahaba zake wema waliouliwa shahidi huko Karbalaa.

Imam Hussein aliishi na babu yake Mtume Muhammad (saw) kwa kipindi cha miaka sita cha ototoni mwake na baada na hapo aliishi na baba yake, Amirul Muuminina Ali bin Abi Twalib (as) kwa kipindi cha miaka 30. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Hussein alikuwa bega kwa bega na kaka yake, Imam Hassan katika matukio yote muhimu ya kijamii na kisiasa ya wakati huo. Baada ya kufariki dunia Muawiya bin Abi Sufiyan mwaka 60 Hijria, mwanaye fasiki, muovu na dhalimu Yazid bin Muawiya alishika hatamu za uongozi na akamwamuru gavana wake katika mji mtakatifu wa Madina amlazimishe Imam Hussein kutoa mkono na baia na utiifu. Imam ambaye alikuwa akielewa vyema uovu na ufuska wa Yazid mlaaniwa, alikataa kumpa mkono wa utiifu na akakhitari njia ya mapambano dhidi ya utawala wake kwa ajili ya kunusuru Uislamu. Imam Hussein aliondoka Madina akielekea Makka na baadaye alipokea barua za Waislamu wa Iraq waliomwita huko na kumuahidi kushirikiana naye katika harakati ya mapambano dhidi ya mtawala huyo dhalimu. Kabla ya kufika Kufa huko Iraq, Imam Hussein (as) akiwa pamoja na watoto, familia na wafuasi wake alizingirwa na jeshi la Yazid katika ardhi iliyojulikana kwa jina la Karbala lakini alikataa kusalimu amri. Hatimaye tarehe 10 mwezi Muharram maarufu kwa jina la Ashuraa, Imam Hussein pamoja na masahaba zake waliuawa shahidi na kukatwa vichwa na jeshi la Yazid katika medani ya Karbalaa baada ya mapambano makali yaliyobakia hai katika historia ya mwanadamu.
Japokuwa harakati na mapambano ya Imam Hussein (as) ilishindwa kidhahiri katika vigezo vya kijeshi, lakini ilikuwa na baraka tele zilizoendelea katika vipindi mbalimbali vya historia. Miongoni mwa taathira kubwa za harakati ya mapambano ya Bwana wa Mashahidi Imam Hussein (as) ilikuwa ni kuwaamsha watu na kuwaondoa katika giza la ujinga, hofu na upotovu. Harakati hiyo ya Imam ilidhihirisha tena mpaka baina ya haki na batili uliokuwa umeanza kutoweka kutokana na mienendo ya watawala madhalimu waliovaa joho la Uislamu. Harakati hiyo ya kufuta ujinga na kuwazindua watu ya siku ya Ashuraa haikuwaamsha Waislamu pekee, bali iliwasha nuru na mwanga pia katika roho za wasio Waislamu. Kwa bahati nzuri mwanga wa harakati hiyo bado unaendelea kumulika katika njia ya wapenda haki na wapigania uhuru na uadilifu kote duniani.
Mwamko wa watu uliosababishwa na harakati ya Imam Hussein katika siku ya Ashuraa ulifuatiwa na harakati nyingi za kupigania haki na uadilifu katika zama hizo na miaka iliyofuata. Miongoni mwa harakati hizo zilizopata ilhamu katika harakati ya Ashuraa ni mapambano ya watu wa Madina dhidi ya utawala wa Yazid, harakati ya Tawwabin na mapambano ya Mukhtar. Harakati kama hizo za mapambano dhidi ya batili, dhulma na uonevu ziliendelea katika miaka iliyofuata. Hii ni kwa sababu Ashuraa iliweka misingi imara ya mapambano ya baadaye na kutoa wito wa kusima kidete dhidi ya dhulma na uonevu. Pamoja na hayo jambo lililoifanya harakati ya Ashuraa kuwa ya kipekee na kuwa na taathira kubwa zaidi katika fikra za wanadamu ni kwamba ilifanyika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake. Imam Hussein aliamua kusabilia nafsi, watoto, masahaba na kila alichokuwa nacho katika njia ya Mwenyezi Mungu na hakujali lolote katika njia hiyo. Hata wakati vita na mapigano yalipopamba moto na mwanaye aliyekuwa na umri wa miezi sita akauawa kwa kupigwa mshale wa shingo akiwa mikononi mwake, Imam alisema: "Nitastahamili yote yanayonipata maadamu yanafanyika mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu."

Miongoni mwa taathira za harakati ya Ashuraa ya Imam Hussein (as) ni kuzidisha moyo wa subra na ukakamavu, kwani kila Mwislamu au mwanadamu huru anaweza kuchota hisa yake katika hazina kubwa ya darsa na ibra za Ashuraa. Wafuasi wa Ahlul Bait na kwa ujumla wanadamu wote waliosoma na kulichunguza vyema tukio la Ashuraa katika medani ya Karbalaa wameathirika la subira na ukakamavu wa Imam Hussein (as) na masahaba zake waaminifu na humkumbuka mtukufu huyo na mapambano yake wakati wote wanapokumbwa na mashaka maishani mwao na kumfanya kigezo na ruwaza njema. Imam Hussein alizingirwa na maadui katika jangwa la Karbalaa kwa siku kadhaa bila ya maji akisumbuliwa na kiu yeye na Ahli yake. Maadui hao walimuua mtoto wake aliyekuwa na miezi sita mbele ya macho yake na wakamtatakata kwa mapanga mwanaye kijana, Ali al Akbar ambaye historia inasema alishabihiana sana na Mtume (saw) kwa umbo na tabia. Hata hivyo Imam Hussein (as) hakuacha kumshukuru na kumdhukuru Mola Muumba katika maafa hayo na alituliza majeraha ya roho yake kwa kumkumbuka Allah SW.
Kuwa huru na kujikomboa na kila kitu ghairi ya Allah ni miongoni mwa darsa na ibra za tukio la Ashuraa. Hivi sasa na baada ya kupita zaidi ya miaka elfu moja baada ya tukio la Karbalaa, sauti ya Imam Hussein akiwaambia maadui zake kwamba: "Kama hamna dini basi kuweni watu huru", ingali inasikika kote duniani. Mwangwi wa ujumbe huo wa Imam Hussein ungali unasikika na unawahimiza wafuasi wa mtukufu huyo na wanadamu wote kupinga na kukataa dhulma, ufuska na kudunishwa. Kwa msingi huo moja ya mafunzo muhimu ya harakati ya Imam Hussein (as) katika medani ya Karbalaa ni kuwa huru na kutokuwa mtumwa wa yeyote yule asiye kuwa Allah. Sifa hizi, mpenzi msikilizaji ndizo zilizoibakisha hai harakati ya Imam Hussein na kuifanya tochi inayomulikia wanadamu wote wenye dini na fikra tofauti katika kipindi chote cha historia.