Hadithi ya Uongofu (64)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 64 kitazungumzia subira na ustahamilivu. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio niliyokuandalieni kwa leo.
Fasili na maana ya kilugha ya subira ni hali ya kuwa na uvumilivu yaani hali ya kutokuwa na papatiko aghalabu baada ya kufikwa na jambo lisilo zuri. Amma katika maana na istilahi ya maulama na wanazuoni wa elimu ya maadili ni kujilazimisha kutenda jambo ambalo linapaswa kufanywa kwa mujibu wa akili na sheria na wakati huo huo kujizuia kufanya kitu ambacho kimekatazwa na sheria na akili. Kimsingi ni kuwa subira ina pande mbili.
Kwa hakika mwanadamu ni kiumbe ambaye Mwenyezi Mungu amemuumba kwa ajili ya lengo kubwa; lengo ambalo si jingine ghairi ya saada na ukamilifu wa mwanadamu na kujikurubisha kwa Mola Muumba. Kwa msingi huo, baada ya mwanadamu kufahamu lengo la Mwenyezi Mungu, anapaswa kufanya hima na idili kwa shabaha ya kulifikia lengo hilo. Hata hivyo kwa kuzingatia kwamba, maisha ya dunia yako kwa namna ambayo daima ni yenye kuambatana na matatizo na vizingiti vingi, mwanadamu anaweza kulifikia lengo lake hilo pale tu atakaposimama kidete mbele ya matatizo, kuwa na subira na uvumilivu pia. Katika Qur'ani Tukufu kuna aya nyingi zinazowataka Manabii, Mitume wa Mwenyezi Mungu, mawalii Wake na waumini kwa ujumla kushikamana na subira na uvumilivu. Kwa mfano katika aya ya 35 ya Surat al-Ahqaaf Mwenyezi Mungu anamhutubu Mtume Muhammad SAW kwa kumwambia:
"Basi subiri, kama walivyo subiri Mitume wenye ustahamilivu mkubwa."
Aidha anasema katika aya ya 153 iliyoko katika Surat al-Baqara kwamba:
"Enyi mlio amini! Takeni msaada kwa subira na Sala. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri."
Imam Ali bin Abi Talib as anazungumzia thamani ya kusubiri na kulitaja suala la subira na kusubiri kwamba, ni katika sifa za wacha Mungu. Aidha anaitaja nafasi ya subira katika imani na kuishabihisha na nafasi ya kichwa katika mwili wa mwanadamu. Anasema:
Itangulizeni subira, kwani subira katika imani ni mithili ya kichwa katika mwili. Kama ambavyo hakuna kheri katika mwili ambao hauna kichwa, vivyo hivyo hakutakuwa na kheri katika imani ambayo ndani yake hakuna subira.
Kwa hakika hadithi hii inaonesha kuwa, mtu ambaye hana subira hawezi kufikia imani yenye ukamilifu. Hii ni kutokana na kuwa, funguo za ibada zote na kufikia uhakika wa ibada hizo ni kuwa na subira. Kwa hakika subira humpa mwanadamu nguvu ili aweze kusimama na kukabiliana na ushawishi wa shetani na matamanio ya kinafsi na kutoa jibu la hapana kwa shetani mlaaniwa na hivyo kutokubali kutumbukia katika madhambi.
Imam Ali bin Abi Talib as anasema katika hadithi nyingine kwamba: Mtu ambaye hana subira na ustahamilivu, imani yake haiwezi kudumu na kubakia.
Katika utamaduni wa Kiislamu mtu mwenye subira ni yule ambaye anastahamili na kusimama kidete katika matatizo yote maishani na katu haonyeshi kushindwa au kutetereka katika jambo lolote. Imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Muhammad Baqir as ya kwamba amesema:
Pepo imejengwa juu ya taabu, ghamu na kusubiri. Hivyo basi kila ambaye atasubiri katika mambo magumu duniani ataingia peponi. Na Jahanamu imengwa katika starehe na matamanio, hivyo basi kila ambaye atajitumbukiza katika starehe, mambo machafu na matamanio mabaya ataingia katika moto wa Jahanamu.
Moja ya sababu muhimu za kufaulu mitihani ya Mwenyezi Mungu ni subira na ustahamilivu pindi mtu anapokabiliwa na matatizo. Mwenyezi Mungu anaashiria hilo katika aya ya 155 ya Surat al-Baqarah kwamba:
"Na kwa hakika tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na nafsi na matunda. Na wabashirie wanaosubiri." Kwa hakika kufanya subira mbele ya aina yoyote ya mtihani na matatizo ni jambo ambalo limetiliwa mkazo katika dini tukufu ya Kiislamu. Umuhimu wa subira katika mabalaa na matatizo unaonekana wazi tunaporejea hadithi ambapo tunaona kuwa, jambo hilo linatajwa kuwa moja ya daraja za juu za waumini. Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema: "Kadiri mtihani na matatizo yanavyokuwa makubwa zaidi, basi ujira na thawabu zake nazo huwa nyingi zaidi."
Subira na ustahamilivu ni miongoni mwa adabu nyingine za kujifunza na kutafuta elimu. Kupokea ukumbusho wa mwalimu, subira na ustahamilivu mbele ya mambo magumu na vizingiti ni miongoni mwa adabu muhimu za uwanafunzi ambazo zimebainishwa wazi na bayana katika kisa cha Khidhr na Nabii Mussa AS. Mtu ambaye hana subira na uvumilivu kutokana na mazingira magumu anayokabiliana nayo katika masomo na kutafuta elimu, yumkini akakatisha masomo na kushindwa kuendelea kuwa na mwalimu wake kwa ajili ya kujifunza. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana wanafunzi wanapaswa kushikamana na subira na ustahamilivu na wajiepushe na haraka na papara katika kujifunza mambo na wasiwe na fikra ya kusoma haraka haraka ili wafikie malengo yao pasina ya kupitia hatua za kielimu kikamilifu na kama inavyotakiwa.
Bwana Mtume Muhammad SAW amezigawa subira katika sehemu tatu. Mtukufu huyo amesema:”Subira zimegawanyika katika sehemu tatu: Subira ya kuvumilia masaibu, subira ya kushikamana na ta’a na subira ya kujizuia na madhambi. Kisha Bwana Mtume akaelezea daraja ya kila moja kati ya subira hizo kwa kusema:” Mtu anayeonesha subira anapofikwa na msiba na masaibu na akazivuka tabu za masaibu hayo kwa subira yake njema, Mwenyezi Mungu anamuinua daraja yake kwa kiwango mithili ya masafa ya baina ya mbingu na ardhi. Mtu anayekuwa na subira na akawa mwenye juhudi katika ta’a na kumwabudu Mwenyezi Mungu, Allah humuinua daraja yake kwa kiwango mithili ya masafa ya baina ya kina cha chini kabisa cha ardhi hadi kwenye Arshi; na mtu anayekuwa na subira ya kujizuia na kufanya madhambi Mwenyezi Mungu humuinua daraja yake kwa kiwango mithili ya masafa ya baina ya kina cha chini kabisa cha ardhi hadi inapoishia Arshi”. Kwa maneno haya matukufu ya Bwana Mtume inatubainikia kuwa subira ya kujizuia na madhambi, kujiepusha na maasi na kutofanya aliyoyakataza Mola ndiyo daraja ya juu zaidi ya subira.
Aidha athari na matunda ya subira yametajwa na kuzungumziwa katika maandiko na mafundisho mengi ya dini. Miongoni mwa athari na matunda hayo ni kwamba subira na mafanikio ni vitu vinavyoandamana sambamba. Imam Ali (AS) amesema:”Mtu mwenye subira ni mwenye kufanikiwa tu hata kama ni baada ya kupita muda mrefu”.
Athari na matunda mengine ya subira ni kwamba sifa hiyo tukufu ya kiakhlaqi humkinga na kumzuia mtu kufanya madhambi kama vile kunung’unika na kulalamikia taqdiri na qudra ya Mwenyezi Mungu; na kwa sababu ya subira na ustahamilivu wake hupata malipo ya thawabu kwa Mola. Imam Ali (AS) amesema tena hivi kuhusiana na subira:” Ikiwa utaonyesha subira na uvumilivu, hukumu aliyokadiria Mwenyezi Mungu juu yako itakufikia tu na utalipwa thawabu; na ikiwa hutovumilia na kunung’unika, taqdiri ya Mwenyezi Mungu itakufikia pia lakini utakuwa umepata dhambi”. Watu wenye kuonyesha subira ya kushikamana na ta’a na kujiepusha na maasi watakuwa na mwisho mwema huko akhera na Mwenyezi Mungu amewawekea malipo ya thawabu na neema nyingi zisizohesabika za Peponi. Kuwa na subira na istiqama ya kuvumilia mabalaa na masaibu humjenga mtu kimaanawi na kumuinua daraja yake katika ukamilifu wa kiutu, na kuyabadilisha masaibu yanayomfika kuwa ni rehma na uraufu wake Mola na hivyo kumfanya awe mja mwenye hisabu nyepesi huko akhera.
Muda wa kipindi hiki umefikia tamati kwa leo. Tukutane wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hikim cha Hadithi ya Uongofu. Ninakuageni nikimuomba Allah atujaalie sote tuwe na subira na ustahamilivu ili tuwee kupata ujira mnono wa kusubiri.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh….