Jan 24, 2017 09:50 UTC

Sura ya Ar-Rum, aya ya 47-49 (Darsa ya 727)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 727 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 30 ya Ar-Rum. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 47 ambayo inasema:

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ رُسُلا إِلَى قَوْمِهِمْ فَجَاؤُوهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَانتَقَمْنَا مِنَ الَّذِينَ أَجْرَمُوا وَكَانَ حَقًّا عَلَيْنَا نَصْرُ الْمُؤْمِنِينَ

Na hakika tulikwisha watuma Mitume kwa kaumu zao, na wakawajia kwa hoja zilizo wazi. Tukawaadhibu wale walio fanya makosa. Na ilikuwa ni haki juu yetu kuwanusuru Waumini. 

Bila ya shaka wapenzi wasikilizaji mngali mnakumbuka kuwa aya ya mwisho tuliyosoma katika darsa iliyopita ilihusu uwezo na hekima ya Allah SW ya kusukuma mawingu kwa upepo na kuwa sababu ya kuteremka rehma ya mvua inayootesha mimea na kuwapa uhai wanadamu. Aya tuliyosoma inaashiria kutumwa kwa Mitume kwa ajili ya kuwaelekeza watu kwenye njia ya uongofu kwa msingi wa hoja na burhani; na aya zinazofuatia zinazungumzia tena maudhui ya kupelekwa pepo zinazowezesha kunyesha mvua inayohuisha ardhi. Ni kama kwamba kuwepo aya hii ya 47 baina ya aya zinazohusu uwezo na hekima ya Mwenyezi Mungu katika uumbaji ni kutaka kubainisha nukta moja makini; nayo ni kwamba mfumo wa uumbaji na wa upangaji sharia inatokana na chanzo kimoja.  Yaani Mungu huyohuyo aliyekuumbeni, akaliamrisha jua, mawingu na mvua vikidhi mahitaji yenu ya kimwili na kimaada, amezingatia pia mahitaji yenu ya kiroho na kimaanawi kwa kuwatuma Mitume ili wakuongozeni kuufikia uongofu kwa kutumia akili, fitra na maumbile yenu. Ni wazi kwamba katika hali hiyo wale watakaoelewa uhakika huo na wakaamini, watapata rehma na fadhila za Allah pamoja na auni na msaada wake. Lakini wale wanaoamua kusimama dhidi ya haki na kuasi amri ya Mwenyezi Mungu watapatwa na adhabu ya Mola. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Mwenyezi Mungu ametimiza dhima yake kwa waja wake kwa kuwapelekea Mitume na miujiza na hoja za wazi kabisa. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa watu waovu na waasi wataadhibiwa baada ya kuwa walishafikishiwa wito wa uongofu na hoja kamili, kwa sababu pasina kufikishiwa hayo, adhabu atakayopewa mtu haitokuwa ya uadilifu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba ni ahadi isiyo na chembe ya shaka ya Allah, kwamba mwisho wa yote waumini watawashinda makafiri na haki itashinda dhidi ya batili.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 48 na 49 ambazo zinasema:

اللَّهُ الَّذِي يُرْسِلُ الرِّيَاحَ فَتُثِيرُ سَحَابًا فَيَبْسُطُهُ فِي السَّمَاء كَيْفَ يَشَاء وَيَجْعَلُهُ كِسَفًا فَتَرَى الْوَدْقَ يَخْرُجُ مِنْ خِلالِهِ فَإِذَا أَصَابَ بِهِ مَن يَشَاء مِنْ عِبَادِهِ إِذَا هُمْ يَسْتَبْشِرُونَ

Mwenyezi Mungu ndiye anaye zituma pepo zikayatimua mawingu, kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo. Na akayafanya mapande mapande, basi ukaiona mvua inatoka ndani yake. Anapo wafikishia awatakao katika waja wake, mara wanakuwa na furaha.

وَإِن كَانُوا مِن قَبْلِ أَن يُنَزَّلَ عَلَيْهِم مِّن قَبْلِهِ لَمُبْلِسِينَ

Na ingawa kabla ya kuteremshiwa walikuwa wenye kukata tamaa.

Kutokana na mwako wa jua na joto lake linalotoa, maji ya bahari hugeuka mvuke na kupanda angani na kugeuka mawingu. Kisha Allah huzipeleka pepo zinazosukuma mawingu hayo na kuyaelekeza hadi kwenye maeneo ya mbali yenye ardhi kavu na yabisi ambapo baada ya kupatikana mazingira ya kimaumbile ya kugeuka mvua, matone safi ya maji hudondoka na kunyesha kwenye ardhi hizo. Adhama ya jambo hili inabainika tunapotafakari na kuelewa kwamba leo hii ili wanadamu waweze kusafirisha na kusambaza gesi, petroli au maji kutoka sehemu moja hadi nyingine wanalazimika kutumia mabilioni ya dola kwa ajili ya kujenga mabomba ya kusambazia, kuchimba mashimo ya chini ya ardhi, kutandika mabomba yenyewe ardhini, kuweka vituo vya udhibiti, utunzaji n.k. Pamoja na kufanya yote hayo, usambazaji huo huweza kukidhi mahitaji ya maeneo fulani tu. Lakini Allah SW ametumia mfumo usio na gharama yoyote kwa mwanadamu ili kuwezesha maji ambayo ndio chanzo cha uhai, yaweze kuwafikia wakaazi wote wa sayari ya dunia; na kuwafanya waneemeke nayo si binadamu peke yao bali viumbe vyote hai vilivyoko kwenye sayari hii.

Kunyesha kwa mvua hakukineemeshi kiwiliwili tu cha mwanadamu bali huipa faraja pia roho na nafsi yake. Kuangalia mandhari ya kufurahisha ya unyeshaji mvua pamoja na maua, bustani na konde zinazonawiri kutokana na kunyeshewa na maji hayo humpa furaha, ukunjufu na uchangamfu kila mtu na kumwondolea hali ya simanzi na huzuni. Mkulima au mfugaji anayetaabika kwa uhaba wa maji au ukame na ambaye anakiona kila alichokitaabikia kiko kwenye hatari ya kumtoka, wakati anapoliona wingu limetanda likiandamana na umeme wa matarajio ya kunyesha mvua, mwanga wa matumaini huangazia macho yake na tabasamu la furaha hujaa midomoni mwake. Hayo ndio matumaini ya kupata rehma na fadhila zisizohesabika za Allah ambazo bishara zake hutolewa na pepo zivumazo na mvua zinyeshazo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tusiyachukulie matukio ya kimaumbile kuwa mambo yanayotokea kwa sadfa na kwa bahati tu. Yote hayo ni alama ya qudra, uwezo na hekima ya Mwenyezi Mungu katika kuendesha masuala yote ya ulimwengu wa uumbaji yakiwemo ya sayari yetu hii ya dunia. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa irada ya Allah imepanga mambo yote katika ulimwengu wa maumbile yafanyike kupitia sababu na visababishi vya kimaumbile, na mfumo mzima wa sababu na natija au matokeo umeumbwa na Mola Mwenyezi mwenye Hekima. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba kuzingatia fadhila na rehma zisizo na ukomo za Allah SW ni tiba na ponyo la hali ya kupoteza matumaini na kukata tamaa ndani ya nafsi ya mwanadamu. Bila ya shaka kila penye ugumu hufuatiwa na wepesi na kila penye dhiki hufuatiwa na faraja. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 727 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie ukunjufu wa riziki ya halali kwa rehma zake na asiyafanye madhambi yetu kizuizi cha kukosa fadhila zake. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/ 

 

Tags