Jan 16, 2017 16:47 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni tena katika mfululizo wa vipindi hivi vinavyokosoa kwa mujibu wa Qur’an Tukufu na suna za Bwana Mtume (saw) makundi ya ukufurishaji yanayotekeleza jinai za kutisha dhidi ya Waislamu wengine hii ikiwa ni sehemu ya 19 ya mfululizo huo.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia misimamo ya wasomi na maulama wa ulimwengu wa Kiislamu katika kulaani na kupinga vikali mienendo ya wanachama wa makundi ya ukufurishaji hususan Daesh (ISIS) ambapo leo tutaendelea kunukuu radiamali za shakhsia hao katika uwanja huo. Hivyo endeleeni kuungana nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Sheikh Ahmad al-Kubaisi, mwanazuoni na mufti wa Waislamu wa Kisuni nchini Iraq, sambamba na kuwajibisha jihadi dhidi ya genge la wale wanaojiita kuwa ni Dola la Kiislamu nchini Iraq na Sham (Daesh-ISIS) anasema: “Wafuasi wa kundi hilo ni washirika wakubwa wa Israel na Saudia. Wanapigana kwa lengo tu la kuudhoofisha na kuusambaratisha Uislamu. Nina hakika kwamba, Daesh ni tawi la Uwahabi ambalo lipo kwa lengo la kuharakisha mkakati wa kusambaratisha Uislamu na kwa hakika limefanikiwa sana kuwasafishia njia ya kupenyeza Wazayuni huko Libya, Tunisia, Yemen, Somalia na Iraq.” Mwisho wa kunukuu. Mbali na maulama hao chuo kikuu cha al-Azhar nchini Misri hakikuachwa nyuma katika kulaani mienendo ya genge hilo potofu ambapo kwa mara kadhaa kimekukuwa kikiwashambulia wanachama wake kwa kuwataja kuwa ni Makhawariji wa zama hizi. Chuo hicho kinalaani vikali hatua ya kundi hilo la Kiwahabi ya kuwarubuni vijana wa Kiislamu na upotofu wake katika kuvuruga usalama na uthabiti wa nchi za Kiislamu. Katika sehemu moja ya taarifa yake al-Azhar inasema: “Kitendo cha genge hilo cha kupeperusha bendera zenye nembo za Uislamu, linakusudia kuwavutia na kuwarubuni vijana wa Kiislamu, katika hali ambayo, dini ya Uislamu inawachukia vikali wanachama wa genge hilo.” Mwisho wa kunukuu. Katika fremu hiyo, Chuo Kikuu hicho cha Kiislamu cha al-Azhar kinawatahadharisha Waislamu wote duniani kutorubuniwa na linganio la wanachama wajinga na wenye kufurutu ada wa kundi hilo kwa kusema: “Daesh hawana tofauti na Khawarij ambao walisimama na kufanya uasi dhidi ya Imam Ali Bin Abi Twalib (as) na kisha wakamtuhumu kwa ukafiri. Kama ambavyo pia walimkufurisha kila mtu ambaye alipinga dhehebu lao. Kundi hilo linaeneza mafundisho ambayo hayana msingi wowote katika dini hiyo ambapo katika hilo linaeneza uongo na uzushi wa wazi ili kwa njia hiyo liweze kuwafanya walimwengu waichukie dini ya Kiislamu. Linauonyesha Uislamu kuwa dini ya umwagaji damu, katika hali ambayo Uislamu ni dini ya amani na inayojitenga na vitendo hivyo.” Mwisho wa kunukuu. Aidha Dakta Abbas Shuman, wakili wa Chuo kikuu cha al-Azhar nchini Misri anasisitizia suala hilo kwa kusema: “Kwa mara kadhaa al-Azhar tumekuwa tukilaani jinai za genge la Daesh kuhusiana na mauaji dhidi ya Waislmu na raia wasio na hatia, kama ambavyo pia tumekuwa tukilaani mwenendo wa kuwahamisha kwa lazima Wakristo na mauaji ya watu wa kabila la Yazidi huko Iraq. Hii ni kwa kuwa katika Uislamu kuna anga ya uhuru wa kidini unayowapa fursa wapinzani wake wote  ilimuradi tu wasishambulie au kufanya jinai dhidi ya wafuasi wa dini hiyo. Kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, mtu yeyote anao uhuru wa kuamini au wa kukufuru.” Mwisho wa kunukuu. Naye Shawki Allam, Mufti Mkuu wa Misri amenukuliwa akizungumzia kundi la Daesh (ISIS) kwa kusema: “Vitendo vinavyotekelezwa na wanachama wa kundi hilo huko nchini Iraq, havina mahusiano yoyote na jihadi. Kwa hakika watu wenye fikra za kufurutu mpaka wanaenda kinyume kabisa na sheria za dini ya Kiislamu. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa, kundi la Daesh linatoa tafsiri potofu ya aya nyingi za Qur’ani kwa maslahi yake binafsi.” Mwisho wa kunukuu.

Muhammed Shehata Jondi, msomi mtajika wa Kiislamu na mjumbe wa  Jumuiya ya Utafiti wa Kiislamu nchini Misri, anasema: “Daesh ni genge la kigaidi ambalo msingi wake ni kufanya ukatili, mauaji na umwagaji damu kwa kuwaelekezea silaha zao Waislamu. Kwa hakika mienendo hiyo imeharamishwa ndani ya dini ya Kiislamu.” Aidha Shehata Jondi anaongeza kwa kusema: “Kundi la Daesh haliwakilishi Waislamu wa Ahlus-Sunnah licha ya kwamba wanachama wa kundi hilo wamekuwa wakijinasibisha na dhehebu hilo. Hii ni kwa kuwa Usuni hauruhusu kwa aina yoyote kufanya vita na mauaji dhidi ya Waislamu wa Shia. Hivyo suala hilo haliwezi kuwa kisingizio cha kuvuruga usalama wa Iraq.” Mwisho wa kunukuu.

******************************

Mitazamo ya maulama wa Kisuni nchini Misri na kwa kuzingatia nafasi ya Chuo Kikuu cha al-Azhar katika ulimwengu wa Kiislamu, imekuwa na umuhimu kwa Waislamu wa Kisuni duniani. Hii ni kusema kuwa, aghlabu ya maulama wengi wa Ahlus-Sunah katika nchini nyingi za Kiislamu wamesomea katika chuo hicho cha al-Azhar. Mbali na Misri, maulama wa Kisuni katika nchi nyingine za Kiislamu wamekuwa na mitazamo iliyo wazi  katika kupinga jinai na mauaji ya genge hilo potofu la Daesh (ISIS). Kwa mfano, Sheikh Sahib Zadeh Aziz, mkuu wa tawi la chuo cha al-Azhar nchini Pakistan amenukuliwa akisema: “Kundi la kigaidi la Daesh ni mpango wa utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kuwaua Waislamu na kumwaga damu, kubaka wanawake na mabinti  zao.” Mwisho wa kunukuu. Katika fremu hiyo, baraza la maulama wa Kiislamu nchini Pakistan sanjari na kutoa ripoti maalumu ya kulaani genge hilo la ukufurishaji ambalo linakiuka misingi ya dini ya Kiislamu lilisema: “Uislamu na Waislamu hawawezi kuvumilia mauaji yanayofanywa na wanachama wa kundi hilo dhidi ya watu wasio na hatia sanjari na kupora mali zao.” Mwisho wa kunukuu. Kadhalika baraza hilo la maulama wa Kiislamu nchini Pakistan liliwataka vijana na Waislamu duniani kuacha mara moja kujiunga au kushirikiana na kundi lolote ambalo linatumia vibaya dini ya Uislamu kufanya jinai na kupuuza misingi ya dini hiyo. Mbali na Pakistan, wasomi wa Kiislamu wapatao 1050 nchini India hawakuwa mbali katika kuungana na Waislamu wengine duniani katika kulaani  jinai za kundi hilo kibaraka wa maadui wa Uislamu ambapo maulama hao walitangaza wazi kwamba Daesh linakinzana kabisa na misingi na mafundisho ya dini ya Kiislamu. Ripoti ya fatwa ya wasomi hao wakubwa wa Kiislamu nchini India iliyochapishwa katika juzuu 15 ilisema: “Uislamu sio dini ya mauaji, uharibifu wala udhalilishaji wa matukufu ya Kiislamu.” Mwisho wa kunukuu. Ripoti ya fatwa hiyo ya wasomi wa Kiislamu nchini India yenye juzuu 15 na ambayo inahesabiwa kuwa fatwa muhimu zaidi katika historia ilitumwa katika nchi mbalimbali za dunia na kwa Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Kati ya watu waliotia saini hati ya fatwa hiyo ni poamoja na Sayyid Ahmed Bukhari, imamu wa jamaa wa msikiti mkuu mjini New Delhi, wasomi wakubwa wa kituo cha waqfu cha Ajmer Sharif na Nizam al-Din, wahudumu wa taasisi ya kielimu ya Reza mjini Mumbai, jumuiya ya maulama na baraza la maulama wa Kiislamu mjini hapo Mumbai, shakhsia na mamia ya wasomi mbalimbali nchini India.

 

*******************************************

Ndugu wasikilizaji mnafaa kufahamu kwamba kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh linaendesha harakati zake nchini Afghanistan suala ambalo pia limewafanya wasomi wa nchi hiyo kusimama na kupaza sauti kulaani jinai za wanachama wake. Katika fremu hiyo baraza la wasomi wa Kiislamu nchini humo lilitangaza kwamba harakati zote za genge hilo hazitambuliwi kwa aina yoyote na dini tukufu ya Kiislamu na badala yake genge hilo linatekeleza ajenda chafu za maadui wa Uislamu kwa kuidhihirisha dini hiyo kuwa ya ukatili. Ripoti hiyo ilitolewa baada ya wanachama wa kundi hilo kutangaza kwamba, kuwabaka mabinti na wanawake wa dini nyingine ni halali na ibada. Mohammad Qasim Halimi, msemaji wa baraza la maulama wa Kiislamu nchini Afghanistan alinukuliwa akisema: “Dini ya Kiislamu imewalingania wafuasi wake kuwa wapole, kufanya udugu na usawa. Kwa msingi huo kuwateka nyara wasichana na kuwabaka, ni vitendo ambavyo havina nafasi katika Uislamu. Vitendo na harakati zote za wanachama wa Daesh si tu kwamba viko kinyume na dini ya Uislamu, bali ni kwamba Uislamu unawalaani watu wanaofanya matendo hayo. Wafuasi wa genge hilo hawawakilishi dini ya Uislamu. Ni mahala gani Uislamu umehalalisha mtu kuwalipua watu wasio na hatia kwa mabomu au kuwaua watoto wadogo na kuwabaka wanawake?  Wanachama wa Daesh (ISIS) si tu kwamba ni wabakaji, bali wanatekeleza hata mauaji ya umati na ushirikina. Matendo yao yote yanapingana na Uislamu. Ni jambo la kusikitisha kwamba hadi leo baadhi ya watu wanawatambua wafuasi wa genge hilo potofu kuwa ni mujahidina wa Uislamu katika hali ambayo magaidi hao wanaichafua dini tukufu ya Kiislamu.” Mwisho wa kunukuu.

Na kufikia hapa ndio tunafikia tamati sehemu ya 19 ya mfululizo wa vipindi hivi. Mimi ni Sudi Jafari kwaherini……./ 

 

 

Tags