Jan 23, 2017 05:37 UTC
  • Jumatatu 23 Januari, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe 24 Rabiuthani 1438 Hijria sawa na Januari 23, 2017.

Siku kama hii ya leo miaka 38 iliyopita sawa na tarehe 4 Bahman mwaka 1357 Hijria Shamsiya, Shapur Bakhtiyar Waziri Mkuu aliyekuwa karibu na utawala wa Shah ambaye alikuwa akielewa kuwa kurejea Imam Khomeini nchini kutoka uhamishoni Paris kungempokonya udhibiti wa hali ya mambo, alitoa amri ya kufungwa viwanja vyote vya ndege vya Iran ili kuzuia kurejea nchini Imam Khomeini. Shapur Bakhtiyar alichukua hatua hiyo baada ya kuchapishwa habari ya kukaribia kuwasili hapa nchini Imam Khomeini kutoka Paris Ufaransa. Hatua hiyo ya serikali ya utawala wa Shah iliwakasirisha wananchi ambao walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa ujio huo wa Imam Ruhullah Khomeini nchini Iran.

Shapur Bakhtiyar

Miaka 67 iliyopita katika siku kama ya leo, Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) liliutangaza mji wa Beitul Muqaddas ambao kibla cha kwanza cha Waislamu kuwa mji mkuu wa utawala huo badala ya Tel Aviv. Uamuzi huo uliofikiwa na Bunge hilo miaka miwili tu baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Wapalestina, uliwakasirisha mno Waarabu na Waislamu. Njama hiyo ya Israel iliyolenga kupata ridhaa ya nchi nyingine ili ziutambue rasmi mji huo kama mji mkuu wake na hivyo zihamishie balozi zao katika mji huo haikuwa na natija, kwani hadi leo mji wa Tel Aviv ungali unatambuliwa kama mji mkuu wa utawala huo vamizi unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Knesset

Katika siku kama ya leo miaka 98 iliyopita yaani tarehe 23 Januari 1919, Chama cha Kifashti cha Italia kiliasisiwa na Benito Mussolini. Wanachama wa chama hicho walikuwa wakivaa mashati meusi kama sare zao. Sare hiyo ilipelekea wafuasi wa chama hicho kujulikana kwa jina la watu wa " Mashati Meusi'.'' Fikra za Kifashti zilikuwa zimejengeka juu ya misingi ya kuunda dola moja kubwa la kidikteta na fikra hizo zilikuwa zikipingana aina yoyote ya uhuru. Oktoba mwaka 1922, Benito Mussolini na wafuasi wake waliuteka mji wa Roma na yeye kushika hatamu za uongozi akiwa Waziri Mkuu. Kuanzia hapo kiongozi huyo akaanza kutekeleza malengo na sera za Chama cha Kifashti. Hata hivyo mwaka 1945, mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia Benito Mussolini alitiwa mbaroni na wazalendo na kisha akanyongwa.

Benito Mussolini

Na Januari 23 mwaka 1556 yaani miaka 461 iliyopita, moja kati ya mitetemeko mikubwa kabisa ya ardhi duniani ulitokea katika jimbo la Shaanxi nchini China. Zilzala hiyo ilisababisha hasara kubwa katika jimbo hilo lililokuwa likihesabiwa kuwa na wakazi wengi zaidi nchini China. Watu wapatao 830,000 walipoteza maisha yao kufuatia janga hilo kubwa na la kutisha la mtetemeko wa ardhi katika jimbo hilo la Shaanxi. 

Miaka 601 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani mwaka 837 Hijiria, katika kipindi cha watawala wa Teimur alifariki dunia malenga wa Kiirani, Sayyid Qasim al Anwar. Alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa na mwenyeji wa mji wa Tabriz ulioko kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya kuishi na kufundisha katika mji wa Harat huko kaskazini magharibi kwa Afghanistan, Sayyid Anwar alianza kupata umashuhuri, kiasi kwamba walijumuika kwake wanafunzi na wafuasi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Hata hivyo kutokana na dhana mbaya ya watawala wa wakati huo dhidi ya malenga huyo, Sayyid Qasim al Anwar, alilazimika kuhama kutoka Harat kwenda Samarqand nchini Uzbekistan ya leo. Miongoni mwa athari za malenga huyo ni pamoja na diwani ya mashairi na vitabu vya "Anisul Arifina" na " Anisul Aashiqina".

Mahala lilipo kaburi la Sayyid Qaim al Anwar

Na mwaka 388 Hijiria katika siku kama ya leo, alifariki dunia mtaalamu wa lugha na alimu wa Kiislamu, Abu Ali Muhammad bin Mudhaffar maarufu kwa jina la Hatami au Baghdadi. Alipata elimu kwa walimu mashuhuri wa wakati huo na baadaye alianza kufundisha masomo ya lugha mjini Baghdad. Shule ya Hatami haikuwa na mithili katika zama hizo na wasomi wakubwa wa zama zile walikuwa wakishiriki katika vikao vya darsa za Abu Ali Muhammad bin Mudhaffar. Miongoni mwa vitabu vya mtaalamu huyo ni pamoja na kitabu cha "Hatamiya" kinachokosoa mashairi ya malenga wa zama zake.

ابوعلی محمد بن مظفر

 

Tags