Mar 09, 2017 13:59 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 25 ya makala yanayokosoa kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na suna za Bwana Mtume (sawa) mienendo ya makundi ya ukufurishaji yanayotenda jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu wengine.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia uharibifu wa athari za kihistoria, maeneo ya kidini na makaburi ya Mitume na masahaba unaofanywa na makundi ya ukufurishaji ya Kiwahabi ambao pia ni kinyume kabisa na mafundisho ya dini ya Kiislamu. Ama katika kipindi cha leo tutazungumzia jinai nyingine inayofanywa na wanachama wa makundi hayo kwa kuwafanya watumwa wa ngono wanawake wanaowakamata, hivyo endeleeni kuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Ndugu wasikilizaji licha ya dini tukufu ya Kiislamu kusisitiza kwa dalili nyingi juu ya umuhimu wa kuheshimiwa wanawake na kuhifadhiwa haki zao, makundi ya ukufurishaji hususan Daesh (ISIS) na kwa kutumia nara ya dini, yamekuwa yakitekeleza vitendo vilivyo dhidi ya ubinaadamu na ukatili wa kutisha dhidi ya wanawake na hivyo kukiuka wazi wazi haki za binaadamu dhidi ya wanawake hao. Makala rasmi yaliyotolewa na kundi la kigaidi la Daesh kwa anwani ya Dabiq, yalielezea kadhia ya 'kuhuishwa upya vitendo vya utumwa kabla ya siku ya Kiama' na kuchukulia suala la kufanywa watumwa wanawake na watoto wa kabila la Yazidi wa mji wa Sinjar, nchini Iraq kuwa ni jambo la kujivunia na kudai kuwa hiyo ilikuwa ni sehemu ya kuhuishwa baadhi ya mafundisho ya Kiislamu yaliyosahaulika.

Vinara wa kundi la kigaidi la al-Qaidah ambao ndio chanzo cha genge la Daesh (ISIS)

Katika Makala hayo Daesh inasema: "Kwa kitendo hicho Dola la Kiislamu limeweza kuhuisha  sheria iliyokuwa imepotoshwa, yaani wa kuwafanya watu watumwa….Kuzifanya watumwa familia za washirikina ni suala ambalo kwa mara ya kwanza katika sheria za Kiislamu limeweza kutekelezwa baada ya kuwa limeachwa kwa muda mrefu….Hao ni watu waabudu masanamu ambao wanamuabudu shetani." Mwisho wa kunukuu. Aidha yanaendelea kusema: "Baada ya kuwatia mbaroni wanawake wa Yazidi pamoja na watoto wao, waligawiwa kwa wapiganaji wa Dola la Kiislamu la–Daesh- walioshiriki katika vita vya kuudhibiti mji wa Sinjar, huku khumsi yao, yaani moja ya tano yao ikikabidhiwa kwa dola hilo." Mwisho wa kunukuu. Kuhusiana na suala hilo, Zainab Bangura, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa sambamba na kusikitishwa na mwenendo wa wanachama wa kundi hilo la kigaidi katika kuwafanya watumwa wanawake, amesema kuwa ukatili huo wa kutisha unaenda sambamba na ukatili wa karne za kati. Bi, Bangura anafafanua kwa kusema kuwa, kitendo cha wanachama wa kundi hilo kuwaahidi kuwapa wapiganaji wake wasichana bikira, ni njama chafu ya kuwavutia vijana walio wengi kuweza kujiunga na genge hilo. Kupitia Jihadun-Nikah, Daesh huwauza wanawake waliowateka nyara kwa thamani ya Dola 500-2000. Ni kutokana na hilo ndipo kukakithiri visa vichungu vinavyowahusu wanawake waliotekwa nyara na kufanywa watumwa wa ngono, visa ambavyo kwa hakika vinauchoma moyo wa kila mpigania uhuru popote alipo duniani.

*****************************************

Suala la kusikitisha zaidi ni kwamba, wakati Daesh likiasisi mfumo wa utumwa na kuwafanya watu wengine kuwa mateka sanjari na kuwabaka wasichana na wanawake, linadai kutekeleza hayo kupitia harakati iliyopewa istilahi ya kufufua sheria zilizosahaulika, suala ambalo kwa hakika halitambuliwi kwa aina yoyote na dini ya Kiislamu. Hii ni kwa kuwa dini ya Kiislamu ilikuja kupiga vita vitendo vya kuwafanya watu wengine kuwa watumwa. Tokea maelfu ya miaka iliyopita kabla ya kudhihiri Uislamu, suala la kuwafanya watu wengine kuwa watumwa lilikuwa limekita mizizi katika jamii za wanadamu duniani, huku likirithiwa baina ya vizazi.

Wakufurishaji wa Kiwahabi wa Daesh

Aidha utumwa sio jambo ambalo liliasisiwa na dini ya Uislamu kwa kuwanyima watu wengine uhuru wao wa kimaisha, bali lilikuwepo hata kabla ya kuzaliwa kwa Nabii wa Allah Muhammad (saw). Aidha ifahamike kuwa, dini ya Kiislamu kupitia Mtume wake Muhammad haikuhusika kwa aina yoyote katika kuendelezwa jambo hilo, na kinyume chake ilikabiliana vikali na suala hilo kwa njia mbalimbali. Kwa ajili hiyo kauli ya wanachama wa kundi la Daesh (ISIS) ya kufufua utumwa na kudai kwamba huko ni kuhuisha suna ya Uislamu, katika hali ambayo Uislamu unakupiga vita, ni suala la kustaajabisha mno na ambalo halina mafungamano yoyote na dini hii ya mbinguni. Hii ni kusema kuwa, Uislamu ni dini inayolingania uhuru na kumfanya mtu mwingine kuwa mtumwa ni kwenda kinyume na matakwa ya Mwenyezi Mungu na dini ya Uislamu. Aidha dini ya Uislamu ni dini ambayo inautambua ubora wa mtu mwingine kwa uchaji-Mungu na kuwa mtumwa kwake yeye Allah, si kwa mwanadamu mwengine. Kwa msingi huo, Mwenyezi Mungu hakubali kumuona mtu akimfanya mwingine kuwa mtumwa wake. Ni kwa ajili hiyo ndipo moja ya madhambi makubwa yasiyosamehewa katika dini ya Uislamu, ni kumnyima mtu mwingine uhuru wake wa kibinaadamu na kuufanya uhuru huo kuwa anasa ya mtu mwingine. Kuhusiana na hilo Mtume (saw) anasema: "Watu wabaya miongoni mwa watu, ni wale ambao wanawanunua na kuwauza watu wengine." Aidha Mtume Muhammad anasema: "Mwenyezi Mungu anasamehe madhambi yote isipokuwa matatu, mtu ambaye anakanusha mahari ya mke wake (yaani anadhulumu mahari ya mke wake) au mtu ambaye anapora haki ya mtumishi wake au mtu ambaye anamuuza mtu ambaye yuko huru." Mwisho wa kunukuu. Kwa mujibu wa riwaya hiyo, kudhulumu mahari ya mwanamke, kumdhulumu mfanyakazi ujira wake na kumfanya mtumwa mtu mwingine, ni miongoni mwa madhambi makubwa ambayo hayana msamaha wowote katika Uislamu.

*************************************

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni Makala yanayokosoa kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na Suna za Mtume Muhammad (saw) makundi ya ukufurishaji hii ikiwa ni sehemu ya 25 ya mfululizo huo. Ndugu wasikilizaji, mwanzoni mwa kudhihiri dini ya Uislamu suala la utumwa lilikuwa limeshika kasi sana, huku likiathiri pia sekta tofauti za wakati huo zikiwemo za utamaduni, uchumi, mahusiano ya kijamii na masuala mengine yanayohusiana na maisha ya mwanadamu. Kwa msingi huo, kupambana na suala hilo lilikuwa suala gumu sana na ambalo lilihitajia muda mrefu sana kulifanikisha. Ni kwa ajili hiyo ndio maana dini ya Uislamu ikatumia mbinu ya kupambana na janga hilo taratibu na kwa muda mrefu. Katika fremu hiyo, kubadili mfumo wa kijamii na kiuchumi, ilionekana kuwa njia yenye taathira chanya kwa ajili ya kukabiliana na wimbi la janga hilo katika jamii ya mwanadamu. Ama hatua ya pili baada ya kuliondoa janga hilo, ilikuwa ni kutangaza marufuku yake sambamba na kuzuia kukaririwa kwake katika jamii. Hivyo ndivyo historia inavyotueleleza kuhusiana na sualo hilo. Ni kupitia ukweli huo, ndio maana historia inathibitisha kwamba, siasa na stratijia za dini ya Uislamu zilijikita katika vita vya kukabiliana na wimbi la utumwa. Kufuatia hali hiyo, hatimaye, utumwa ukafutwa haraka katika jamii kuliko hata mila na desturi nyingine chafu zilizokuwepo kipindi hicho. Kwa kuweka sheria na miongozo mbalimbali, Mtume wa Uislamu alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kusambaratisha wimbi hilo. Mpango wa Mtume ulikuwa ni kuandaa mazingira ya kuachiliwa huru watumwa wote waliokuwa chini ya minyororo ya watu wengine ili waweze kuishi maisha ya kawaida katika jamii. Katika uwanja huo Mtukufu Mtume (saw) akaasisi baadhi ya stratijia za ushawishi kwa ajili ya kuwaachilia huru watumwa wengi kila siku. Katika hilo Nabii wa Allah akawa anawachochea Waislamu kwenda kuwanunua watumwa kwa mabwana zao na kisha kuwaachilia huru. Hakuna shaka kwamba moja ya malengo ya kitendo hicho ilikuwa ni kukata taratibu mzizi wa utumwa katika jamii, kwa kuwaachilia huru watumwa wengi sanjari na kuunda misingi mipya ya kijamii na kiuchumi ambayo ingekuwa mbali na minyororo ya janga hilo. Na hata katika moja ya vita Mtume (saw) alitangaza kwa kusema: "Kila mateka ambaye atawafundisha kusoma na kuandika Waislamu 10, basi atakuwa huru," suala ambalo lilipelekea kuachiliwa huru idadi kubwa ya mateka na watumwa. Aidha mbali na hapo dini ya Uislamu iliweka fidia ya baadhi ya madhambi kukiwemo kuua kwa kukusudia, kuwa ni kumuachilia huru mtumwa. Hii ni katika hali ambayo kumwachilia huru mtumwa katika njia ya Mwenyezi Mungu, kumetajwa kuwa moja ya ibada muhimu sana na kitendo chenye fadhila nyingi katika Uislamu. Katika hilo, Waislamu wa mwanzo walikuwa wakishinadana ambapo hata imepokelewa kuwa, Amiril-Muuminina, Ali Bin Abi Twalib (as) aliweza kuwaachilia huru watumwa 1000 kutoka katika minyororo ya mabwana zao. Hatua hizo zilifanikisha kwa kipindi kifupi sana kuachiliwa huru idadi kubwa ya watumwa katika jamii. Kwa mtazamo wa Uislamu harakati hiyo, ilikuwa ni mwanzo na utangulizi kwa ajili ya kufuta kabisa wimbi la utumwa katika jamii ya Kiislamu.

*********************************************

Itafahamika kuwa kabla ya kudhihiri dini ya Uislamu kulikuwepo na njia nyingi za kuwafanya watu kuwa watumwa, ambazo hata hivyo dini ya Uislamu ilizipiga marufuku. Kwa mtazamo wa Uislamu, kuwafanya watumwa makafiri ambao wanaishi kwa amani na Waislamu, ni suala ambalo limekatazwa na kukekemwa pia. Katika aya ya 8 ya Surat Mumtahina Mwenyezi Mungu anasema: "Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu." Mwisho wa aya. Kwa utaratibu huo, Qur'ani Tukufu imesisitiza kuishi vyema na wafuasi wa dini nyingine kama ambavyo inawataka Waislamu na wasio Waislamu kuwa na tabia nzuri na kuheshimiana. Kwa ajili hiyo, vitendo vya wanachama wa makundi ya kigaidi kama vile Daesh, Jab'hatu Nusra na Boko Haram  vya kuwashambulia watu kama vile watu wa kabila la Yazidi huko nchini Iraq, au kitendo cha wanachama wa Boko Haram cha kuwateka nyara wanafunzi wa kike huko nchini Nigeria na kisha kuwafanya kuwa watumwa wa ngono, ni kinyume kabisa na mafundisho ya dini ya Uislamu na kinachotakiwa kulaaniwa na kila mpenda haki duniani. Kwa mujibu wa aya tuliyosoma, Qur'ani Tukufu inawakataza Waislamu kupigana vita au kuwabagua watu ambao hawawapigi vita wao, kama ambavyo pia hairuhusiwi kuwaua. Hii ni katika hali ambayo wale waliotekwa nyara na wanachama wa kundi la Daesh na Boko Haram huko Iraq na Nigeria, ni wanawake na wasichana ambao ima walikutwa majumbani kwao au shuleni wakijishughulisha na kazi zao za kila siku. Ghafla walivamiwa na kujikuta wakiwa mikononi mwa wanachama wa magenge hayo ya Kiwahabi na kuondoshwa majumbani kwao huku wakitumikishwa katika utumwa wa ngono na wengine wengi kati yao kuuawa kwa dhulma. Kwa hakika kitendo hicho kinalaaniwa vikali na dini tukufu ya Uislamu.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 25 ya makala haya inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

 

Tags