Mar 09, 2017 14:07 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 26 ya makala yanayokosoa kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na suna za Bwana Mtume (sawa) mienendo ya makundi ya ukufurishaji yanayotenda jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu wengine.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia kitendo cha kufanywa watumwa wanawake wa Kiislamu na wasiokuwa wa Kiislamu kunakofanywa na makundi ya kigaidi na ukufurishaji katika maeneo yanayodhibitiwa na magaidi hao. Tukasema kuwa, mbali na vitendo hivyo kukiuka misingi ya ubinaadamu, kunakinzana kabisa na mafundisho ya Qur'ani na suna za Bwana Mtume (saw). 

Hata kama mwanzoni mwa kudhihiri dini ya Uislamu kulikuwepo vitendo vya utumwa baina ya Warabu na wasio Waarabu, lakini Mtume Muhammad (saw) aliweka sera na miongozo ya kuachiliwa huru watumwa wote sambamba na kuhitimisha kabisa mfumo huo wa utumwa katika jamii ya mwanadamu. Mikakati ya Uislamu ilikuwa ni kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi mbali na uepo wa mfumo wa utumwa. Ama hatua ya pili baada ya kuupiga vita utumwa kijamii na kiuchumi ilikuwa ni kuupiga marufuku ili usirejee tena. Hivyo ndivyo historia inavyotueleza kuhusu suala hilo. Aidha historia ya dini ya Uislamu inathibitisha kutekeleza siasa endelevu na mikakati ya kupambana na utumwa.

Sehemu ya jinai mbaya sana zilizofanywa na wanachama wa genge hilo la Kizayuni

Ni kwa ajili hiyo ndio maana tatizo hilo likatoweka haraka katika jamii ya Kiislamu kuliko ada nyingine mbaya. Kwa msingi huo, madai ya wanachama wa makundi ya kigaidi na ukufurishaji ya kuhuisha utumwa na kudai kwamba, huko ni kufufua suna ya Uislamu iliyosahaulika, ni kukinzana kikamilifu na Qur'ani Tukufu na suna za Mtume Muhammad (saw). Kuhusiana na suala hilo tunakuleteeni kisa kimoja cha kihistoria. "Imepokewa kuwa, jeshi la Sham kwa kutumia mfumo wa kushambulia kwa kuvamia, lilidhibiti moja ya maeneo yaliyokuwa chini ya utawala wa Imamu Ali Bin Abi Twalib (as). Askari mmoja wa jeshi lile alimshika mwanamke wa Kiyahudi aliyekuwa akiishi chini ya utawala wa mtukufu huyo na kumnyang'anya kwa nguvu hereni, mikufu na bangili mwilini mwake. Baada ya Amirul-Muuminina Ali (as) kusikia tukio hilo, alikasirishwa sana na kitendo hicho na kusema: "Ikiwa Mwislamu atafariki dunia kutokana na uchungu wa moyoni kwa kashfa hii, basi hafai kushutumiwa bali kwa matazamo wangu kifo chake kinafaa." Mwisho wa kunukuu. Kisa hicho pamoja na mambo mengine kinaashiria hali ya juu iliyonayo dini ya Kiislamu katika kuthamini utu na ubinaadamu kutoka kwa waasisi wa dini hii. Kiasi kwamba mtu asiye Mwislamu kwa sababu tu ya kuishi kwa Waislamu basi anatakiwa kuheshimiwa na kulindwa haki zake. Baada ya hayo ni vipi makundi ya ukufurishaji na kigaidi yanatekeleza ukatili na kuwadhalilisha Waislamu wengine wenye kutamka shahada mbili sambamba na kuwafanya watumwa wanawake wao?

****************************

Ndugu wasikilizaji makundi ya Kiwahabi na ukufurishaji yamepata umaarufu kwa kuwafanyia kila aina ya madhila wanawake na wasichana wa Kiislamu. Katika hilo magaidi hao huwa wanawatumia wanawake katika utekelezaji wa mashambulizi ya kigaidi kwa kuwavisha mikanda ya miripuko na kisha kuwalazimisha kujiripua katikati ya watu.

Sehemu nyingine ya jinai ndogo za magaidi hao wa Kiwahabi

Mbali na hayo ili wanawake waweze kuishi katika eneo walipo Mawahabi hao, hukabiliwa na mienendo iliyo kinyume na ubinaadamu yakiwemo mashinikizo na kutekelezwa sheria kali na nzito dhidi yao. Katika maeneo yanayotawaliwa na magaidi hao wa Kiwahabi siku zote wanawake hunyimwa haki muhimu za kijamii na kibinaadamu sambamba na kukumbwa na aina tofauti za ukatili wa kijinsia kama vile kuolewa kwa nguvu,  kukabiliwa na jihadun-Nikaah, utumwa wa ngono na mfano wa hayo. Hii ni kwa kuwa makundi hayo humtazama mwanamke kwa mtazamo waliokuwa nao Waarabu wa enzi za ujahili kabla ya kubaathiwa Mtume Muhammad (saw). Aidha mitazamo na fatwa za mamufti wa Kiwahabi kuwahusu wanawake, zinabainisha ni kwa kiasi gani wafuasi wa genge hilo la Uwahabi walivyo na fikra sawa na zile za enzi za ujahili. Katika fatwa zao tofauti wanapomzungumzia mwanawake mamufti hao husema: 'Uepo wote wa mwanamke ni shari,' 'mwanamke ni shetani,' 'mwanamke ni mtego wa shetani,' 'mwanamke ni mbwa mweusi na punda ambao ikiwa watapita mbele ya mtu mwenye kusali basi sala yake inabatilika', 'wanawake ni wasio na nguo, msiwape nguo ili kwa njia hiyo waendelee kusalia majumbani,' 'hakuna kitu chenye madhara na hatari kwa mwanamume kuliko wanawake,' 'watoto wachanga wana akili kuwaliko wanawake', 'wakati mwanamke alipoumbwa shetani alishangilia', 'wanawake ni haramu kuendesha vipandwa na wanawake wanaoendesha wanatakiwa kuuawa', 'mwanamume anaweza kumtaliki mke wake kwa kutumia ujumbe tu,' 'haifai wanawake kutumia intaneti isipokuwa kama watakuwa na mtu maharimu karibu yake', 'kulala mwanamke karibu na ukuta ni haramu kwa kuwa ukuta una jina la jinsia ya kiume (jidaaru)', 'mtoto wa kike ni haramu kukaa na baba yake sehemu ya faragha' na mfano wa mambo hayo ya kuudhi na kukera. Na hivyo ndivyo mamufti wa Kiwahabi wenye mtazamo finyu wanavyowachochea magaidi na wakufurishaji katika kutekeleza jinai nchini Syria na Iraq sambamba na kuhalalisha kile wanachokiita kuwa eti ni ndoa ya jihadi 'Jihadun-Nikaah.' Kwa mfano tu Nasir al-'Umar, mmoja wa mamufti wa Kiwahabi alitoa fatwa kadhaa katika kuwahalalishia magaidi wanaofanya jinai nchini Iraq na Syria kwamba endapo watakosa mwanamke aliye halali kumuoa, basi wanaruhusiwa kuwaoa hata maharimu wao.

*********************************************

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako kipindi kilicho hewani ni makala yanayokosoa mienendo ya makundi yanayowakufurisha Waislamu wengine na kutenda jinai za kutisha dhidi yao, hii ikiwa ni sehemu ya 26 ya makala hayo.

Jihaadun-Nikaah ni istilahi iliyoibuliwa na makundi ya kigaidi na ukufurishaji baada ya kujiri machafuko nchini Syria. Katika kuwavutia wasichana na wanawake wa Kiislamu kwa ajili ya kukidhi haja za kimwili za magaidi hao, mamufti wa Kiwahabi walitoa fatwa za kuhalalisha uchafu huo ambao uko kinyume kabisa na mafundisho ya dini ya Kiislamu. Katika hilo wanawake wengi kutoka nchi tofauti walijikuta wakielekea Syria kwa ajili ya kushiriki ngono na wanachama wa magenge hayo ya Kiwahabi (Answar Suna). Aidha mwanamke yeyote aliyekataa kushiriki ufuska huo, alikabiliwa na adhabu ya kifo. Kutokana na hali hiyo mamia ya wanawake wa Kiislamu na wasio kuwa Waislamu waliuawa kikatili kutokana na wao kukataa kushiriki uchafu huo. Ndugu wasikilizaji mnafaa kufahamu kwamba, kinyume na mitazamo hasi na isiyo sahihi na kimantiki ya Mawahabi kumuhusu mwanamke, dini ya Kiislamu inamtazama mwanamke kwa mtazamo kamilifu ulio chanya. Hii ni kwa kuwa  kudhihiri nuru ya Uislamu, ulikuwa mwanzo wa kufutiliwa mbali tamaduni na tabia chafu za kijahilia. Aidha katika kipindi ambacho watoto wa kike walikuwa wakizikwa wakiwa hai huku wanawake wakionekana kama viumbe wasio na thamani na wa kudharauliwa, dini ya Uislamu ilimtambulisha mwanamke kama kiumbe wa thamani na hakika ya mwanadamu mwenye haki sawa na mwanamume. Kwa hakika nukta hizo zilihitimisha mitazamo hasi ya ujahili iliyokuwepo enzi hizo. Kuhusiana na suala hilo Mwenyezi Mungu Mtukufu anaashiria nafasi ya mwanamke na mwanamume katika aya ya kwanza ya Suratn-Nisaa kwa kusema: "Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni. " Mwisho wa aya.

******************************************************

Aya hiyo pamoja na mambo mengine inaashiria mambo kadhaa lakini kuu zaidi ni kwamba, Mwenyezi Mungu Muumba wa dunia amemuumba mwanamume na mwanamke kutokana na asili moja na kwa ajili hiyo hakuna aliye mbora kumliko mwingine. Ndugu wasikilizaji mtafahamu kwamba Mtume Muhammad (saw) alikabiliana vikali na fikra potofu za ujahili kuhusu wanawake. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Nabii huyo wa Allah akaitukuza sana nafasi ya binti yake Bibi Fawimat Zahraa (as). Katika fremu hiyo Bibi Fatwima (as) alikuwa akisema kuwa, sababu ya baba yake huyo ambaye ni Nabii wa Allah kumpa hadhi hiyo ilikuwa na maana ya kufutilia mbali tabia na ada chafu za kijahilia. Hakuna shaka kwamba, Bibi Fatwima alikuwa kiigizo chema kwa wanawake wote duniani huku akiwa ni daraja ya juu kabisa ya ukamilifu wa mwanamke na ya kupigiwa mfano. Kuhusiana na hilo Bukhari katika kitabu chake cha Sahihi Bukhari ananukuu hadithi ya Mtume (saw) akisema: "Fatwimat anatokana na kipande cha nyama yangu, yeyote anayemuudhi yeye basi bila shaka ameniudhi mimi." Mwisho wa kunukuu. Ndugu wasikilizaji ni vyema mfahamu kwamba katika historia yote dini ya Uislamu, imekuwa ikiheshimu nafasi ya mwanamke. Amirul-Muuminina Ali Bin Abi Twalib (as) ameisifu nafasi ya mwanamke huku akimfananisha na ua zuri la kuvutia kwa kusema: "Hakika mwanamke ni ua lenye harufu nzuri na wala sio mwanamapambano." Mwisho wa kunukuu. Katika riwaya hiyo Imamu Ali (as) anamtaja mwanamke kuwa kiumbe muhimu mwenye kufaa kupewa hadhi na heshima kinyume kabisa na fikra potofu za makundi ya Kiwahabi ya ukufurishaji na kigaidi. Kwa ajili hiyo ni suala la kawaida kwamba lazima kuamiliana na kiumbe huyo (mwanamke) kwa upole na huruma. Kama ambavyo haifai kuamiliana naye kwa ukatili na uzito nje ya uwezo wake. Katika jamii ambayo mtu aliyekuwa na mtoto wa kike alionekana mwenye fedheha na aibu kubwa, huku watoto wa kike wakizikwa wakiwa hai, Mtume wa Uislamu alikabiliana na hali hiyo kwa kusema: "Watoto wenu bora ni wa kike." Mwisho wa kunukuu. Kadhalika mtume wa Uislamu aliwataka watu kuamiliana kwa namna iliyo bora na wanawake kwa kusema: "Himizaneni kuwafanyia vizuri wanawake, ndio kheri." Aidha akizungumzia kitendo cha kuwadhalilisha wanawake Mtume wa Allah anasema: "Watu waungwana ni wale ambao wanawaheshimu wanawake, na watu duni ni wale wenye kuwadhalilisha." Mwisho wa kunukuu.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 26 ya makala haya inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

 

Tags