Alkhamisi 3 Novemba, 2016
Leo ni Alkhamisi tarehe 3 Mfunguo Tano Safar 1438 Hijria sawa na Novemba 3, 2016.
Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume wa Uislamu Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharifu katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na alikuwa mashuhuri kwa elimu kubwa na maarifa, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama hizo. Kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu na mtu aliyebobea katika maarifa. Kipindi cha uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote kwa mnasaba huu adhimu wa kuzaliwa Imam Baqir (AS).

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, askari vibaraka wa utawala wa Shah uliokuwa ukitawala Iran waliivamia nyumba ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini mjini Qum na kumtia mbaroni. Baada ya kumhamishia mjini Tehran, utawala wa Shah ulimbaidishia Imam Khomeini nchini Uturuki. Utawala wa Shah uliamua kufanya hivyo kutokana na uungaji mkono wa Imam Khomeini kwa harakati za mapambano za wananchi Waislamu wa Iran za kutaka kujitawala, uhuru na kutetea thamani za Kidini. Lengo la kumpeleka uhamishoni Imam Khomeini lilikuwa kusimamisha mapambano yake na wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala huo kwani utawala wa Shah ulitambua kwamba kuwepo Imam nchini kunawaamsha wananchi dhidi ya utawala huo wa kidikteta.
Miaka 60 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, wakati wa mashambulio ya askari wa utawala dhalimu wa Israel dhidi ya Misri, wanajeshi wa utawala huo waliuvamia mji wa Khan Yunis katika Ukanda wa Gaza huko Palestina na kuwaua kwa umati wakazi wa mji huo. Baada ya kuukalia kwa mabavu mji huo, askari hao waliwanyonga askari 25 wa Kimisri. Unyama wa askari wa Israel haukuishia hapo, kwani waliishambulia hospitali ya mkoa mjini Khan Yunis na kuwaua kwa umati wauguzi, madaktari na wagonjwa wote waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo. Watu wapatao 275 waliuawa katika mashambulio hayo.
Miaka 38 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 13 Aban mwaka 1357 Hijria Shamsia, kulifanyika maandamano makubwa ya wanafunzi na wanachuo mjini Tehran. Maandamano hayo ya yalikandamizwa vibaya na askari wa utawala wa Shah na kusabbisha umwagaji damu mkubwa. Katika siku kama hii ambayo ilisadifiana na kumbukumbu ya kubaidishwa Imam Khomeini huko Uturuki, kundi kubwa la wanafunzi na wanachuo, wakiwa na lengo la kulaani kitendo hicho cha mfalme Shah walikusanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran. Askari wa utawala wa Shah walishambulia kundi hilo la wanachuo na wanafunzi na kuwauwa shahidi wanafunzi na wanachuo wengi. Tarehe 13 Aban ina umuhimu mkubwa katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, na ndio maana imepewa jina la "Siku ya Mwanafunzi."