Ijumaa tarehe 09 Disemba, 2016
Leo ni Ijumaa tarehe 9 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na tarehe 9 Disemba 2016 Milaadia.
Tarehe 9 Rabiul Awwal mwaka 260 Hijria ilikuwa siku ya kwanza ya uongozi wa Imam wa Zama Mahdi (as), Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake. Imam wa Zama alishika hatamu za uongozi baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Hassan Askari (as). Imam Mahdi (as) amekwenda ghaiba kwa amri ya Mwenyezi Mungu na atadhihiri katika kipindi cha zama za mwisho za dunia na kuijaza dunia haki na uadilifu kama zinavyosema hadithi sahihi zilizopokewa na wanazuoni mashuhuri wa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu.
Tarehe kama ya leo mwaka 1961 ardhi ya Tanganyika ambayo hii leo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilijikomboa na kupata uhuru. Tanganyika ilianza kukoloniwa na Ujerumani mwaka 1880 hadi mwaka 1919 wakati ilipoanza kukoloniwa na Uingereza na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa mkoloni huyo hadi ilipojipatia uhuru wake wa kujitawala katika tarehe kama ya leo. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na baadaye akachaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika.
Siku kama hii ya leo miaka 29 iliyopita, yalianza mapambano yasiyo na kikomo ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza. Mapambano hayo ya ukombozi ambayo ni mashuhuri kwa jina la "Intifadha ya Kwanza" yalianzishwa baada ya kushadidi mauaji na ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina na pia kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi zao na utawala huo ghasibu. Hayo yalijiri baada ya wananchi Waislamu wa Palestina kukatishwa tamaa na hatua zilizokuwa zikichukuliwa na nchi za Kiarabu na taasisi nyingi za Palestina kwa ajili ya kurejeshewa haki zao.
Siku kama ya leo miaka 274 iliyopita Carl Wilhelm Scheele mwanakemia mashuhuri wa Sweden na mmoja kati ya waasisi wa elimu ya kemia ya leo alizaliwa huko Stockholm mji mkuu wa nchi hiyo. Mwanakemia huyo aliendelea na masomo yake kutokana na jitihada na hamu yake kubwa aliyokuwanayo licha ya familia yake kuwa duni. Carl Wilhelm ambae aliishi katika zama za kuchanua kwa elimu ya kemikali, mwezi Oktoba mwaka 1772 alifanikiwa kugundua gesi ya chlorine baada ya juhudi za miaka mitano. Gesi hiyo ni moja kati ya mada muhimu za kemikali na inatumika sana viwandani. Mbali na hayo mwanakemia huyo aligundua pia manganese na Glicerine.
Na miaka 258 iliyopita vita vya Madras vilianza na kudumu kwa miezi 13. Vita hivyo vinahesabiwa kuwa mojawapo ya vita vikali zaidi vya kikoloni kati ya Uingereza na Ufaransa huko India. Vita hivyo vilianza baada ya Ufaransa kuishambulia bandari ya Madras huko kusini mwa India, ambayo ilikuwa ikidhibitiwa na Waingereza. Ufaransa ilipigana ikiwa na wanajeshi elfu tatu dhidi ya Uingereza iliyokuwa na wapiganaji elfu 22. Mwezi Januari mwaka 1761, Ufaransa ilisalimu amri mbele ya Uingereza baada ya kikosi cha dhiba kushindwa kufika vitani