Apr 04, 2017 08:27 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (69)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na ni wakati wa kujiunga name tena katika sehemu nyinginr ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Katika kipindi kilichopita  tulijadili na kuzungumzia suala la kuwa na mtazamo wa mbali na tulisema kwamba, moja ya siri kubwa za mafanikio ya mtu anayemuamini Mwenyezi Mungu ni kuwa na muono na mtazamo wa mbali. Katika kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 69 ya mfulizo huu, tutazungumzia engo nyingine ya kuwa na muono wa mbali. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

*******

Kwa hakika kuwa na muono wa mbali hakupatikana isipokuwa kwa mtu kuwa na fikra na busara. Mtu ambaye ana muono wa mbali, kabla ya kufanya jambo au kazi yoyote ile awali hupima engo zote za kazi na jambo lile. Imam Ali bin Abi Twalib as anaelezea fasili na maana ya mtazamo wa mbali katika Nahaj al-Balagha kwa kusema: Muono wa mbali ni kufikiria.

Kwa hakika mtu mwenye muono wa mbali huwa hafanyi jambo hivi hivi pasina ya kufikiri na kutafakari hasa natija ya amali anayotaka kuifanya. Mtu huyu huchunguza engo zote na jambo lolote tarajiwa na kisha hutathmini natija jumla ya jambo hilo. Imam Ja'far Swadiq as anautaja muamala wa mtu huyo wa kuamiliana na jambo hilo kwa namna hii kwamba, ni natija ya dhana na shaka ya mtu. Anasema: Mtazamo wa mbali ni taa ya dhana na shaka.

Kwa maana kwamba, mtu ambaye ana mtazamo wa mbali si mwenye kuwa na dhana nzuri ya mia kwa mia kuhusiana na jambo fulani. Bali hupima na kutia katika mzani mambo yote tarajiwa yanayoweza kujitokeza; na kashi baada ya hapo huingia uwanjani kuifanya kazi husika akiwa na tahadhari kamili.

Kiuhakika ni kuwa, mtu mwenye muono na mtazamo wa mbali wa mambo ni mtu wa tahadhari. Hivyo basi mtu huyo haiingii uwanjani kwa ajili ya kufanya jambo fulani pasina kuchunguza na kutathmini engo zote jumla za jambo lenyewe na matokeo yake. Mtu mwenye mtazamo wa mbali ni mara chache kumuona akijiingiza katika jambo la pata potea yaani la bahati nasibu. Hamuamini kila mtu au si mwenye kuamini kila kitu, bali imani yake juu ya jambo fulani msingi na chimbuko lake ni hoja na dalili thabiti ambazo zimemfikisha katika hatua ya yakini. Ni kwa msingi huo, ndio maana Imam Ali as anasema kuwa, kuwa na imani si ya mahala pake ni kinyume na mtazamo na muono wa mbali. Anasema: Kuwa na imani kabla ya mtihani ni kinyume na muono wa mbali.

 

Katika mafundisho ya Kiislamu na aya za Qur'ani Tukufu, upande wa kuwa na tahadhari katika muono wa mbali ni jambo ambalo limetiliwa mkazo mno. Katika aya ya 6 ya Surat al-Hujurat Mwenyezi Mungu anawataka waumini kufanya uchunguzi kwanza wa habari yoyote wanayoletewa. Aya hiyo inasema:

Enyi mlio amini! Akikujieni mpotovu na khabari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kuto jua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyo yatenda.

Aya hii inaonyesha kwamba, kabla mtu hajachukua uamuzi kuhusiana na khabari aliyoletwa kwanza anapaswa kufanya uchunguzi na kupata yakini kuhusiana na usahihi au kutokuwa sahihi habari husika.

Kwa hakika kuwa na mtazamo wa mbali kwa namna fulani ni aina ya umakini na utumiaji wa hali ya juu wa akili sambamba na tahadhari. Mtu mwenye muono wa mbali, daima ni mwenye kuwa na umakini katika kuchagua na uchukuaji maamuzi na siku zote ni mwenye kujaalia hatari zinazoweza kujitokeza kuhusiana na jambo analotaka kulifanya au uamuzi anaotaka kuuchukua. Kwa hakika suala la kuwa na mtazamo na muono wa mbali ni nukta muhimu sana.

Nukta nyingine muhimu ya kuzingatia ni hii kwamba, katika kuchukua tahadhari katika mambo, haifai kuchupa mipaka. Kama ambavyo pia katika ushujaa haipaswi kuchupa mipaka pia kwani yote mawili yana madhara ndani yake. Kama ambavyo ushujaa wa kuchupa mipaka unakemewa kutokana na hatari zinazoweka kujitokeza vivyo hivyo kuwa na tahadhari kupita kiasi huhesabiwa kuwa ni uoga jambo ambalo nalo linakemewa. Kwa msingi huo kuwa na mtazamo wa mbali kunapaswa kujengeka juu ya msingi wa uwiano na ufanyaji mambo wa kati na kati. Imam Hassan al-Askary as anasema kuwa: Katika muono wa mbali kuna kipimo ambacho hakipaswi kuzidi, kwani kuchupa na kukivuka kipimo hicho ni uoga na hofu.

 

Kuwa na muono wa mbali ni jambo lenye athari na baraka katika maisha ya mwanadamu. Jambo hilo hupelekea kuweko hali ya kusimama kidete, kuwa na subira, kuwa na azma na irada katika mambo, msimamo thabiti na kutegemea mantiki na akili. Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) anauarifisha mtazamo na muono wa mbali kwamba, ni rasilimali ya mwanadamu.

Kwa msingi huo kama mtu hatakuwa na muono na mtazamo wa mbali katika mambo, basi anapaswa kukubali kwamba, ataandamwa na balaa na matatizo mengi na hivyo kuwekwa mbali na malengo na matokeo yake ni kushindwa kufikia katika natija na matokeo mazuri ya mambo mbalimbali. Miongoni mwa athari na baraka hizo ambayo tunaweza kuiashiria hapa ni suala la kuwa na azma imara na thabiti katika kufanya mambo.

Mtu ambaye anapima na kuchunguza engo zote za kazi au jambo analotaka kufanya na akawa na mtazamo wa mbali kisha akatathmini matokeo ya mbali na ya karibu bila shaka ataanza kuifanya kazi hiyo akiwa na irada na azma imara huku lengo lake likiwa ni kuhakikisha kwamba, anaifanikisha kazi hiyo. Hata hivyo kadiri kiwango cha mtazamo wa mbali cha mhusika kinavyopungua basi vivyo hivyo azma ya mtu nayo huwa dhaifu. Hii ni kutokana na kuwa, mwenye mtazamo huo huwa hana uhakika na hatima ya kazi anayoifanya. Kuizingatia akhera ni kilele cha mtu kuwa na mtazamo wa mbali.  Kwa mtazamo wa Imam Ali bin Abi Twalib (as) ni kuwa, mtu mwenye mtazamo wa mbali ni yule ambaye mambo ya dunia hayamghafilishi na kufanya amali kwa ajili ya akhera. Mtu mwenye mtazamo wa mbali licha ya kuwa, ni mwenye kuwa na tahadhari lakini hutambua thamani ya wakati. Hutambua kwamba, fursa hupita kama unavyopita upepo yaani kama ambavyo upepo unakuja kwa haraka na kupita kwa haraka, fursa pia ndivyo ilivyo. Kwani yamkini fursa ulioipata sasa hivi usiipate tena. Hivyo la msingi ni kutumia vizuri fursa hiyo. Kwa mfano fursa ya ujana ambayo mtu anayo anapaswa kuitumia kwani ikipita si yenye kurejea tena.

Sifa nyingine ya watu wenye mtazamo wa mbali ni kwamba, huwa ni wenye subira na wenye kutaamali na kutafakari. Imam Ali as anasema kuhusiana na sifa hiyo kwamba: Mtu mwenye mtazamo wa mbali zaidi ni yule mwenye subira na hali ya kutafakari na kutaamali juu ya hatima ya kazi anayotaka kuifanya na kulifanya hilo kuwa mtindo na mbinu yake. Aidha anasema kuwa: Mtu mwenye mtazamo wa mbali ni yule ambaye akipata neema na ujazi hushukuru na anapoondolewa neema hiyo, huwa mwenye subira na ustahamalivu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki umefikia tamati kwa leo. Msikose kujiunga nami wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu. Ahsanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.