Sura ya Al-A'nkabut, 41-45 (711)
Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 41-45 (Darsa ya 711)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 711, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 29 ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 41 na 42 ambazo zinasema:
مَثَلُ الَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّهِ أَوْلِيَاء كَمَثَلِ الْعَنكَبُوتِ اتَّخَذَتْ بَيْتًا وَإِنَّ أَوْهَنَ الْبُيُوتِ لَبَيْتُ الْعَنكَبُوتِ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ
Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano wa buibui alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui, lau wangelikuwa wanajua.
إِنَّ اللَّهَ يَعْلَمُ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ
Kwa hakika Mwenyezi Mungu anajua kila kitu wanacho kiomba badala yake Yeye. Na Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima.
Katika darsa kadhaa zilizopita tulisoma aya zilizoeleza hatima iliyowapata watu wa kaumu mbalimbali walioasi na kusimama kukabiliana na wito wa Mitume wa Allah. Aya ya 41 tuliyosoma, ambapo jina la sura hii ya A'nkabut limetokana na aya hiyo imetoa tashbihi ya kuvutia na iliyo wadhiha kabisa ya kubainisha hali ya makafiri kwa kueleza kwamba watu hao, badala ya Mwenyezi Mungu wanawaendea watu au vitu vingine, hali ya kuwa ghairi ya Yeye Mola, yeyote yule na chochote kile, hata watawala wenye nguvu kubwa kabisa za madaraka kama Firauni ni dhaifu mno na si lolote si chochote mbele ya nguvu za Allah SW. Ni sawa kabisa na nyumba ya buibui ambayo imejengwa na utando dhaifu na hafifu ambao uvumiwapo na upepo tu huraruka na kupeperuka. Na watu wanaomtegemea mwengine yeyote ghairi ya Mwenyezi Mungu pia huwa kwa hakika egemeo lao hilo ni sawa na utando wa buibui, ambao hauna dhamana na hauwezi kuaminika katika mazingira magumu na ya tabu ya maisha.
Kama washirikina wangekuwa wanajua kwamba kile walichokitegemea ni mithili ya utando wa buibui wasingekiendea wala wasingekitegemea; kama ambavyo lau kama wangejua kuwa Muumba wao anajua kwamba badala ya Yeye, wameamua kuwaendea viumbe wake, basi wangeliacha kufanya hivyo na kurejea kwake Yeye Mola. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba moja ya mbinu za Qur'ani ni kutumia umithilishaji na ushabihishaji kwa ajili ya kuweka wazi hakika ya mambo; na mifano bora zaidi ya umithilishaji ni ile inayoweza kueleweka na kufahamika katika kila mahala na zama na kwa watu wa hali na matabaka yote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, msingi wa imani ni imara na madhubuti, lakini msingi wa shirki ni legelege na dhaifu mno. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba badala ya kumtegemea asiyekuwa Allah, ambaye ni duni na dhaifu mithili ya nyumba ya buibui, tumuelekee na kumtegemea Mungu ambaye ni mwenye hekima na asiyeshindika.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 43 na 44 ambazo zinasema:
وَتِلْكَ الأَمْثَالُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ وَمَا يَعْقِلُهَا إِلاَّ الْعَالِمُونَ
Na hiyo ni mifano tunawapigia watu, na hawaitii akilini ila wenye ilimu.
خَلَقَ اللَّهُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ بِالْحَقِّ إِنَّ فِي ذَلِكَ لآيَةً لِّلْمُؤْمِنِينَ
Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Kwa hakika katika hayo kuna Ishara kwa Waumini.
Aya hizi zinaashiria umuhimu wa mifano inayotolewa na Qur'ani na kueleza kwamba: isidhaniwe kuwa mifano hii inayopigwa na Qur'ani ni mifano ya kawaida na isiyo na faida; haya ni maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo yameelezwa ili hakika ya imani na kufru iwe wazi na wadhiha zaidi kwa watu. Ikiwa umithilishaji huu unaonekana kitu cha kawaida na rahisi kwa watu wa kawaida, una nukta za kina na za thamani kubwa kwa watu alimu na wajuzi. Nukta makini ambazo hubainika zinapozingatiwa kielimu; na akili huweza kuzifahamu barabara.
Kisha aya zinaendelea kwa kuzungumzia uumbaji wa Mwenyezi Mungu na kueleza kwamba Mwenyezi Mungu ambaye ni mjuzi wa kila kitu, asiyeshindika na mwenye hekima hakuumba ulimwengu burebure na bila ya lengo, bali alifanya hivyo kwa msingi wa haki. Watu waumini wanalifahamu hilo, lakini washirikina na makafiri hawako tayari kutafakari na kuuelewa uhakika huo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba umithilishaji wa Qur'ani ni makini na wenye maana ya kina; na ni wanazuoni na watu waelewa tu ndio wanaoweza kubaini maana ya kina ya umithilishaji huo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa dunia imeumbwa kulingana na ratiba na lengo maalumu; si kitu kilichotokana na sadfa na bahati tu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba washirikina na makafiri uono wao unakomea kwenye utambuzi wa vitu vilivyoko kwenye ulimwengu wa maumbile. Lakini uono wa waumini unavuka kwenye mpaka wa utambuzi wa vitu hivyo tu na huviangalia kama alama na ishara ya kuwepo kwa Muumba wake na huwafikisha kwenye utambuzi wa kumjua Mwenyezi Mungu SW.
Darsa ya 711 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 45 ambayo inasema:
اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلاةَ إِنَّ الصَّلاةَ تَنْهَى عَنِ الْفَحْشَاء وَالْمُنكَرِ وَلَذِكْرُ اللَّهِ أَكْبَرُ وَاللَّهُ يَعْلَمُ مَا تَصْنَعُونَ
Soma uliyo funuliwa katika Kitabu, na usimamishe Sala. Hakika Sala inamzuilia (mtu) mambo machafu na maovu. Na kwa yakini dhikri ya Mwenyezi Mungu ndilo jambo kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yafanya.
Aya hii inamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW, lakini ujumbe wake haumhusu mtukufu huyo tu bali unajumuisha waumini wote. Allah SW amemhutubu moja kwa moja Mtume wake ili kuwafanya waumini wawe na mazingatio makubwa zaidi. Katika aya hii yameusiwa mambo mawili; moja ni kusoma Qur'ani na jengine ni kusimamisha Sala. Ni wazi kwamba udumishaji wa mambo mawili haya una taathira kubwa mno kwa maisha ya watu; na kuzembea na kupuuza utekelezaji wake kunaidhoofisha imani ya mtu kwa sababu Qur'ani na Sala ni chemchemu mbili kuu za kujenga na kunawirisha imani za waumini. Tab'an ikiwa usomaji Qur'ani utafanyika kwa tafakuri na mazingatio ya maana ya aya, bila ya shaka taathira yake huwa kubwa zaidi na huifanya imani ya Muislamu iwe imara zaidi. Kusimamisha Sala pia, kwa kusali angalau rakaa 17 za Sala za faradhi kwa siku, kama kutafanyika kwa utaratibu sahihi na kuambatana na mazingatio ya moyo humwezesha mtu kujiweka mbali na madhambi na mambo maovu. Miongoni mwa faida za Sala ni kumtakasa na kumsafisha mtu na uchafu wa kiroho. Tab'an sifa ya Sala ya kumkinga mtu na madhambi ndiyo faida ya daraja ya chini ya ibada hiyo tukufu, lakini ya daraja ya juu na muhimu zaidi ya Sala ni dhikri na utajo wa Allah na wa neema na rehma zake, ambao ni wenye utukufu na thamani ya juu zaidi kuliko kitu chochote. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kusoma Qur'ani na kusimamisha Sala ni mambo yenye nafasi ya kwanza katika ratiba za malezi za Uislamu; na hili ni jambo lililousiwa mno na viongozi wa dini. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Qur'ani, imebainisha falsafa ya baadhi ya hukumu za dini, ikiwemo Sala ambayo ni kumweka mbali mtu na uchafu na kumuelekeza kwenye mazingatio ya kumkumbuka Allah SW. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kufanya mambo mema na matukufu kama kusoma Qur'ani na kutekeleza ibada ya Sala huwa na taathira ya kumweka mbali mtu na mambo maovu. Wa aidha tunajifunza kutokana na aya hii kuwa Sala ina mchango mkubwa mno katika kumrekebisha mtu na jamii kwa jumla. Wapenzi wasikilizaji, kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake wanaonufaika kiimani na kimatendo kutokana na kusoma Qur'ani na kusimamisha Sala. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/