Dec 14, 2016 04:23 UTC
  • Jumatano, Disemba 14, 2016

Leo ni Jumatano tarehe 14 Mfunguo Sita Rabiul Awwali 1438 Hijria sawa na Disemba 14, 2016.

Miaka 1374 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 14 Mfunguo Sita mwaka 64 Hijria, Yazid bin Muawiya alikufa huko Sham (Syria ya leo) baada ya kutawala kwa muda wa miaka mitatu na miezi tisa. Katika mwaka wa kwanza wa utawala wake wa kidhulma, Yazid bin Muawiya alitoa amri ya kuuliwa kikatili Imam Husain AS, mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW pamoja na wanawe na wafuasi wake watiifu katika jangwa la Karbala. Katika mwaka wa pili wa ukhalifa wake, aliwaua kwa umati wakazi wa mji mtukufu wa Madina na katika mwaka wa mwisho wa utawala wa Yazid, mji mtakatifu wa Makkah ulizingirwa na Masjidul Haram ikaharibiwa. Kabla ya kutwaa madaraka kwa nguvu, Yazid bin Muawiya bin Abi Sufyan alikuwa ameghiriki katika maasi na maisha ya anasa na hakuwa na utambuzi wowote juu ya misingi na mafundisho ya Kiislamu. Waislamu walimchukia sana Yazid kutokana na dhulma na ukatili mkubwa aliowafanyia Watu wa Nyumba toharifu ya Bwana Mtume Muhammad SAW na wapenzi wa Ahlul Bait AS na kutokana na jinai zake nyengine nyingi.

Siku kama ya leo miaka 211 iliyopita, yaani tarehe 14 Disemba 1805, mhunzi George Branclon wa Uingereza aligundua nishati ya mkaa mawe. Kabla ya hapo, makaa ya mawe yalikuwa yakitumiwa kama mojawapo ya vifaa vya kujengea nyumba. Shehena ya kwanza ya madini ya makaa ya mawe yaliyotumiwa katika nishati ya kutia joto, ilipatikana katika bandari moja iliyoko Uingereza.

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita inayosadifiana na tarehe 14 Disemba 1981, Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel, lilichukua uamuzi wa kuunganishwa milima ya Golan ya Syria na ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Utawala huo ghasibu ulighusubu ardhi hizo za Syria, katika vita vya mwaka 1967 kati ya Israel na Waarabu. Hadi sasa yamefanyika mazungumzo kadhaa yenye shabaha ya kurejeshwa milima hiyo ya Syria kutoka katika makucha ya utawala ghasibu wa Israel.

Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, inayosadifiana na 14 Disemba 1995, yalithibitishwa kwa mara ya mwisho makubaliano ya amani ya Bosnia yaliyojulikana kwa jina la makubaliano ya Dayton katika kikao kilichofanyika Paris, Ufaransa. Makubaliano hayo ambayo yalifanyika kwa mashinikizo ya viongozi wa Marekani tarehe 21 Novemba 1995, yalitiwa saini na viongozi wa Waislamu, Waserbia, na Wacroatioa wa Bosnia. Mafanikio pekee ya makubaliano hayo kwa upande wa Waislamu, yalikuwa ni ukomeshwaji wa mauaji ya halaiki na ukandamizaji uliokuwa ukifanywa na Waserbia ambao katika kipindi hicho waliwauwa Waislamu wasiopungua laki mbili na nusu.

Rais wa Serbia, Slobodan Milošević (kushoto) , Rais wa Bosnia, Alija Izetbegović (katikati) na Rais wa Croatia Franjo Tuđman

Na siku kama ya leo miaka 470, inayosadifiana na 14 Disemba 1546, alizaliwa Tycho Brahe mnajimu na mwanahisabati wa Denmark. Kwa miaka kadhaa msomi huyo alipata elimu na kufanya utafiti nchini Ujerumani, na kugundua nyota mpya kwa njia ya falaki.

Tycho Brahe