Dec 06, 2016 11:04 UTC
  • Familia Salama (17)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Familia salama. Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala ya leo tutaangazia umuhimu wa safari na matembezi katika familia. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.

Kustarehe na kuburidika ni kati ya mahitaji muhimu katika maisha ya mwanadamu. Kila mwanadamu, kwa kutegemea hali na umri wake huwa anapenda kubadilisha hali yake ya maisha ya kila siku na kupata jambo lenye kumsisimua na kumfurahisha. Kwa msingi huo, kilicho na umuhimu hapa ni kuainisha na kutambua ni aina gani za starehe zinazopaswa kuwepo katika familia.

Michezo, matembezi, safari, kutembelea jamaa na marafiki ni kati ya mambo yanayoweza kufanyika wakati wa mapumziko na hivyo kuleta uchangamfu katika familia.

Kuhusu ulazima wa mwanadamu kuwa na starehe na burudani, Mtume Muhammad SAW alisema:

"Jihusisheni na harakati za burudani na michezo kwani sipendi kuona utumiaji mabavu katika dini. "

 

Baadhi ya burudani sahali ambazo wengi wanaweza kujihusisha nazo ni kama vile kutembelea kwenye mabustani, maeneo kama vile fukwe za bahari na mito, misitu isiyo hatari n.k. Kwa kutembelea maeneo kama hayo, mwanadamu huweza kupata utulivu wa moyo hasa baada ya siku kadhaa za kazi na jitihada mbali mbali.

Katika siku ya mapumziko au wikendi, wanafamilia wanaweza kutembelea maeneo kama hayo tuliyoyataja na wakiwa hapo kuzungumzia masuala yao mbali mbali na hilo huweza kuimarisha mahaba na ukuruba zaidi baina yao.

Familia nyingi hupenda safari fupi fupi ambazo hazina gharama kubwa lakini zilizojaa furaha na burudani. Moja ya njia za kupunguza gharama za safari kama hizo ni kubeba chakula  na kukila eneo la wazi nje ya nyumba yaani pikniki na hilo pia huimarisha mapenzi na mahaba miongoni mwa wanafamilia. Katika mazingira kama hayo wanafamilia huweza kucheza pamoja na kupata burudani za aina mbali mbali na hilo hubakia katika kumbukubu za wanafamilia hasa watoto.

Aidha wakati wazazi wanapotaniana na watoto wakiwa katika burudani kama hizo, jambo hilo huwafanya watoto wawatizame wazazi kama marafiki na hivyo kuimarisha mapenzi na ukuruba baina yao.

Iwapo wanafamilia watafanya shughuli zao wanazozikariri kila siku iwe ni kazi au masomo na kisha kurejea nyumbani na hali hiyo kujirudia kwa muda mrefu, huibua uchovu wa kiakili na hivyo kuna haja ya kuwa na shughuli au harakati za nje ya nyumba zenye lengo la kustarehe au kuburudisha kwa njia halali na  zisizo kinzana na mafundisho ya dini.

Aidha mbali na kutumia wakati wa likizo au wikendi katika burudani, wanafamilia wanaweza kutumia wakati huo kuelekea katika sehemu za ibada zilizo mbali au karibu. Kwa msingi huo kuna haja ya kujengwa misikiti au maeneo mengine ya ibada yenye suhula mbali mbali ambazo watoto, mabarobaro   au hata watu wazima wanaweza kuzitumia kwa ajili ya michezo na burudani zinginezo halali  ili wakishamaliza michezo yao waweze kutekeleza ibada. Jambo kama hili litawawezesha kuwa na mazoea ya kuelekea msikitini au maeneo mengine ya ibada mara kwa mara.

Unaposafiri unajifunza mambo mengi

 

Aidha wazazi wenye uwezo wanapaswa kuwapangia wanafamilia wote safari katika maeneo ya kitalii hasa kwa kuzingatia kuwa nchi nyingi za Kiafrika zina vivutio ving vya kitalii hasa mbuga za wanyama na milima. Hivi sasa serikali nyingi za Afrika zina mipango maalumu ya kuwavutia watalii wa ndani ya nchi ili kuondoa ile dhana kuwa vivutio vya kitalii ni vya wageni pekee. Aidha kuna athari nyingi za kihistoria katika nchi za Afrika hasa katika pwani ya Afrika Mashariki na hayo ni kati ya maeneo ambayo wanafamilia wenye uwezo wanaweza kuyatembelea ili  kujifunza kuhusu historia hasa ya ustaarabu wa Kiswahili.

Hali kadhalika miji mingi ya Afrika Mashariki ina majengo ya makumbusho au museum na hayo ni kati ya maeneo mazuri ya kutembelea ambayo kiingilio chake huwa si ghali na wengi wanaweza kujimudu. Majumba hayo huwa na mengi ya kujifunza kuhusu historia ya nchi ambayo hata wanaotembelea huyasoma katika vitabu vya shuleni. Kwa hivyo kutembelea jumba la makumbusho mbali na kuwa sehemu ya burudani ya familia kunaweza pia kuwa na faida nyingi za kimasomo.

Kwa ujumla ni kuwa safari huwa ni nafasi muhimu katika kumpumzisha mwandamu kiakili na kumpunguzia mashinikizo ya kiroho. Safari hata kama itakuwa fupi huondoa ile hali ya maisha ya kujikariri kila siku na hivyo kumpa mwenye kusafiri nishati na ari mpya.

Wanafamilia wanaposafiri wote kwa pamoja hiyo huwa ni fursa ya wao kuwa na ukuruba na kukaa pamoja kwa muda mrefu na hilo bila shaka huimarisha mahaba na mapenzi miongoni mwao.

Unaposafiri unapata fursa ya kuona mambo mengi

 

Katika safari kama hizo wanaosafiri hupata fursa ya kula pamoja na katika baadhi ya maeneo kutembea pamoja na kumbukumbu za safari kama hizo zikihifadhiwa  kupitia picha n.k huleta hisia za mapenzi wakati zinapotizamwa katika miaka ya baadaye.

Kwa hakika tokea jadi, safari zimekuwa zikimpa mwandamu fursa ya kuvumbua mambo mapya, kuwafahamu watu wapya na kujifunza kuhusu mila na desturi za wengine. Mtume Mtukufu wa Uislamu amesema hivi kuhusu safari: "Hata kama katika safari hautapata faida za kifedha, kwa yakini utaweza kujifunza mengi."

 

Tags