Jan 24, 2017 09:53 UTC

Sura ya Ar-Rum, aya ya 50-54 (Darsa ya 728)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 728 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 30 ya Ar-Rum. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 50 na 51 ambazo zinasema:

فَانظُرْ إِلَى آثَارِ رَحْمَتِ اللَّهِ كَيْفَ يُحْيِي الأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا إِنَّ ذَلِكَ لَمُحْيِي الْمَوْتَى وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

Basi ziangalie athari za rehema ya Mwenyezi Mungu, jinsi anavyo ihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Basi hakika huyo, bila ya shaka, ndiye Mwenye kuhuisha wafu. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu.

 وَلَئِنْ أَرْسَلْنَا رِيحًا فَرَأَوْهُ مُصْفَرًّا لَّظَلُّوا مِن بَعْدِهِ يَكْفُرُونَ

Na kama tungeutuma upepo na wakauona umekuwa rangi ya manjano, juu ya hayo wangeendelea kukufuru.

Katika darsa iliyopita tulitaja nukta kadhaa kuhusu upepo na mvua na nafasi yao katika kuirutubisha na kuinawirisha ardhi ya sayari hii ya dunia pamoja na wakaazi wake. Aya hizi tulizosoma zinaeleza kwamba: upepo na mvua vinafanya kazi kwa amri ya Mwenyezi Mungu; na kuathiri kwa viwili hivyo pia kuko kwenye mamlaka yake Yeye Mola. Akitaka Yeye Allah, mvua huwa sababu ya rehma kutokana na upepo na mvua hiyo kuhuisha na kuinawirisha mimea kwa kuifanya ichipue; na kuwa ya kijani kibichi ardhi iliyokuwa imekufa wakati wa msimu wa baridi na wa jua kali la ukame. Na pia atakapo Yeye Mola, anaweza kutuma upepo wa kuunguza ukayakausha mazao yote na kuyapukutisha chini majani ya kijani ya miti yakawa kama yanavyokuwa majani ya manjano yaliyokauka wakati wa msimu wa mapukutiko.

Mvua wapenzi wasikilizaji, ina athari na baraka nyingi mno kwa maisha ya wanadamu na viumbe vingine hai katika ardhi. Kunawiri kwa rangi ya kijani kibichi mimea na miti, kuwa safi na mwanana hali ya hewa, kujaa maji visima na chemchemi, kutiririka maji ya mito na maporomoko na kuwepo kadiri na wastani wa joto la hali ya hewa, yote hayo ni sehemu tu ya athari za rehma hiyo kubwa ya Allah. Pamoja na hayo haifai fikra zetu zikomee kwenye vitu hivyo vya kimaumbile na visababishi vyake; bali tuondoe fikra na mtazamo wetu kwenye ulimwengu wa leo wa kimaada na kuuelekeza kwenye ulimwengu wa baada ya kifo na kuamini kwamba Mwenyezi Mungu ni Mweza pia wa kufufua wafu Siku ya Kiyama na kuwapa uhai tena. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Quráni inaitaja mvua kuwa ni rehma ya Allah inayoipa uhai ardhi na wakaazi wa sayari hii ya dunia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kunyesha mvua na kuhuika tena ardhi ni ishara na alama ya qudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla wa kuileta Siku ya Kiyama na kuwafufua tena viumbe. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba watu wenye subira ndogo ya kukabiliana na matatizo, misukosuko na matukio machungu ni rahisi kupoteza dini na imani zao na kumkufuru Mwenyezi Mungu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 52 na 53 ambazo zinasema:

فَإِنَّكَ لا تُسْمِعُ الْمَوْتَى وَلا تُسْمِعُ الصُّمَّ الدُّعَاء إِذَا وَلَّوْا مُدْبِرِينَ

Kwa hakika wewe huwezi kuwasikilizisha wafu, wala kuwasikilizisha viziwi wito wakisha geuka kukupa mgongo.

وَمَا أَنتَ بِهَادِي الْعُمْيِ عَن ضَلالَتِهِمْ إِن تُسْمِعُ إِلاَّ مَن يُؤْمِنُ بِآيَاتِنَا فَهُم مُّسْلِمُونَ

Wala wewe huwezi kuwaongoza vipofu na upotevu wao. Huwezi kuwasikilizisha ila wale wanao ziamini Aya zetu. Hao ndio Waislamu, walio nyenyekea.

Aya hizi tulizosoma zinawagawanya watu katika makundi manne. Kundi la kwanza ni la watu ambao kidhahiri wako hai, lakini hawafahamu ukweli wowote wa haki na wala hawaiamini. Kundi la pili ni la watu ambao hawako tayari kusikiliza wito wa Mitume. Wao wanayapa mgongo maneno ya haki na kujiweka mbali nayo. Amma kundi la tatu ni la watu ambao hawana macho ya kuonea haki na wamezama kwenye lindi la upotofu. Na kundi la nne ni la watu waumini ambao wanaitafuta haki kwa macho na masikio yao ili waifahamu na kuikubali; na pale haki inapowabainikia husalimu amri mbele yake na kuifuata.

Aya hizi zinaonyesha kuwa katika utamaduni wa Qur'ani, mbali na uhai na mauti ya kimwili, wanadamu wana uhai na mauti ya kiroho pia. Si hasha watu wanaoonekana kidhahiri wamekufa, kwa mtazamo wa Quráni wakawa wako hai kama walivyo wanaokufa shahidi katika njia ya haki; na si ajabu watu wanaoonekana kidhahiri wako hai, kwa mtazamo wa Quráni wakawa ni wafu, kwa sababu wameghariki kwenye dimbwi la upotofu na kuzikosesha nafsi zao nuru ya uongofu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ikiwa mtu hatokuwa na utayari wa kuikubali haki, hata maneno ya Mtume mteule wa Allah hayatomwathiri kitu. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwa na masikio, macho na akili tu hakutoshi. Muhimu zaidi, ni kuwa na moyo wa kuikubali haki ambao humsaidia na kumuelekeza mtu kwenye kuisikiliza, kuiona na kuikubali haki. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kuifanyia inadi, ukaidi na kuipa mgongo haki humtumbukiza mtu kwenye lindi hatari la kina kirefu na lenye giza totoro la upotofu ambalo uwezekano wa kutoka ndani yake ni mdogo mno. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa jukumu la Mitume na viongozi wa dini ni kuwaelimisha na kuwaongoza watu; si kuwalazimisha waikubali haki kwa nguvu. Kadhalika tunajifunza kutokana na aya hizi kwamba imani na itikadi ya moyoni tu haitoshi; lazima mtu ajisalimishe mbele ya haki kwa matendo pia.

Darsa ya 728 ya Quráni inahatimishwa na aya ya 54 ambayo inasema:

اللَّهُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن ضَعْفٍ ثُمَّ جَعَلَ مِن بَعْدِ ضَعْفٍ قُوَّةً ثُمَّ جَعَلَ مِن بَعْدِ قُوَّةٍ ضَعْفًا وَشَيْبَةً يَخْلُقُ مَا يَشَاء وَهُوَ الْعَلِيمُ الْقَدِيرُ

Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni katika udhaifu kisha akajaalia nguvu baada ya udhaifu, kisha akajaalia baada ya nguvu udhaifu tena na uzee. Anaumba atakavyo. Naye ndiye Mjuzi, Mwenye uweza.

Kwa kuwa maudhui kuu ya sura hii ya Ar-Rum ni kubainisha neema za Mwenyezi Mungu na ishara za Tauhidi, aya hii ya 54 imeashiria awamu na vipindi tofauti vya uhai wa mwanadamu, tangu anakoanzia hadi anakoishia na kueleza kwamba, wakati unapotoka tumboni mwa mama hadi kipindi cha miaka kadhaa ya mwanzo, wewe kiumbe mwanadamu ulikuwa dhaifu usiyejiweza. Lakini ulipofikia umri wa uchipukizi hadi ujana, ukawa shababi mwenye nguvu; na ulipofikia umri wa uzee ukawa dhaifu tena usiyejiweza ukucha wala kidole. Hizi ni marhala zilizowekwa na Allah SW; na wewe mwanadamu huhusiki katika hilo kwa namna yoyote.

Kwa hakika laiti kama uumbaji ungekuwa kwenye mamlaka ya mwanadamu, hakuna yeyote miongoni mwetu ambaye angependa azeeke, adhoofike na kupoteza nguvu na uwezo wake wa kimwili. Kwa hivyo nguvu na uwezo wa ujana pia hauko kwenye mamlaka na hiyari ya mtu, hata aweze kuudumisha na kubaki nao katika kipindi cha uzeeni. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mwanzo na mwisho wa mwanadamu ni udhaifu. Haifai kwa mtu ambaye hali yake iko baina ya vipindi viwili vya udhaifu, kuwa na ghururi na majivuno kwa sababu ya miaka michache ya kuishi katika hali ya nguvu na siha. Aidha kwa kuzingatia kwamba kipindi tunapokuwa na nguvu na uwezo ni kifupi, inapasa tuijue thamani yake na kukitumia vizuri na kwa namna bora kabisa. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa vipindi na awamu za udhaifu, na uwezo na nguvu anavyopitia mwanadamu vimewekwa kwa hekima na Allah SW aliye mweza wa kila kitu. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuzitumia katika njia ya kheri neema za nguvu za kimwili za kipindi cha ujana pamoja na fursa hii ya kupita ya uhai wa kidunia. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/     

 

Tags