Jumanne, 21 Februari, 2017
Leo ni Jumanne tarehe 23 Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na 21 Februari, 2017.
Siku kama ya leo miaka 197 iliyopita, alizaliwa Reinhart Dozy, mtaalamu wa masuala ya mashariki mwa dunia raia wa Uholanzi. Dozy alizamili katika fani za historia na lugha huku akifikia daraja ya PHD katika fani ya fasihi akiwa na umri wa miaka 24. Reinhart Dozy alipendelea sana kusomea tamaduni za Kiislamu ambapo mbali na kuwa mahiri katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kijerumani, alikuwa pia mtaalamu katika lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Uholanzi alifanya utafiti mwingi wa tamaduni za Kiarabu na historia ya Kiislamu, hususan Waislamu wa Andalusia, kusini mwa Uhispania. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Historia ya kisiasa na tamaduni za Kiarabu katika Andalusia' 'Historia ya Uislamu kuanzia mwanzo wake hadi katikati ya karne ya 19' na 'Tamaduni za mavazi ya Kiislamu.' Reinhart Dozy alifariki dunia mwaka 1883.
Miaka 133 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sayyid Muhammad Ibrahim mashuhuri kwa lakabu ya Sayyidul Ulamaa, alimu na fakihi wa Kiislamu wa nchini India. Alikuwa mmoja wa maulama watajika na mahiri mwanzoni mwa karne ya 14 Hijria. Baada ya kufariki dunia baba yake, Muhammad Ibrahim alichukua jukumu la baba yake la kueneza mafundisho ya dini katika baadhi ya miji ya India. Mwanazuoni huyo alifanya hima kubwa ya kueneza misingi na itikadi za Kiislamu katika ardhi ya India.
Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, inayosadifiana na 21 Februari 1916 vilianza vita vikubwa vya umwagikaji damu vilivyojulikana kwa jina la 'Verdun' kati ya Ujerumani na Ufaransa. Vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa miezi kumi vilimalizika kwa kushindwa vikosi vya Ujerumani na wanajeshi karibu milioni moja wa nchi hizo mbili kuuawa. Kushindwa huko ni miongoni mwa sababu za kushindwa Ujerumani kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia.

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, wananchi wa Misri na Syria walishiriki kwenye kura ya maoni ya kuunganisha nchi mbili hizo chini ya Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Wananchi wa nchi hizo mbili walimchagua Jamal Abdul-Nasser kiongozi wa wakati huo wa Misri, kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Baada ya kupita miezi kadhaa, Yemen nayo ilijiunga kwenye muungano huo. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa zaidi ya miaka mitatu, kwani Syria ilitangaza kujitoa kwenye muungano huo kutokana na kutoridhishwa na uongozi wa Jamal Abdul-Nasser.
Tarehe 21 Februari miaka 52 iliyopita, Malcolm X, Mmarekani mweusi aliuawa baada ya kushambuliwa na magaidi nchini humo. Malcolm X alizaliwa mwaka 1925, na wakati alipokuwa kwenye rika la ujana alifahamiana na makundi ya vijana wa Kiislamu na hatimaye kusilimu. Itikadi ya mwanaharakati huyo wa Kiislamu iliwachukiza watawala wa Marekani na makundi ya ubaguzi wa rangi nchini Marekani. Malcolm X aliuawa akihutubia mkutano. Alikuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, Wamarekani weusi ambao wanakandamizwa na kubaguliwa na serikali ya Marekani wanaweza kujipatia uhuru na uadilifu chini ya mwavuli wa utawala wa Kiislamu.
Katika siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, wapiganaji shupavu wa Iran walianzisha operesheni ya 'Khaybar' dhidi ya majeshi ya Iraq, kwenye vita vya kulazimishwa vilivyoazishwa na utawala wa Baath wa Saddam Hussein. Katika operesheni hiyo iliyofanyika katika eneo la Hoor al Hoveyzeh kusini magharibi mwa Iran, wapiganaji shupavu wa Iran walifanikiwa kuvuka maji na kukiteka kisiwa chenye utajiri mkubwa wa mafuta cha Majnoon, kilichoko karibu na mji wa Basra kusini mashariki mwa Iraq.
