Maadhimisho ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sehemu ya Pili)
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka hapa mjini Tehran, na karibuni kusikiliza sehemu ya pili ya vipindi hivi maalumu ambavyo tumekuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaingia katika mwaka wa 38 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Miaka hii yote inapasa kuchukuliwa kuwa ni miaka ya kuvumilia matatizo na machungu na wakati huohuo kupata uzoefu na ukakamavu wa kisiasa na kiuchumi katika mapambano ya taifa la Iran mkabala wa mashinikizo, mapungufu na vikwazo.
Marekani na washirika wake wamekuwa wakitumia kila mbinu na fursa kuizuia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufikia maendeleo ya kielimu na kiteknolojia. Wamewekeza pakubwa katika kuidhoofisha Iran na kuifanya isiweze kufikia lengo lake hilo kuu la kielimu. Katika kipindi hiki chote, Marekani imekuwa ikitumia chombo cha mashinikizo yakiwemo ya vikwazo vya mafuta, kuvuruga soko la fedha za kigeni na bidhaa, kuzuia uwekezaji wa kigeni na kutoa vitisho vya mashambulio ya kijeshi dhidi ya Iran lakini pamoja na hayo yote imeshindwa kabisa kuitenga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ngazi za kimataifa. Hivi sasa pia ambapo Marekani imeanza kutawaliwa na rais mpya aliye na misimamo ya kipekee inayowashangaza wengi duniani, nchi hiyo bado ina ndoto nyingi kuhusiana na taifa la Iran. Pamoja na hayo rais huyo anashauriwa kuchukua msimamo wa kimantiki kwa kutazama historia ya waliomtangulia katika utawala wa nchi hiyo, na hasa ya rais aliyeondoka madarakani hivi karibuni wa nchi hiyo Barack Obama. Baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia huko Vienna Austria kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la nchi 6 za 5+1, Rais Barack Obama katika mahojiano yake na gazeti la New York Times alikiri waziwazi kushindwa Marekani kurefusha muda wa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran.
Huenda Donald Trump ambaye ni mwanagenzi katika siasa za Marekani, haufahamu vyema mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa hivyo anapasa kutalii na kuchunguza kwa makini historia ya waliomtangulia kuhusiana na suala zima la Iran. Vitisho vidogo na vikubwa vya watawala wa Marekani katika miaka hii yote havijafua dafu mbele ya irada thabiti ya mapambano ya taifa la Iran. Taifa hili limesimama imara katika nyanja za kazi, juhudi na ukakamavu na kubadilisha matatizo, vitisho, changamoto na vikwazo mbalimbali kuwa fursa ya kujijengea mustakbali mwema. Limetumia uwezo wake wote kukata kila aina ya utegemezi. Taifa la Iran linajua vyema chanzo cha kubakia nyuma kimaendeleo katika kipindi cha miaka 200 iliyopita na kutambua kwamba njia ya kujitawala halisi inapatikana katika maenedeleo ya kielimu na teknolojia ya kisasa. Ni kwa kutilia maanani suala hilo ndipo katika kujibu chokochoko za maadui, taifa la Iran likaamua kusimama imara kama lilivyofanya katika medani ya vita vya kijeshi. Limesimama imara katika medani ya elimu kwa anwani ya jihadi kubwa na kupambana vikali kwa ajili ya kufikia malengo ya kielimu na maendeleo katika nyanja za elimu za kisasa, na bila shaka limelipa gharama kubwa katika njia hiyo. Mashahidi wa nyuklia wa Iran yaani wasomi na wanasayansi wa Iran ambao waliuawa hivi karibuni na vibaraka wa Marekani na utawala haramu wa Israel ni thibitisho tosha la mapambano endelevu ya Iran katika uwanja wa elimu na taaluma.
Takwimu za kimataifa za uzalishaji elimu zinaonyesha kwamba katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa na mwenendo endelevu na wa kudumu wa uzalishaji elimu kwa kadiri kwamba mwishoni mwa mwaka 2014, taifa hili lilikuwa la kwanza kati ya nchi za Kiislamu na za Mashariki ya Kati na ya 16 kimataifa katika uzalishaji wa elimu.
Iran imepiga hatua kubwa na muhimu katika uwanja wa elimu na hasa katika sekta ya uzalishaji wa seli shina. Katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Chuo cha Utafiti cha Ruyan kina mchango mkubwa katika uwanja huo kwa kadiri kwamba kimefanikiwa pia kupata elimu ya ushabihishaji viumbe (cloning). Miaka kadhaa iliyopita Iran ilifanikiwa kurusha katika anga za mbali satalaiti za Navid, Rasad na Fajr na pia kutuma katika anga hizo wanyama hai kwa malengo ya utafiti wa kielimu. Yote hayo yalifanyika katika kipindi ambacho Iran ilikuwa imewekewa vikwazo vikali vya kimataifa, jambo linalothibitisha wazi kwamba mipango ya utafiti wa anga za mbali ya Iran si suala la muda mfupi tu bali ni mpango wa muda mrefu unaotekelezwa kwa makini na uangalifu mkubwa. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi pekee ya eneo la Mashariki ya Kati ambayo imeweza kuwatumia wasomi na wanasayansi wake wa ndani kufanikisha mipango kama hiyo muhimu ya kurusha angani satalaiti za utafiti katika nyanja tofauti za kielimu, na bila shaka itapanua zaidi uwanja huo katika siku zijazo. Hivi sasa Iran imewekwa kwenye orodha ya nchi tano zenye nguvu zinazoinukia katika masuala ya anga za mbali. Kwa kurusha angani satalaiti ya Omid, Iran ilifanikiwa kujiunga na nchi chache duniani zilizo na teknolojia na uwezo wa kutengeneza na kurusha angani satalaiti za utafiti.
Faisal Qasim, ambaye ni mmoja wa watangazaji mashuhuri wa televisheni ya al-Jazeera wanaoipinga vikali Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na harakati za mapambano ya Kiislamu katika eneo anasema hivi kahusu suala hilo: ‘Waarabu wanapasa kuiga mfano wa Iran katika suala la uwekezaji, kuwa na mipango, subira na kusimama imara. Badala ya kukemea na kuilaumu tu Iran, wanapasa kuwa na mipango madhubuti ya kukabiliana nayo. Tazameni busara na werevu wa Iran na jinsi imeweza kutumia vyanzo na utajiri wake katika njia ya kujitosheleza kwa muda mrefu na sasa imebadilika na kuwa nguvu kubwa ambayo haiwezi kupuuzwa katika matukio ya kieneo na kimataifa.’
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Taasisi ya Kielimu ya Scopus, ambayo hupima na kutathmini ustawi wa kielimu katika nchi tofauti za dunia, mwaka 2013 Iran iliweza kujipatia nafasi ya nane kimataifa katika uwanja wa uchapishaji wa makala za taaluma ya nano. Kufikia sasa ni nchi chache sana ulimwenguni ambazo zimefanikiwa kuchapisha na kubuni mipango ya kitaifa ya nano, na Iran ni moja ya nchi hizo chache. Imeweza kuzalisha zaidi ya bidhaa 3000 za nano katika nyanja tofauti za viwanda, dawa na tiba na bidhaa zinazohitajika katika viwanda vinavyojishughulisha na masuala ya teknolojia ya nano. Teknolojia ya nano ina umuhimu mkubwa katika nyanja tofauti zikiwemo za uzalishaji na uwekaji akiba ya nishati, kuzidisha umri wa mazao ya kilimo, uondoaji sumu kwenye maji, ugunduzi na uainishaji wa magonjwa, usambazaji na hifadhi ya madawa, usafishaji hewa, kudhibiti maradhi na mambo mengine mengi. Kuhusu suala hilo Herzi Halevi, Mkuu wa Idara ya Habari za Kijeshi ya utawala haramu wa Israel anasema: ‘’Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka kadhaa iliyopita imefanikiwa kupata maenedeleo makubwa katika uwanja wa elimu na teknolojia. Imeweza kupata maendeleo makubwa katika elimu za kisasa ikiwemo ya kuzalisha viumbe vinavyoshabihiana (cloning), seli shina na utengenezaji madawa. Licha ya kuwepo vikwazo lakini baada ya Mapinduzi, Iran imeweza kusomesha na kuwalea wataalamu katika sekta za utengenezaji ndege, taaluma za afya na tiba na kupata mafanikio makubwa katika nyanja hizo. Leo tunakabiliwa na ukweli huu usiopingika kwamba Iran ya Kiislamu imeweza kukwea vilele vya juu zaidi kielimu, kiufundi na teknolojia ya kisasa ulimwenguni na kupata mafanikio makubwa katika nyanja hizo.’’
Mafanikio haya yamepatikana katika mazingira ambayo Marekani ilikuwa imeeneza vikwazo vyake hadi kufikia kupiga marufuku uchapishaji wa makala za kielimu za Iran katika majarida na magazeti ya nchi za Magharibi na kuzuia wanafunzi na wasomi wa Iran kushiriki katika semina na makongamano ya kielimu ya Marekani na nchi za Ulaya. Wasomi na wanasayansi wa nyuklia wa Iran waliwekwa kwenye orodha ya watu waliowekewa vikwazo na nchi za Magharibi na baadhi yao kuuawa kigaidi na vibaraka wa nchi hizo hapa nchini. Kwa hakika jambo hilo lilikuwa tangazo la vita vya moja kwa moja vya kielimu dhidi ya Iran. Kutokana na siasa zao za chuki dhidi ya Iran nchi za Magharibi hata zilikataa kuiuzia Iran fueli iliyopasa kutumika katika tanuri la utafiti wa kielimu la Chuo Kikuu cha Tehran, jambo ambalo liliisukuma Iran ukutani na kuifanya kutokuwa na chaguo jingine isipokuwa kutegemea wasomi na wataalamu wake wa ndani katika kuzalisha fueli hiyo ya nyuklia ili ipate kutumika katika masuala ya utafiti wa kiviwanda na kitiba.
Zaidi ya asilimia 90 ya biashara ya Iran hufanyika kupitia njia za baharini na takriban mafuta yote ya nchi hii huuzwa nje kupitia meli za mafuta. Kwa msingi huo meli za mizigo na mafuta za Iran hukata masafa marefu ili kufikia masoko ya kimataifa katika pembe tofauti za dunia. Takriban meli zote za mizigo na mafuta hutumia fueli inayotokana na visukuku (fossil). Hata kama fueli hiyo ni rahisi lakini katika miaka ya hivi karibuni baadhi ya nchi kama vile Marekani, China na Russia zimekuwa zikitekeleza mipango ya kuzalisha fueli ya nyuklia ili itumike kwenye meli hizo badala ya fueli ya visukuku.
Katika moja ya makala zake, gazeti la Christian Science Monitor la nchini Marekani liliashiria vikwazo na athari zake kwa uchumi wa Iran na kuandika kwamba vikwazo hivyo vimeipelekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuchukua hatua ya kujiendeleza kielimu. Kwa mujibu wa gazeti hilo, vikwazo hivyo havijaweza kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa sababu kila mara vikwazo hivyo vinapozidishwa ndivyo Iran inavyopata azma na moyo zaidi wa kujiendeleza katika kila nyanja.
Bila shaka vikwazo hivyo vinatokana na ukakamavu na mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya mashinikizo ya kidhulma yanayotolewa dhidi yao na udhihirishaji wa vipawa vikubwa vya kielimu walivyonavyo. Suala hili linathibitisha wazi kwamba hakuna vikwazo wala vizuizi vyovyote vinavyoweza kulizuia taifa la Iran kufikia maendeleo na vilele vya juu zaidi kielimu.