Apr 03, 2017 07:53 UTC
  • Jumatatu 3 Aprili, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe 5 Rajab 1438 Hijria sawa na 3 Aprili 2017.

Tarehe 5 Rajab miaka 1194 iliyopita aliuawa shahidi Abu Yusuf Yaqub ibn Is'haq, maarufu kwa jina la Ibn Sikkit, msomi wa Kiislamu na mtaalamu mkubwa wa lugha ya Kiarabu. Alizaliwa katika mji wa Khuzestan unaopatikana kusini magharibi mwa Iran. Ibn Sikkit alielekea mjini Baghdad na familia yake na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo. Umaarufu wa Ibn Sikkit katika elimu ulimfanya Mutawakkil, mmoja kati ya watawala wa Abbasia kumwalika kwa lengo la kuwafundisha watoto wake. Ibn Sikkit alikuwa na mapenzi makubwa kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (SAW); jambo hilo lilimkasirisha sana Mutawakkil na alichukua hatua ya kumuua. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyu ni kile kiitwacho "Islahul Mantik."

ابن سکّیت

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, mji wa Baghdad ulikombolewa na Rashid A'li Gilani kiongozi wa mrengo uliokuwa ukiwapinga Waingereza, baada ya mapigano yaliyotokea kati ya wazalendo waliokuwa na uchungu wa nchi yao dhidi ya serikali ya London. Gilani alikuwa akiungwa mkono na Ujerumani na kutokana na kutopata misaada kwa wakati mwafaka, vikosi vya majeshi ya Uingereza vilifanikiwa kuwakandamiza wafuasi wake. Baada ya tukio hilo serikali ya Iraq ilijiunga na nchi waitifaki katika Vita vya Pili vya Dunia.

Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, yaani sawa na tarehe 3 Aprili 2002, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulizi makubwa katika mji wa Jenin ulioko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, katika ardhi za Palestina. Mashambulio hayo yalikuwa mwendelezo wa mashambulizi ya wiki kadhaa ya Wazayuni kwenye eneo hilo, kwa shabaha ya kuzima Intifadha ya wananchi wa Palestina. Kwenye mashambulio hayo ya majeshi ya Wazayuni huko Jenin, asilimia 70 ya mji huo ilibomolewa kabisa, mamia ya Wapalestina kuuawa shahidi na watu wengine wasiopungua 5,000 kukosa makazi.