Jan 24, 2017 09:58 UTC

Sura ya Ar-Rum, aya ya 55-60 (Darsa ya 729)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 729 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 30 ya Ar-Rum. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 55, 56 na 57 ambazo zinasema:

وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ يُقْسِمُ الْمُجْرِمُونَ مَا لَبِثُوا غَيْرَ سَاعَةٍ كَذَلِكَ كَانُوا يُؤْفَكُونَ

Na siku itakapo simama Saa wakosefu wataapa kwamba hawakukaa duniani ila saa moja tu. Hivyo ndivyo walivyo kuwa wakigeuzwa.

وَقَالَ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ وَالإِيمَانَ لَقَدْ لَبِثْتُمْ فِي كِتَابِ اللَّهِ إِلَى يَوْمِ الْبَعْثِ فَهَذَا يَوْمُ الْبَعْثِ وَلَكِنَّكُمْ كُنتُمْ لا تَعْلَمُونَ

Na walio pewa ilimu na Imani watasema: Hakika nyinyi mlikwisha kaa katika hukumu ya Mwenyezi Mungu mpaka Siku ya kufufuliwa. Basi hii ndiyo Siku ya kufufuliwa! Lakini nyinyi mlikuwa hamjui.

فَيَوْمَئِذٍ لّا يَنفَعُ الَّذِينَ ظَلَمُوا مَعْذِرَتُهُمْ وَلا هُمْ يُسْتَعْتَبُونَ

Basi Siku hiyo hautawafaa walio dhulumu udhuru wao, wala hawatopokelewa toba yao. 

Moja ya sifa za watu waovu na wanaoikufuru haki ni kwamba, wanapokuwa hapa duniani wanakana na wala hawakubali kuwepo siku ya kufufuliwa. Kwa mujibu wa aya tulizosoma, watu wa aina hii hata ifikapo Siku ya Kiyama pia hawatokuwa tayari kuungama kwamba Kiyama kimejiri na wao wamesimamishwa kwenye uwanja wa hisabu. Hivyo watasema, hapa tulipo tunaendelea kuwa katika dunia ileile. Kilichotokea ni kuwa tumelala kwa muda tu na sasa tumeamka. Lakini watu waumini walioitambua haki na waelewa wa hakika ya mambo watawaambia watu hao: Hii ni Siku ya Kiyama; na kulingana na alivyokadiria Mwenyezi Mungu, nyinyi mumepita kwenye kipindi cha barzakhi cha baina ya duniani na Kiyama na leo mumehudhurishwa kwenye mahakama ya siku hiyo. Wakati madhalimu na waovu watakapodhihirikiwa na ukweli halisi wa kitu kiitwacho Mahakama ya Kiyama, hapo sasa, ndipo watataka kuomba msamaha na maghufira na kutubia. Lakini kwa mujibu wa aya hizi, uombaji radhi huo wa waovu katika siku hiyo hautokuwa na faida yoyote na wala toba yao haitokubaliwa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba fikra pogo humuelekeza mtu kwenye njia pogo. Upotofu katika fikra na itikadi huandaa mazingira ya kuenea maovu na madhambi katika jamii. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa elimu na imani vina uhusiano wa pande mbili. Elimu ya kweli inamwita mtu kwenye imani na kuikubali haki; na imani sahihi inawashajiisha watu kujifunza elimu na ujuzi. Aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba hatima ya mwanadamu imefungamana na amali zake. Dhulma na uovu anaofanya mtu, havitokuwa na mwisho mwema kwake kuanzia hapa duniani mpaka huko akhera. Kadhalika aya hizi zinatutanabahisha kuwa kuomba msamaha na kutubia mtu kwa madhambi aliyofanya kutakuwa na faida kwake endapo kutafanyika hapa duniani; ama kwenda kutubia huko akhera hakutokuwa na tija yoyote.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 58 na 59 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ ضَرَبْنَا لِلنَّاسِ فِي هَذَا الْقُرْآنِ مِن كُلِّ مَثَلٍ وَلَئِن جِئْتَهُم بِآيَةٍ لَيَقُولَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ أَنتُمْ إِلاَّ مُبْطِلُونَ

Na hakika tulikwisha wapigia watu kila mfano katika hii Qur'ani. Na ukiwaletea Ishara yoyote bila shaka walio kufuru watasema: Nyinyi si chochote ila ni wabatilifu. 

كَذَلِكَ يَطْبَعُ اللَّهُ عَلَى قُلُوبِ الَّذِينَ لا يَعْلَمُونَ

Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo piga muhuri kwenye nyoyo za wasio jua.

Qur'ani wapenzi wasikilizaji ni kitabu cha mwongozo wa uongofu, na yale yote yenye taathira kwa ajili ya uongofu wa mwanadamu yamebainishwa ndani ya kitabu hicho; yaani bishara njema na indhari, mwongozo na mawaidha, maamrisho na makatazo, ushajiishaji na ukemeaji, hoja na burhani pamoja na kila njia na taratibu za kuandaa mazingira ya uongofu kwa mtu na kumweka mbali na upotofu.

Hoja za Tauhidi na kumwabudu Mungu pekee wa haki zimeelezwa katika aya tofauti za Qur'ani. Ndani ya kitabu hiki cha mbinguni zimebainishwa kwa njia mbalimbali njia na utaratibu sahihi wa kuishi na kujiweka mbali na sifa chafu za kiakhlaqi. Imeelezwa pia ndani yake namna ya kumwabudu Allah usiku na mchana katika masiku tofauti ya mwaka. Katika jumla ya aya zake zaidi ya 6,000, kitabu kitukufu cha Qur'ani kimezungumzia kwa sura na namna tofauti itikadi, hukumu za ufanyaji mambo na akhlaqi, ambavyo ni misingi ya kifikra na kivitendo ya kila mtu ampwekeshaye na kumwabudu Mola mmoja tu wa haki. Pamoja na hayo, watu ambao hawataki kuikubali haki na wameamua kuikufuru, kuikaidi na kuikana wanayaona yote haya ni mambo batili na yasiyo na msingi wala mashiko; bali hufikia hadi ya kutokuwa tayari hata kuzisikiliza aya za Mwenyezi Mungu. Kisha aya zinaendelea kwa kueleza sababu ya ukafiri na ukanushaji huo kwa kusema: Kutokana na kukithirisha na kushupalia kwao kufanya madhambi, Mwenyezi Mungu SW amepiga muhuri juu ya nyoyo za watu wa aina hiyo na hivyo wameipoteza neema ya kuitambua na kuifahamu haki. Ni sawa kama walivyo wezi waliokubuhu katika kufanya jinai na uhalifu wanaotiwa jela na kufungiwa kwenye selo. Uhalifu waliotenda wezi hao ndio unaomfanya jaji asiwe na njia nyingine ya kutekelezea uadilifu isipokuwa kuwahukumu kifungo. Matokeo yake ni watu hao kuikosa neema ya uhuru. Kwa hivyo ikiwa wafanya madhambi nao pia watatubia na kuacha maovu Mwenyezi Mungu atawasamehe; la kama wataendelea kufanya madhambi na maasi nyoyo zao zitatiwa kufuli na kuikosa neema ya kuielewa haki. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Quráni imeletwa kwa ajili ya wanadamu wote; na inatumia njia na mbinu mbali mbali kwa ajili ya kuyaongoza na kuyaelekeza matabaka tofauti ya watu kwenye uongofu. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa watu waliofadhilisha kufuata njia ya batili, sio tu hawaikubali haki bali wanaiona haki yenyewe kuwa ni batili na waumini wanaoifuata pia ni wafuasi wa batili. Hivyo tujihadhari tusije tukatekwa na kuathiriwa na propaganda za wafuasi wa njia ya batili. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba malipo ya ukafiri na kuifanyia inadi haki ni kuikosa neema ya uongofu wa Allah; na bila ya shaka hasara ya jambo hilo inamrejea mwanadamu mwenyewe; si Yeye Mola.

Darsa ya 729 ya Quráni inahatimishwa na aya ya 60 ambayo inasema:

فَاصْبِرْ إِنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ وَلا يَسْتَخِفَّنَّكَ الَّذِينَ لا يُوقِنُونَ

Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Wala wasikuhafifishe wale wasio kuwa na yakini.

Aya hii, ambayo ndiyo aya ya mwisho pia ya sura hii ya Ar-Rum inasema: Katika zama zote za historia waumini wamekuwa daima wakiandamwa na kauli za kuudhi na kubughudhi na miamala ya manyanyaso na mateso ya makafiri. Kwa sababu hiyo wanatakiwa wawe na subira na uvumilivu na wala wasitetereshwe na vitisho na rabsha zao. Kwa sababu Allah SW ameahidi kwamba ikiwa waumini watasimama imara na wakawa na istiqama, bila ya shaka watashinda tu. Kisha aya inaendelea kwa kumhutubu Bwana Mtume SAW na waumini ya kwamba: Kama mtaathiriwa na maneno yao mtapatwa na hofu na taharuki; hivyo badala ya muqawama na kusimama imara mtajidogesha na kujidunisha nafsi zenu na kuishia kufanya mambo duni na yasiyo na thamani. Au kutokana na kuathiriwa na maneno mabaya ya maadui mtahamaki na kukasirika kufika hadi ya kupoteza utulivu na udhibiti wa nafsi na kuishia kufanya mambo yatakayosababisha mupoteze hadhi zenu na kuyumbisha nafasi yenu katika jamii. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba waumini wanatakiwa wawe thabiti na wasimame imara katika njia yao na wawe na subira na uvumilivu kutokana na mwenendo mbaya wa maadui. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa rabsha na makelele ya watu wasio na imani na wasiojali dini yasituathiri katika uchukuaji wetu wa maamuzi.  Tuiamini ahadi ya Mwenyezi Mungu ya ushindi wa watu wa haki dhidi ya watu wa batili; kwani imani hiyo itatupa hakikisho la utulivu wa nafsi. Vilevile aya hii inatutaka tuelewe kwamba watu wasio na subira na uvumilivu huwa duni na hafifu katika jamii. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 729 ya Quráni imefikia tamati; na kama nilivyotangulia kueleza, ndiyo inayohatimisha tarjumi na maelezo ya sura ya 30 ya Quráni tukufu ya Ar-Rum. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuyatekeleza yale yote tuliyojifunza katika sura hii. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/ 

Tags