Nov 07, 2016 07:58 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Nov 7

Mkusanyiko wa matukio kem kem ya spoti yalitoawala anga mbali mbali ndani ya siku saba zilizopita......................

Iran mabingwa wa dunia, mchezo wa Kutunisha Misuli 2016

Kikosi cha Iran cha mchezo wa kutunisha misuli kimetwaa ubingwa wa mashindano ya dunia ya mchezo huo mwaka huu 2016 yaliyofanyika nchini Uhispania. Timu hiyo ya Iran ya mchezo wa kutunisha misuli iliibuka kidedea baada ya kutwaa medali 3 za dhahabu, moja ya fedha na shaba moja katika mashandano hayo yaliyofanyika katika mji wa Benidorm, mashariki mwa Uhispania. Sayyid Rouhullah Mirnourullahi aliipa Iran ya Kiislamu dhahabu ya kwanza katika kitengo cha sentimita 168 huku mwenzake Mehdi Parvani akitia kibindoni dhahabu ya pili, safu ya sentimita 171. Dhahabu nyingine ya Iran ilitwaliwa na Kayvan Rezapour huku fedha na shaba zikinyakuliwa na Hesam Khosravi na Mohammad Reza Ja’fari kwa usanjari huo. Duru ya 11 ya mashindano hayo Mabingwa wa Kutunisha Misuli kwa upande wa wanaume ambayo pia ni duru ya 70 katika mahesabu ya shirikisho la mchezo huo International Federation of Bodybuilding and Fitness, ilianza Novemba 3 na kumalizika Novemba 7 nchini Uhispania, kwa kuwaleta pamoja wanamichezo 235 kutoka mabara tofauti.

Soka ya Ufukweni: Iran yaibuka ya 2 Kombe la Dubai

Timu ya taifa ya soka ya ufukweni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeubuka ya pili katika mashindano ya Kombe la Dubai ya mchezo huo mwaka huu 2016 huko Umoja wa Falme za Kiarabu UAE. Iran ilishindwa kufurukuta mbele ya Brazil siku ya Jumamosi katika mchuano wa fainali uliopigwa katika ufukwe wa Dubai International Marine Club na kukubali kichapo cha mabao 6-2 kutoka mibabe hiyo ya mpira wa miguu wa ufukweni ya Amerika Kusini. Mabao ya Iran katika fainali hiyo yalifungwa na Moslem Mesigar na Mohammad Ahmadzadeh. Vijana wa Iran walitinga fainali ya mashindano hayo baada ya kuikung'uta Tahiti mabao 8-6 siku ya Ijumaa. Russia iliifunga Tahiti mabao 4-3 na kuambulia nafasi ya tatu katika mashindano hayo ya kieneo. Duru ya sita ya mashindano hayo yanayojulikana kama Samsung Beach Soccer Intercontinental Cup Dubai 2016, ilianza Novemba 1 na kufunga pazia lake Novemba 5 mjini Dubai, huko Imarati.

Iran yashinda medali 2 za dhahabu Mashindano ya Wushu

Shahrbanou Mansourian

Mabingwa wa kike wa Iran katika mchezo wa wushu wameshinda medali 2 za dhahabu katika duru ya 6 ya Mashindano ya Kimataifa ya mchezo huo yaliyofanyika huko China. Siku ya Jumamosi, Shahrbanou Mansourian aliipa Iran medali ya dhahabu katika kategoria ya wanamichezo wenye kilo zisizodidi 65, baada ya kumsasambua Mfilipino Hergie Bacyadan kwa pointi 2-1. Mapema siku hiyo Muirani mwingine Sedigheh Dariaeivarkadeh alijishindia medali ya dhahabu baada ya kumlemea Nguyen Thi Trang wa Vietnam, katika kitengo cha kilo zisizozidi 60. Mashindano hayo yalianza Novemba 4 na kumalizika Novemba 6, katika mji wa Xi’an, nchini China.

Mwezi Novemba mwaka jana, wanariadha wa kike wa Iran walijishindia medali 3 za dhahabu katika Mashindano ya Kimataifa ya Mchezo wa Wushu, yaliyofanyika katika mji mkuu wa Indonesia, Jakarta. Wushu ni mchezo ulioibukia China mwaka 1949, unaojumuisha kwa kiasi fulani masumbwi, mieleka na taekwondoh, ingawa mbinu nyinginezo mpya zimekuwa zikijumuishwa kwenye mchezo huo kila leo.

TP Mazembe mabingwa Kombe la Shirikisho

Klabu ya soka ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndiyo mabingwa wa Kombe la Shirikisho barani Afrika mwaka 2016.

Klabu ya soka ya TP Mazembe ya DRC wakisherehekea ushindi

Hii ni baada ya kuichabanga Mo Bejaia ya Algeria mabao 4-1 katika fainali ya pili iliyochezwa Jumapili jioni katika uwanja wa Kamalondo mjini Lubumbashi huko DRC. Kiungo Rainford Kalaba raia wa Zambia alipachika nyavuni mabao 2 ya Mazembe hivyo kutawazwa kuwa mfungaji bora katika mashindano haya kwa kutikisa nyavu mara 8. Kwa ujumla, Mazembe walipata ushindi wa mabao 5-2 ikizingatiwa kuwa fainali ya kwanza walitoka sare bao 1-1 walipocheza ugenini. Mbali na kunyanyua kombe hilo maarufu kama Confederation Cup, Mazembe imetia kapuni zaidi ya laki 6 na nusu za Marekani huku mshindi wa pili Mo Bejaia ikitia kibindoni zaidi ya dola laki nne na nusu. Kibarua kinachowasubiri vijana wa Mazembe ni fainali ya Kombe la Super watakapomenyana na klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyoshinda taji la klabu bingwa barani Afrika msimu huu.

Riadha: Keitany wa Kenya ashinda New York Marathon

Mwanariadha wa Kenya Mary Keitany ameng'ara na kupeperusha bendera ya taifa yake katika mbio za New York Marathon kwa upande wa wanawake, kwa kutumia masaa mawili, dakika 24 na sekunde 26. Keitany anakuwa mwanamke wa kwanza kushinda mbio hizo za Marekani mara tatu mfululizo katika kipindi cha miongo mitatu. Bingwa wa dunia kutoka Eritrea Ghirmay Ghebreslassie, alimshinda Mkenya Lucas Rotich mbio za wanaume na kuwa mshindi wa New York Marathon kwa kutumia muda wa masaa 2:07:51.

Ligi ya EPL

Debi la kukata na shoka la mahasimu wa London Kaskazini ndilo lililozungumziwa zaidi mwishoni mwa wiki na imebainika kuwa, mibabe hiyo ya soka Uingereza inatoshana nguvu. Licha ya kuchezea nyumbani Emirates, Arsenali ilikubali kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Tottenham katika kipute hicho cha Jumapili. Nusura Gunners waambulie patupu, lakini Kevin Wimmer wa Spurs akawanusuru kwa bao alilojifunga katika dakika ya 42.

Klabu ya Liverpool (jezi jeupe) inaongoza EPL kwa sasa

Mchezaji Harry Kane ambaye alikuwa na jeraha la kifundo cha mguu alirejea dimbani kwa bao la penati lililoiwezesha Hotspurs kubaki kuwa timu pekee ambayo haijashindwa mpaka sasa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza kunako dakika ya 51. Kwengineko, Man U waliisasambua Swansea mabao 3-1 wakati ambapo mabingwa watetezi Leicestar walikuwa wakiendeleza msururu wa kutandikwa msimu huu, kwa kunyukwa mabao 2-1 na Westbrom. Chelsea waliinyeshea Everton mabao 5-0 huku Watford ikikubali kichapo cha mbwa cha mabao 6-1 kutoka Liverpool.

Liverpool imetuama kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 26 huku The Blues ikifuata kwa karibu na pointi 25. Man City ambao walilazimishwa sare ya 1-1 na Middlesbrough, kwa sasa italazimika kutosheka ba nafasi ya tatu ikiwa na alama 24, pointi sawa na Arsenal ingawa wanatofautiana kwa idadi ya magoli.

 ................................................TAMATI...........................................