Mar 01, 2017 08:34 UTC
  • Iran yaunda mashine ya kusafisha maji ya chumvi inayotumia nguvu za jua

Karibuni katika mjumuiko huu wa vipindi ambavyo huangazia maendeleo mapya katika sekta za sayansi, teknolojia na tiba duniani na hasa nchini Iran na baadhi ya maeneo mengine duniani. Leo tutaangazia mafanikio ya Iran katika kuunda mashine ya kusafisha maji ya chumvi inayotumia nishati ya jua. Karibuni

Kuwepo maji matamu ambayo  ni safi na salama ya kunywa ni kati ya masuala muhimu na ya kimsingi katika maisha ya mwanadamu. Kwa kawaida maji ya mvua, chemichemi, theluji iliyoyeyuka, ya mtoni au ziwani huitwa "maji matamu" kwa maana kwamba kimsingi yanafaa kunywewa au kumwagilia mimea.

Moja ya matatizo makubwa katika nchi za ulimwengu wa tatu na hasa barani Afrika na Mashariki ya Kati ni upatikanaji wa maji matamu ambayo ni salama kwa mwanadamu. Karibu asilimia 71 ya eneo lote la sayari ya dunia limefunikwa kwa maji lakini asilimia 97 ya maji hayo ni ya chumvi na hayafai kwa ajili ya kunywa. Ni asilimia moja tu ya maji ya kunywa duniani ndiyo yanyopatikana kwa urahisi. Pamoja na hayo tunaona kukiwa na ubadhirifu mkubwa wa maji matamu. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, karbu watu bilioni 1.2 duniani (asilimia 17 ya watu wote duniani) wanakabilwia na uhaba wa maji safi ya kunywa

Kwa hivyo kuhakikisha kuwa kunapatikana maji safi na salama ya kunywa kote duniani ni jambo muhimu sana na kwa msingi huo kunafanyika jitihada za kuhakikisha maji hayo yanapatikana kwa njia za utumizi wa teknolojia mpya. Leo maeneo mengi duniani kwa kuzingatia ustawi wa kasi wa idadi ya watu yanakabiliwa na tatizo la kukidhi mahitaji ya maji matamu. Taathira mbaya za ukosefu wa maji matamu ni kuzorota afya ya umma na pia kupungua mazao ya kilimo.

Katika kuisaidia jamii ya mwanadamu kukabiliana na tatizo hilo, wanasayansi wa Iran wamefanikiwa kuunda mashine ya kuyafanya maji ya chumvi yawe matamu. Mashine hiyo inatumia nishati ya jua kufanya kazi hiyo muhimu na hivyo inaweza kutumiwa katika maeneo ya mbali yasiyo na umeme wa kawaida. Watafiti Wairani kwa kutumia teknolojia ya mabomba ombwe wamefanikiwa kuyafanya maji ya chumvi yawe matamu kwa kutumia mashine yenye kutegemea nishati ya jua. Mbali na kusafisha maji ya chumi na kuyafanya yawe matamu, mshine hiyo pia ina uwezo wa kusafisha maji ya kawaida yenye vijidudu na kuyafanya yawe salama kwa ajili ya mwanadamu kuyanywa.

@@@@

Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Koroush Khosravi anasema ukosefu wa maji matamu ni moja ya changamoto muhimu nchini Iran na kuongeza kuwa: "Katika ardhi ya Iran kuna kiasi kikubwa cha maji ya chumvi ambayo yanapaswa kubadilishwa kuwa maji matamu bila gharama za juu ili kutosheleza mahitaji ya wakazi wa nchi hii. Kuyafanya maji yawe matamu kwa kutumia nishati ya jua ni moja ya njia muafaka tuliyobuni kwa ajili ya kuyasafisha maji. Katika mbinu hii tumetumia teknolojia ya bomba ombwe. Mashine yenye kutumia teknolojia hii inapata nishati yake kutoka katika jua na kuyabadilisha maji ya chumvi kuwa maji matamu." Mashine hii ina uwezo mkubwa wa kuyafanya maji yaliyo na viwango mbali mbali vya chumvi kuwa matamu.

Bomba ombwe la mashine hii linajumuisha eneo la chini lenye rangi nyeusi na upande mwingine kuna sehemu isiyo na rangi ambapo baina ya pande hizo mbili kuna ombwe. Wakati miale ya jua inapoangazia eneo lisilo na rangi na kupita hadi kufika sehemu nyeusi, eneo hilo jeusi hupata joto na kwa kuzingatia kuna ombwe baina ya maeneo hayo mawili, joto haliwezi kurejea katika anga na hivyo jote katika eneo hilo hupelekea hali ya unyevu kuibuka. Katika mazingira kama hayo, maji ya chumvi hungia ndani ya mfumo wa mashine hiyo na joto lililoingia huchemsha maji na kwa kupitia katika condenser maji ya chumvi hubadilika na kuwa maji matamu.

Kwa mujibu wa msimamzi wa mradi huo, Bw. Khosravi, nukta nyingine  muhimu waliyozingatia katika uundaji wa mashine hiyo ya kuyafanya maji ya chumvi kuwa matamu ni kupunguza uchafuzi wa mazingira. Mashine hiyo si tu kuwa inayafanya maji ya chumvi kuwa matamu bali pia inaweza kuyasafisha maji matamu yenye vijidudu na kuyafanya yawe salama kwa ajili ya kutumiwa na mwanadamu.

Katika kufanikisha mradi huu, wataalamu wa mji mdogo  wa Lanjan katika mkoa wa Isfahan wameunda mabati maalumu (solar panel)  ya chombo hicho cha nishati ya jua katika mashine hiyo ya kuyafanya maji ya chumbi kuwa matamu.

Mustafa Doori, mhandisi katika Kituo cha Elimu ya Kiufundi cha mji mdogo wa Lanjan anasema ili kuhakikisha kuwa chombo cha kubadilisha maji ya chumvi kuwa matamu kinatumika katika misimu yote hata msimu wa baridi kali, wataalamu wa kituo hicho wameunda mabati maalumu yaliyo na uwezo wa kuhifadhi nishati.

Kwa msingi huo, mashine hiyo ya kubadilisha maji ya chumvi kuwa matamu imeundwa kwa njia ambayo inatumia nishati jadidika pasina kuwa na madhara yoyote kwa mazingira na pia kwa bei nafuu ambayo watu wa matabaka yote ya jamii wanaweza kuimudu. Mashine hiyo pia inaweza kutumika katika kijiji cha mbali zaidi pasina kuhitajia wataalamu kuisimamia kwani imeundwa kwa teknolojia sahali na haihitajii ukarabati wala usimamizi maalumu.

Naam wapienzi wasikilizaji, makala yetu ya teknolojia mpya inafikia tamati hapa kwa leo ambapo tumeangazia mafanikio ya wataalamu wa Iran katika kuunda mashine ya kusafisha maji ya chumvi inayotumia nishati ya jua. Usikose kujiunga nasi wiki ijayo tukuletee mapya zaidi katika uga wa sayansi, teknolojia na tiba, kwaherini.