Mar 01, 2016 11:46 UTC
  • Uislamu Chaguo Langu (96)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huwaangazia watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina huamua kufuata njia ya haki maishani yaani Uislamu. Katika makala yetu ya leo tutamuangazia Mtaliano aliyesilimu Sara Teras.

Sara Teras anaanza kusimulia kisha cha kusilimu kwake kwa kusema: "Mimi nina umri wa miaka 29 na nimesoma tiba ya maradhi ya mifugo na katika familia yangu, mimi na baba yangu tulikuwa Wakristo na mama yetu Myahudi."
Bi. Teras anaendelea kusema: "Tokea ujanaani kwa ujumla nilikuwa nikivaa mavazi ya heshima pasina kujua chochote kuhusu Uislamu. Katika dhifa zote nilizohudhuria nilijitahidi kuvaa mavazi ya heshima kwani nilikuwa nikipata utulivu. Wakati huo nilikuwa sijawahi kumuona Mwislamu yeyote kwa karibu na wala sikuwa nikiujua Uislamu. Kile ambacho nilikuwa nimesikia kuhusu Waislamu ni kuwa Uislamu unawadhulumu wanawake na kwamba wanaume Waislamu huwatumia wanawake kama watumwa. Lakini sasa baada ya kufanya utafiti wa kina nimefikia natija kuwa nilikuwa na dhana potofu kuhusu Uislamu. Nimefurahi sana kwa sababu nimeweza kufahamu haki."
Sara anasema akiwa barobaro alivutiwa sana na masuala ya kidini. Pamoja na hayo yalimuibukia masuala mengi kuhusu dini na maisha. Anaendelea kusema: "Fitra na maumbile asilia ya wanaadamu wote ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kuvutiwa na dini ni hisia iliyo katika wanaadamu wote. Kumuamini Mwenyezi Mungu na dini ni hitajio ambalo iwapo litakidhiwa kwa njia sahihi, basi mwanaadamu atapata usalama na utulivu. Mimi pia nilikuwa nikitafuta jibu kuhusu hitajio hili. Lakini pamoja na utafiti wote niliofanya kuhusu dini mbali mbali sikuweza kufikia natija bali maswali mengi zaidi yaliibuka na hapo nilichanganyikiwa zaidi," anasema mwanamke huyu Mtaliano aliyesilimu. Bi. Sara anafafanua hapa kuhusu cheche ya kwanza iliyopelekea aelekee katika nuru ya Uislamu kwa kusema: "Mimi sikuwa nikimjua Mwislamu yeyote wala cheche ambayo ingenipa hamu ya kuujua Uislamu. Hali hii iliendelea hadi wakati nilipoingia katika chuo kikuu. Nilivutiwa sana kuona wanafunzi kutoka matabaka na dini mbali mbali. Nilishangaa sana baada ya kujuana na wanafunzi kadhaa na kuona mienendo yao. Hapo chuoni nilijuana na mtu ambaye tabia yake ilinistaajabisha. Alikuwa tofauti na wengine kutokana na sifa zake za kuwa mkweli, mcha Mungu na mnyenyekevu. Lakini sikuwa nikijua kuwa yeye ni Mwislamu. Kwa hakika ninaweza kusema kuwa nilianza kuiga tabia yake. Baadaye niliweza kufahamu kuwa ni Mwislamu na hivyo baadhi ya marafiki zangu walinitaka nijiweke mbali naye. Lakini mimi sikuwa na sababu ya kufuata maagizo waliyonipa kwani nilimtazama kama mtu mtakasifu na aliyekuwa na tabia bora kuliko mtu mwingine yeyote niliyekuwa nimewahi kukutana naye. Nilimuuliza kuhusu baadhi ya fikra na tabia zake nzuri. Alinijibu kwa kusema dini yake ndio chanzo cha hayo yote. Jambo lililonishangaza ni kuwa maneno na mienendo yake ilikuwa tofauti kabisa na yale niliyokuwa nimeyasikia kuhusu Uislamu. Nilimtaka anifahamishe zaidi kuhusu Uislamu na kwa njia hiyo niliweza kuujua Uislamu."
@@@@
Mtaliano aliyesilimu, Bi. Sara Teras aliweza kuufahamu Uislamu kupitia kujuana na Mwislamu aliyekuwa akitekeleza mafundisho ya dini hii tukufu. Hapo Bi. Sara alibadilisha taswira potofu aliyokuwa nayo kuhusu Uislamu na kwa msingi huo akaanza kufanya utafiti na uchunguzi kuhusu dini hii tukufu. Hapo tunaweza kusema kuwa kujuana kwake na Mwislamu mwenye imani kamili kulitoa msaada mkubwa kwake katika kuujua kwa kina zaidi Uislamu. Akiwa katika utafiti wake, kila wakati lilipomjia swali alimuuliza rafiki yake Mwislamu. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Uislamu ni dini ambayo inaenda sambamba na maumbile asilia au fitra ya mwanaadamu na kila mwanaadamu ambaye kweli anatafuta uhakika basi Mwenyezi Mungu humuongoza katika njia ya haki. Mimi pia kwa msaada wake Mwenyezi Mungu niliondoka katika mkondo potofu na kufuata njia sahihi ya Uislamu."
Bi. Sara Teras katika kujibu swali hili kuwa, "Je, awali uliposilimu haukuona ugumu katika kutekeleza ibada za faradhi katika dini,"? Na, Je uliwahi kujuta kuhusu uamuzi wako wa kusilimu? Alijibu kwa yakini na kusema: "Kamwe sijawahi kujuta. Kwa hakika niliposilimu nilihisi kana kwamba nimezaliwa upya na niliweza kufikia utulivu na hivyo sikuwa na wasi wasi tena na kile kinachonishughulisha ni kumridhisha na kumfurahisha Mwenyezi Mungu. Kila ninaposoma Qur'ani huweza kupata utulivu kamili. Aya za Qur'ani zina maajabu mengi na zimeweza kujibu maswali yote niliyokuwa nayo na zimeweza kunikurubisha zaidi katika Uislamu."
Mtaliano huyu aliyesilimu anaongeza kuwa: "Qur'ani ndio njia bora ya kujifunza kuhusu Uislamu. Kwa hakika Qur'ani ndicho kitabu bora zaidi cha kumuongoza mwanaadamu."
Kutokana na kuenea Uislamu miongoni mwa wakaazi asili wa Ulaya, wataalamu wa nchi hizo za Magharibi wangali wanafanya utafiti kuhusu suala hilo. Baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa kusilimu wanawake wa Ulaya ni kwa sababu ya kuporomoka maadili na watu kupoteza utambulisho wao katika jamii za Magharibi na Ulaya. Wataalamu wanaamini kuwa kwa mtazamo wa kisaikolojia wanawake huwa wanataka himaya na hii ni himaya ambayo ipo katika mafundisho ya Kiislamu. Wanawake wa nchi za Magharibi wameona namna ambavyo anasa, ufuska na ufisadi ulivyoshusha hadhi yao ya kimaanawi na hivyo wametambua kuwa Uislamu ndilo kimbilio pekee la mwanaadamu mwenye kutafuta umaanawi na utulivu wa moyo.
Shahid Murtadha Mutahhari, mwanafasafa na mwanafikra maarufu wa Kiislamu anasema hivi: "Moja ya sifa za kipekee za Uislamu ni kuwa dini hii inatambua uwezo na sifa maalumu za mwanamke na mwanaume. Kila mmoja wao ana uwezo wake wa ubunifu kwa maslahi ya ustawi wa jamii na wote wanaweza kushirikiana lakini katika mazingira salama, takasifu na ya kimantiki ili kuepusha jamii kupotea na kutumbukia kwenye upotofu na ufuska wakati wa kuelekea katika saada."
Bi. Sara Teras anasema alianza kuvaa hijabu ya Kiislamu punde baada ya kusilimu na anaongeza kuwa anaamini Uislamu si tu kuwa si kizingiti katika harakati zake za kijamii bali sasa anaendelea na kazi zake akiwa na usalama na utulivu zaidi kutokana na stara ya Hijabu. Mtaliano huyu aliyesilimu anasema Hijabu ni jambo la wajibu katika kuilinda jamii kutokana na ufisadi na ufuska. Anaongeza, baada ya kuslimu alitambua vyema namna inavyoenezwa taswira potofu kuhusu Waislamu na Uislamu na anamaliza kwa kusema: "Mimi nina fakhari kubwa sana kuwa Mwislamu na dini hii tukufu imeniletea utulivu na furaha tele."

Tags