Hadithi ya Uongofu (66)
Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji wa kuwa nami katika kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu kinachokujieni kutoka hapa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kipindi chetu kilichotangulia kilizungumzia athari na matokeo ya subira na tulisema kwamba, subira ni nguzo muhimu ya imani na humpeleka mtu upande wa kuelekea peponi. Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 66 kitazungumzia aina ya subira. Tafadhalini kuwa nami hadi mwisho wa kipindi wa hiki.
Bwana Mtume Muhammad SAW amenukuliwa akiigawa subira katika sehemu tatu. Mtukufu huyo amesema:”Subira zimegawanyika katika sehemu tatu: Mosi, subira ya kuvumilia msiba na masaibu. Mtu anayeonesha subira anapofikwa na msiba na masaibu na akazivuka tabu za masaibu hayo kwa subira yake njema, Mwenyezi Mungu atamuandikia daraja mia tatu ambapo masafa kati ya daraja moja na nyingine ni umbali wa mbingu na ardhi.
Pili, subira ya kushikamana na ta’a na subira ya kujizuia na madhambi. Mtu anayekuwa na subira na akawa mwenye juhudi katika ta’a na kumwabudu Mwenyezi Mungu, Allah humuinua daraja yake kwa kiwango mithili ya masafa ya baina ya kina cha chini kabisa cha ardhi hadi kwenye Arshi. Tatu ni subira ya kujizuia na kufanya madhambi Mwenyezi Mungu humuinua daraja yake kwa kiwango mithili ya masafa ya baina ya kina cha chini kabisa cha ardhi hadi inapoishia Arshi”. Kwa maneno haya matukufu ya Bwana Mtume inatubainikia kuwa subira ya kujizuia na madhambi, kujiepusha na maasi na kutofanya aliyoyakataza Mola ndiyo daraja ya juu zaidi ya subira.
Kwa hakika subira katika kushikamana na taa ni mithili ya kusimama kidete mbele ya mambo magumu na matatizo na hivyo kutii amri za Mwenyezi Mungu. Kutii amri za Mwenyezi Mungu katika Sala, Hija, kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kutekeleza mambo ya wajibu ya kutoa fedha kama vile Khumsi na Zaka.
Makusudio juu ya kufanya subira katika kujizuia kufanya dhambi na maasi, ni kusimama kidete mbele ya vishawishi vya matamanio ya nafsi ambapo kama hakutakuwa na subira kama hiyo, mawimbi na tufani ya matamanio na hawaa ya nafsi huja na kubeba imani na taqwa yote pamoja na utakasifu na mapenzi.
Kufanya subira juu ya kutofanya maasi nako ni kustahamili na kusimama kidete mtu mbele ya matukio machungu kama vile kuwapoteza wapendwa, kupata hasara kubwa ya kifedha, kuwa hatarini heshima na hadhi yake kijamii na kukumbwa na maradhi mabaya na yasiyo na tiba. Imam Ali bin Abi Talib as anabainisha aina za subira kwa kusema: Subira ina matawi manne ambayo ni shauku, woga, kuipa mgongo dunia na kusubiria. Kisha anabainisha hayo kwa kusema, mtu mwenye hamu na shauku ya pepo hukaa kando na kuachana na matamanio ya nafsi yenye kukengeusha, na mtu anayeogopa moto wa Jahanamu hukaa mbali na mambo yaliyoharamishwa na aidha mtu mwenye kuwa na zuhdi na kuipa mgongo dunia, huwa na kasi katika kutekeleza au kufanya jambo la kheri.
Moyo wa mwanadamu ni kituo cha huba na hisia. Kila mara mtu anapompoteza mtu ambaye ni kipenzi chake, huingiwa na huzuni na kuwa na ghamu na kutokwa na machozi.
Katika hali ya kawaida, moyo wa mwanadamu huonyesha radiamali mkabala na matukio mabaya na macho ya mwanadamu ambayo ni dirisha la moyo, huathirika na taathira iliyopata moyo na hivyo hulia. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana kulia na kuomboleza kwa ajili ya kupoteza azizi na mtu muhimu na kipenzi ni jambo la kawaida na kiutu. Lakini kila ambacho ni muhimu ni kwamba, mwanadamu akipatwa na msiba au akiomboleza hapaswa kutamka maneno ambayo yanaonyesha kutoshukuru au kushtakia. Kwa hakika mja hapaswi kutamka maneno ambayo hayaendani na hadhi yake kama mja mtiifu kwa Mola Muumba. Kuhusiana na jambo hilo, Bwana Mtume saw amenukuliwa akisema:
"Sio katika sisi yule ambaye anapopatwa na msiba huudhuru uso wake na kuchanachana nguo zake au kutoa maneno kama ya watu wa zama za ujahilia."
Inasimuliwa kuwa, wakati Mtume saw alipofiwa na mwanawe Ibrahim, alilia kwa namna ambayo machozi yalitiririka na kulowesha kifua chake. Baadhi ya watu ambao hawakuwa na utu walimwambia, Ewe Mtume wa Allah! Wewe umetukataza kulia lakini mbona mwenyewe unalia? Mtume saw akawajibu kwa kuwaambi, hiki sio kilio bali ni kuonyesha huba, huruma na mapenzi, na mtu ambaye hana huba, huruma na mapenzi basi, hatajumuishwa katika rehma za Mwenyezi Mungu.
Kwa hakika maisha ya hapa duniani daima huambatana na misiba na matatizo. Uwezo na nguvu za mwanadamu pia huonekana katika misiba na matatizo anayokabiliwa nayo. Endapo mtu atadiriki uwepo wa Mwenyezi Mungu pamoja na nguvu za Mola Muumba kwa ulimwengu huu, na wakati huo huo akatambua falsafa na hekima ya maisha ya hapa duniani basi atafahamu na kuelewa vyema kwamba, dunia ina mambo ya lazima ambapo misiba, huzuni, machungu na masaibu ni mambo ambayo hayatenganishiki na dunia pamoja na maisha ya hapa duniani. Kustahamili na kuvumilia machungu pamoja na matatizo na mashinikizo mbalimbali maishani, humfanya mwanadamu asonge mbele kuelekea katika njia ya ukamilifu na saada ya milele.
Kwa msingi huo, pindi Muumini anapokabiliwa na tatizo lolote au mushkili hulihesabu jambo hilo kuwa, ni mtihani kutoka kwa Mwenyezi Mungu na bila shaka, kuna hekima juu ya hilo na hulibadilisha gumu hilo na kuwa njia ya kuelekea katika ukamilifu. Ni kwa namna hiyo ndio maana misiba yote, kwake yeye huwa myepesi na yenye kuvumilika. Kuvumilia mtu misiba na matatizo hunyanyua daraja ya subira ya mtu na kumfikisha katika kuridhia. Imam Ja'far Sadiq as amewagawanya wanaosubiri katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni watu wenye kusubiri juu ya mabalaa na masaibu ambapo wanapokumbwa na hayo huchukia na kuudhika, lakini pamoja na hayo husubiri na kuvumilia na wala si wenye kulalamika na kushtakia kwa watu. Imam Sadiq as anasema kuwa, hilo ni kundi la watu wa kawaida katika jamii na ujira wa subira yao ni bishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Amma kundi la pili ni la watu ambao sio tu kwamba, hawachukii na kukasirishwa na balaa iliyowashukia na kuathiriwa nayo, bali huupokea mtihani huo kwa mikono miwili na hutambua kuwa, hayo ni miongoni mwa mapenzi na huba ya Mwenyezi Mungu kwao. Imam Sadiq as analitaja kundi hilo kuwa ni la watu maalumu na kwamba, ujira wao ni kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu.