Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 31-35 (Darsa ya 709)
Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 31-35 (Darsa ya 709)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 709, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 29 ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 31 na 32 ambazo zinasema:
وَلَمَّا جَاءَتْ رُسُلُنَا إِبْرَاهِيمَ بِالْبُشْرَى قَالُوا إِنَّا مُهْلِكُو أَهْلِ هَذِهِ الْقَرْيَةِ إِنَّ أَهْلَهَا كَانُوا ظَالِمِينَ
Na wajumbe wetu walipo mjia Ibrahim na bishara, walisema: Hakika sisi tutawaangamiza watu wa mji huu, kwani watu wake hakika wamekuwa madhaalimu.
قَالَ إِنَّ فِيهَا لُوطًا قَالُوا نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَن فِيهَا لَنُنَجِّيَنَّهُ وَأَهْلَهُ إِلاَّ امْرَأَتَهُ كَانَتْ مِنَ الْغَابِرِينَ
Akasema: Hakika humo yumo Lut'i. Wao wakasema: Sisi tunajua zaidi nani aliyemo humo. Hapana shaka tutamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa mkewe aliye miongoni mwa wenye kubaki.
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa kaumu ya Nabii Luti ilikuwa ya watu waovu na mafasiki. Watu hao, badala ya kuzingatia maneno ya mantiki ya Mtume wao, walimkejeli na kumfanyia stihzai Nabii wao huyo na kumtuhumu kuwa ni muongo. Hata hivyo Nabii Lut (as) hakurudi nyuma wala kuacha kazi ya kukataza maovu kwa sababu ya mashinikizo na vitisho vya watu wa kaumu yake; bali alimuelekea Allah na kumwomba ampe nusura na ushindi dhidi ya watu hao waovu.
Aya tulizosoma zinaendelea na maudhui hiyo kwa kueleza kwamba: Mwenyezi Mungu aliwatuma malaika kwa Nabii Ibrahim (as) ili wakampe bishara njema ya kupata mtoto katika umri wa uzee aliokuwa nao na vilevile kumjulisha kuhusu adhabu itakayowashukia watu wa kaumu ya Nabii Lut (as). Na hii ni kwa sababu Nabii Lut alikuwa Mtume mfanya tablighi na mfikishaji wito wa Nabii Ibrahim katika mji wake; na Allah alikuwa amesha mtakabalia dua aliyomwomba ya kutaka watu waovu wa kaumu yake washukiwe na adhabu. Aya tulizosoma zinasema: wakati Nabii Ibrahim aliposikia habari ya kuteremshwa adhabu alihofia hatima ya Nabii Lut ambaye alikuwa akiishi katika mji ule; lakini malaika walimjibu kwa kumwambia: 'kutokana na kaida na utaratibu wa Allah, sisi hatuyachomi mabua tukachanganya na mahindi pamoja; ni wale wafanya madhambi tu ndio watakaofikwa na adhabu.' Hata mke wa Nabii Lut, ambaye alijitenga na safu ya waumini na kujiunga na tapo la waliokufuru hakutoka nje ya kaida na kanuni hiyo ya Allah. Pamoja na kwamba mwanamke huyo alikuwa akiishi kwenye nyumba ya Mtume lakini hakuwa miongoni mwa waliookoka na adhabu.
Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba malaika ni watendaji katika mfumo wa ulimwengu. Ni watoaji biashara njema ya rehma za Allah na pia ni wateremshaji wa adhabu ya Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kwenda kinyume na utaratibu sahihi wa kukidhi ghariza na matamanio ya kijinsia kunahesabiwa kuwa ni dhulma. Ni dhulma dhidi ya nafsi yake mwenyewe mtu, familia yake na jamii kwa jumla. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba ikiwa dhulma itaenea na kuzagaa katika jamii, watu wa jamii hiyo wanakaribia kuangamizwa. Kadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa mke na watoto wako huru katika kuchagua njia ya kufuata. Mke wa Nabii Lut alifadhilisha kufuata njia ya makafiri lakini watoto wake walichagua kufuata njia ya baba yao.
Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 33, 34 na 35 ambazo zinasema:
وَلَمَّا أَن جَاءَتْ رُسُلُنَا لُوطًا سِيءَ بِهِمْ وَضَاقَ بِهِمْ ذَرْعًا وَقَالُوا لا تَخَفْ وَلا تَحْزَنْ إِنَّا مُنَجُّوكَ وَأَهْلَكَ إِلاَّ امْرَأَتَكَ كَانَتْ مِنَ الْغَابِرِينَ
Na wajumbe wetu walipo mfikia Lut'i, aliwahuzunikia, na akapata dhiki kwa ajili yao. Wakasema: Usihofu wala usihuzunike. Hakika sisi tutakuokoa wewe na ahali zako, ila mkeo aliye miongoni mwa wenye kubaki.
إِنَّا مُنزِلُونَ عَلَى أَهْلِ هَذِهِ الْقَرْيَةِ رِجْزًا مِّنَ السَّمَاء بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ
Kwa yakini sisi tutawateremshia watu wa mji huu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya uchafu wanao ufanya.
وَلَقَد تَّرَكْنَا مِنْهَا آيَةً بَيِّنَةً لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ
Na hakika tumeacha katika mji huo Ishara ilio wazi kwa watu wanao tumia akili zao.
Kutokana na aya nyengine za Qur'ani inaonyesha kwamba Nabii Lut hakuwatambua malaika kwa sababu walijitokeza katika umbo la vijana wazuri wenye sura jamili. Kwa hivyo alichelea wageni wake hao wasije wakavunjiwa heshima na watu wachafu na mafasiki wa kaumu yake. Kwa sababu hiyo akawa mwenye ghamu na huzuni huku akiwa ametingwa na kuemewa ni vipi ataweza kulinda heshima ya wageni wake hao. Lakini malaika wakajitambulisha na kumuhakikishia mtume huyo wa Allah kwamba mikono ya watu wale wachafu haitoweza kuwafikia wao na kwamba muda si mrefu watashukiwa na adhabu kiasi kwamba haitobaki athari yoyote ya watu hao zaidi ya nyumba zao zilizobomoka na kuporomoka.
Kwa mujibu wa aya hizi tulizosoma, watu kushupalia, kuendelea na kukithirisha kufanya madhambi katika jamii ni jambo hatari, kwa sababu si wafanyaji tu peke yao bali si hasha watu wote katika jamii wakafikwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu; adhabu ambayo itatoa funzo na ibra kwa wengine. Kulingana na aya nyengine za Qur'ani, kwanza zilzala na tetemeko kubwa na la kutisha la ardhi liliutingisha na kuupindua juu chini mji wa Sodom, mahala walipokuwa wakiishi watu hao, kisha mvua kali ya mawe ikawamiminikia na kuwafanya watu wote na vitu vyote vizikwe na kufunikwa na kifusi cha mawe na udongo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kama jamii itakuwa imefisidika na kuharibika kwa maovu kuna uwezekano wa uharibifu huo kupenya na kuingia kwenye sehemu zake zote. Ifikiapo hali hiyo hata familia safi na nzuri kimaadili huwa hazina raha wala usalama tena majumbani mwao na wazazi wa familia hizo huhofia hali za watoto wao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa jukumu la kulinda heshima ya mgeni liko mikononi mwa mwenyeji na inapasa heshima yake ndani ya nyumba ya mwenyeji wake ilindwe. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba muumini ni mtu mwenye ghera ya dini yake, na popote pale anaposhuhudia hatari, upotofu au ufisadi huchukua hatua, na si kupuuza na kutojali na kuyapita maovu na utovu wa maadili vivi hivi tu. Kadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa mafungamano ya kifamilia na kuwa na uhusiano wa nasaba na waja wema hakutoshi peke yake kumfanya mtu aokoke na kupata nusra duniani na akhera. Bali si hasha makazi ya mke wa Mtume yakawa motoni, kama ilivyo kwa mke wa Nabii Lut (as) na makazi ya mke wa taghuti mkubwa kama Firauni yakawa kwenye Pepo ya neema. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 709 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani, na atupe mema akhera na atulinde na adhabu ya moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/