Dec 17, 2016 04:25 UTC
  • Jumamosi, 17 Desemba 2016

Leo ni Jumamosi tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na tarehe 17 Desemba 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 491 iliyopita kwa mujibu wa nukuu na kauli za maulama wengi wa Kiislamu, alizaliwa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Makka. Baba yake, Abdullah alifariki dunia kabla ya kuzaliwa Mtume na mama yake, Amina binti Wahab, alifariki dunia mtukufu huyo akiwa na umri wa miaka sita. Katika kipindi cha mwanzoni mwa ujana wake Muhammad alikuwa akijitenga na jamii ya kijahilia ya watu wa Makka na kwenda kwenye pango la Hiraa lililoko karibu na mji wa Makka na kuketi huko kwa masaa kadhaa akitafakari katika maumbile ya dunia na kufanya ibada. Malaika Jibrilu alimteremkia mtukufu huyo akiwa katika pango hilo na kumpa ujumbe wa Mola Muumba. Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) alikumbana na mashaka mengi katika jitihada zake za kufuta ibada ya masanamu na kueneza imani ya Tauhidi na kumwabudu Mungu Mmoja. 

Katika siku kama ya leo miaka 1355 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa mjukuu wa Mtume saw, Imam Ja'far Swadiq (as) katika mji mtakatifu wa Madina. Kipindi cha maisha yake kilikuwa zama za kuchanua elimu na maarifa, tafsiri ya Qur'ani na kuenea elimu mbalimbali. Imam Swadiq (as) alitumia fursa hiyo ambayo ilisadifiana na kuanza kuporomoka utawala wa Bani Umayyah na kuchukua madaraka utawala wa Bani Abbas, kwa ajili ya kueneza maarifa asili ya Kiislamu na kulea kizazi cha wasomi na maulama katika nyanja mbalimbali. Kwa minasaba hii adhimu Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran inatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote duniani. 

Miaka 113 iliyopita katika siku kama ya leo, ndege ya kwanza duniani iliyokuwa ikitumia injini ya mota, ilifanikiwa kuruka na kupaa angani kwa dakika moja baada ya kufanyiwa majaribio kadhaa. Ndege hiyo ilitengenezwa na ndugu wawili walioitwa Wilbur Wright na Orville Wright na kufanyiwa majaribio katika jimbo la North Carolina nchini Marekani. Ndugu hao wawili walikuwa watengeneza baiskeli ambao baadaye walipata shauku kubwa ya kutengeneza ndege yenye kutumia injini ya mota.

Ndugu wawili, Wilbur Wright na Orville Wright

Katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, Dakta Muhammad Mufattih alimu na msomi mwanamapambano wa Kiirani aliuawa shahidi na magaidi waliokengeuka na waliokuwa na fikra potofu. Baada ya kumaliza masomo ya awali alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha mjini Qum Iran ambapo sambamba na kusoma masomo ya kidini alikuwa akisoma pia katika Chuo Kikuu cha Tehran ambapo alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika falsafa. Daka Mufattih alikuwa na nafasi muhimu katika harakati za mapinduzi za ya Kiislamu nchini Iran.

Daka Muhammad Mufattih

Na katika siku kama ya leo miaka 6 iliyopita, kijana mmoja wa Kitunisia kwa jina la Tarek el-Tayeb Mohamed Bouazizi alijiteketeza kwa moto na kuanzisha harakati ya ukombozi wa wananchi wa nchi hiyo dhidi ya utawala wa kidikteta wa Habib Bourguiba na Zainul Abidin bin Ali uliodumu kwa kipindi cha nusu karne. Kujichoma moto kwa Bouazizi ilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Tunisia na katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi. Bouazizi ambaye alikuwa na shahada ya chuo kikuu alikuwa akiuza bidhaa za mkononi mitaani aliponyanganywa bidhaa zake na kudhalilishwa na afisa wa kike wa Halmashauri ya Mji na ndipo alipoamua kujiteketeza kwa moto, kitendo ambacho kiliamsha hasira za wananchi wa Tunisia na kuwa chachu ya harakati iliyohitimisha utawala wa dikteta Zainul Abidin. Dikteta huyo alikimbia nchi na kwa sasa anapewa hifadhi na watawala wa kifalme wa Saudi Arabia.

Tarek el-Tayeb Mohamed Bouazizi