Mar 01, 2016 11:53 UTC
  • Uislamu Chaguo Langu (98 - Mwisho)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huwaangazia watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina huamua kufuata njia iliyojaa nuru maishani yaani Uislamu. Katika makala ya leo tutamuangazia Mmarekani aliyesilimu Thomas Clayton. Karibuni.


Thoma Clayton alisafiri katika mojawapo ya nchi za Kiislamu ambapo alivutiwa sana na mandhari ya Waislamu wakisali sala ya jamaa na papo hapo akapata ilhamu na hatimaye akaamua kusilimu. Clayton anaanza kusimulia alivyosilimu kwa sentensi hii:  "Nilivutiwa sana na mandhari ya Waislamu wakiswali sala ya jamaa pembizoni mwa shamba kubwa na maridadi la kijani kibichi.


Jua lilikuwa limewaka wakati wa adhuhuri. Nilikuwa nikipita katika barabara na mara nikasikia sauti maridadi sana katika eneo hilo. Nilikuwa nikipita kati kati ya miti na hapo nikaona mandhari maridadi na ya kuvutia sana. Nilimuomna Muislamu akipaza sauti katika mnara wenye mvuto ambao ulikuwa umejengwa kwa mbao.  Hapo bila kujua nilihisia roho yangu yote ikivutiwa kwa njia ya ajabu. Maneno kama vile Allahu Akbar na la Ilaha ila Allah (hakuna apasaye kuabudiwa ila Allah) yalifika katika masikio yangu. Sikuwa nikifahamu ni nini kitakachofuata baada ya maneno hayo. Hatua kwa hatua niliona watu wakianza kujumuika katika eneo hilo. Watu wa marika mbali mbali walifika hapo na kukaa kwa pamoja huku wakiwa wanaheshimiana. Kila mmoja wao alikuwa na mkeka alioutandika katika uwanja uliokuwa na nyasi za kijani kibichi. Hatua kwa hatua idadi ya watu ilizidi kuongezeka. Niliona watu wakivua viatu vyao na kuketi kwenye mistari mirefu isiyopinda. Nilitazama mandhari hiyo nikiwa nimenyamaza kimya. Nilishangaa kuona kuwa watu wote pasina kujali tabaka walikuwa pamoja. Miongoni mwao kulikuwepo wazungu, watu kutoka Asia na watu kutoka Afrika. Wote waliketi pamoja. Kwa hakika nilihisi udugu uliokuwepo katika mjumuiko huo. Moyo wa udugu katika mjumuiko huo uliacha athari ambayo nitaendelea kuihisi milele. Imepita miaka mingi sasa tokea wakati huo.  Mwaka wa tukio hilo niliamua kusilimu na kubadilisha jina langu na sasa ninajulikana kama Mohammad."


Wapenzi wasikilizaji, Uislamu ni dini hai ambayo inaenda sambamba na fitra ya mwanaadamu na ndio dini pekee ambayo inaweka wazi njia ya saada ya mwanaadamu katika sekta zote. Ni kwa sababu hii ndio kila siku tunashuhudia kuongezeka idadi ya watu wanaosilimu. Hawa ni watu ambao wanataka kutambua falsafa sahihi ya maisha ili waweze kupata hadhi ya kukidhi mahitaji yao ya kiroho.


Hivi sasa tunashuhudia idadi kubwa ya watu duniani wakivutiwa na dini hii. Muelekeo huu unaashiria jibu muafaka kwa hitajio la kimsingi la mwanaadamu. Pamoja na hayo katika kipindi chote cha historia kumekuwepo na dini na madhehebu anuai katika vipindi mbali mbali vya historia ya mwanaadamu. Lakini idadi kubwa ya madhehebu au dini zimeingia katika upotofu na hivyo haziwezei tena kumuongoza mwanaadamu. Hivyo tunaona namna baadhi ya wanaadamu wanavyoacha dini hizo baada ya kutopata muongozo. Mwanaadamu wa leo anataka dini yenye utajiri mkubwa wa kimaanawi. Dini ambayo inaenda sambamba na maisha na yenye kuwasilisha njia na mpango sahihi  wa maisha na kuleta utulivu na ridhaa katika roho ya mwanaadamu ambayo  leo inakumbwa na masaibu mengi. Hii ni dini ambayo haisambaratiki kutokana na matukio ya zama, ni dini ambayo inaenda sambamba na ustawi na maendeleo ya mwanaadmau katika sekta za elimu, utamaduni na jamii. Imam Khomeini MA, hayati Kiongozi Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria nukta muhimu kuhusu suala hili kwa kusema: "Sisi tunaamini kuwa dini pekee yenye uwezo wa kumuongoza mwanaadmau ni Uislamu. Iwapo dunia inataka kuokoka kutoka katika maelfu ya matatizo yaliyopo na mwanaadamu aishi maisha bora basi njia pekee ni kufuata Uislamu."


Bw. Clayton anasema ameamua kufuata Uislamu kwa sababu dini hii tukufu imejibu maswali yake na iko karibu zaidi na hisia zake. Hii ndio sababu alipoona mandhari ya sala ya jamaa akaathiriwa sana na amali hii muhimu ya ibada katika Uislamu. Alivutiwa sana na namna Waislamu wanavyohusiana na Mwenyezi Mungu. Wakati wa sala ya Jamaa, jamii ndogo ya Waislamu hukusanyika. Katika sala hiyo watu wa rangi mbali mbali kutoka kila tabaka la jamii husimama katika safu moja wote wakiwa sawa. Wote huwa wamefika hapo kwa lengo la pamoja la kumuabudu Mwenyezi Mungu. Mjumuiko huo kwa hakika huwa ni dhihirisho la jamii ambayo inatakiwa na Uislamu kote duniani. Jamii ambayo watu wake hufungamana na mafundisho ya kidini hasa maadili bora na wote wanatambua kuwa Mwenyezi Mungu anatazama kila wanachokifanya, ni jamii ambayo itakuwa mbali na ufisadi, ufuska, dhulma na maovu mengine yote.


@@@


Bw. Clayton anaendelea kusema:  “Uislamu unatutaka tuwe na akhlaqi na maadili mema, tuwe ni wenye kuwajibika na wenye kuwatakia wengine mema, tutetee haki na tusikiuke haki zetu na hali kadhalika tusipore mali za watu wengine. Uislamu unatufunza tufanye mambo ambayo yataleta kheri kwa jamii na tujiepushe na ufuska na maovu mengine yote. Aidha tunatakiwa tuwe ni wenye kutekeleza amali bora kama vile kusimamisha sala kwani ibada hiyo ni mojawapo ya njia za kudhihirisha utiifu wetu kwa Mwenyezi Mungu SWT,” anasema Mmarekani huyu aliyesilimu.


Ukizingatia kidogo nasaha hizo utagundua kuwa Uislamu ni dini ambayo inataka mwanaadamu awe na maisha bora binafsi na kijamii. Hapa tunapaswa kusema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona bado kuna watu ambao wako mbali na umaanawi na mafundisho ya kidini kutokana na kuzingatia kupita kiasi masuala ya kidunia na kimaada. Ulimwengu wa Magharibi ambao unadai kuwa umestaarabika sasa umezama katika kinamasi cha kuabudu matamanio ya nafsi jambo ambalo limesababisha matatizo mengi katika jamii. Hivi sasa Wamagharibi wanajaribu kutumia njia mbali mbali kujinusuru na kuleta utulivu katika jamii lakini hawajafanikiwa kutokana na kutafuta suluhisho lisilofaa. Mwandishi Mjerumani Spengler katika kitabu chake chenye anwani ya ‘Decline of the West’ au ‘Kuporomoka Magharibi’ anasema:  “Sisi sasa tunaelekea katika mkondo uliopinda, tunaelekea katika kiza na maangamizi. Ni sawa na zama za Ufalme wa Roma na ustaarabu wake ambao hatimaye uliangamia.”


Mmarekani aliyesilimu Bw. Clayton anamaliza maneno yake kwa kusema: ‘Mimi nilitamka na kuamini kalima ya La Ilaha ila Allah kutoka kina cha moyo wangu. Imani yangu iko katika hisia zangu zote na ninaamini kuwa Uislamu ni dini ambayo inaenda sambamba na fitra au maumbile asilia ya mwanaadamu. Wakati mwanaadamu anapomuamini Mwenyezi Mungu kikamilifu basi huwa hawezi tena kupoteza matumaini maishani. Tunapaswa kufahamu kuwa Mwenyezi Mungu Mwenye uwezo anafahamu yote yanayojiri na atatusaidia tunapohitajia. Ni kwa kutenda amali njema na kumuamini Mola Muumba ndio mwanaadamu anapoweza kuokoka.


Tags