Hadithi ya Uopngofu (70)
Ni matumaini yangu kuwa, mubukheiri wa afya na ni wasaa na wakati mwingine wa kujiunga nami wapenzi wasikilizaji katika mfululizo wa kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.
Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 70 ya mfululizo huu kitazungumzia uadilifu na insafu. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa name hadi mwisho wa kipindi hiki kutegea sikio kile nilichokuandalieni hii leo. Karibuni.
*****
Insafu au uadilifu ni moja ya sifa njema za kiakhlaqi na kimaadili. Maana ya insafu ni kuchunga uwiano, haki na usawa katika vitendo na wakati wa kuamiliana na wengine katika jamii unayoishi. Imam Ali bin Abi Twalib as anasema katika sehemu moja ya wosia wa Imam Ali bin Abi Twalib as kwa mwanawe Hassan as: Ewe mwanangu! Wapendelee watu kile ambacho unapenda ufanyiwe na kile ambacho kwako wewe si kizuri, basi usipende kiwakute wengine. Usidhulumu kama ambavyo hupendi udhulumiwe na fanya wema kama ambavyo unapenda ufanyiwe wema na hisani. Usiseme usilolijua, hata kama unajua kidogo na usiwaambie watu kitu ambacho wewe hupendi watu wakuseme kwa hilo.
Kwa hakika kuchunga insafu na uadilifu ni jambo gumu, lakini mwanadamu anapaswa kudiriki umuhimu wa hilo na hivyo kufanya mambo kwa insafu na uadilifu. Mmoja wa Maswahaba wa Imam Ja’far Swadiq (as) aliandika barua yenye maswali mbalimbali ambayo alitaka kufahamu majibu yake na akampatia Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Abdul-A’ala ambaye alikuwa akielekea Madina ili ampatie Imam Swadiq as. Aidha swali moja ambalo hakuliandika katika barua ile alimtaka Abdul-A’ala amuulize Imam Swadiq ana kwa ana. Bwana yule alitaka kujua Mwislamu ana haki gani kwa Waislamu wengine.
Abdul A’ala anasimulia kwa kusema: Nilipofika mjini Madina nilikwenda kwa Imam Swadiq as na kumkabidhi barua ile ya maswali na kisha nikamuuliza kuhusu swali la haki ya Mwislamu kwa ndugu yake Mwislamu. Hata hivyo kinyume na matarajio yangu, Imam alijibu maswali yote isipokuwa swali lililohusiana na haki ya Mwislamu kwa ndugu yake Mwislamu.
Wakati nilipotaka kuondoka mjini Madina na nikiwa tayari nimejiandaa kwa safari, nilikwenda Kwa Imam Swadiq as kwa ajili ya kumuaga. Nilipofika nilimwambia, Ewe Imam hujajibu swali nililokuuliza kuhusu haki ya Mwislamu kwa ndugu yake Mwislamu. Imam akasema, nachelea kusema ukweli wa jambo hilo kisha usilifanyie kazi na kisha ukatoka katika dini ya Mwenyezi Mungu. Kisha Imam akasema: Miongoni mwa taklifu ngumu kabisa za Mwenyezi Mungu kuhusiana na waja wake ni mambo matatu:
Mosi, kuchunga insafu na uadilifu baina yake na wengine kiasi kwamba, aamiliane na ndugu yake Mwislamu kama anavyopenda wengine waamiliane nae hivyo hivyo. Pili, asiwe mgumu kwa mali yake kwa ndugu zake Waislamu na aamiliane nao kwa usawa. Na jambo la tatu ni kwamba, amkumbuke Mwenyezi Mungu katika kila hali. Na kusudio la kumtaja na kukumbuka Mwenyezi Mungu sio kutamka mtawalia Subhanallah Walhamdulilahi, la hasha, bali lililokusudiwa ni kwamba, unapokutana na jambo la haramu mkumbuke Mwenyezi Mungu na usilifanye jambo hilo.
Insafu na uadilifu kwa maana ya usawa na uwiano, ni moja ya sifa aali za kimaadili za mwanadamu. Watu ambao ni wa insafu na uadilifu wanashabiana zaidi na Mtume saw. Mtume saw amenukuliwa akisema kwamba: Je nikujulisheni tabia gani miongoni mwa tabia zenu ambayo inashabihiana zaidi na mimi? Akajibiwa, ndio Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mbora huyo wa viumbe akasema: Ni yule ambayo mwenye tabua nzuri zaidi, mwenye subira zaidi na ambaye kwa ndugu zake ni mwenye kutenda wema zaidi na mwenye insafu zaidi.
Aidha amesema; mtu bora kabisa ni yule ambaye ni mnyenyekevu akiwa katika hali ya neema na akiwa katika hali ya kuwa muhitaji huwa mwenye zuhdi na kuipa mgongo dunia, mwenye insafu katika hali ya kuwa na uwezo na akiwa na nguvu ni mwenye kusubiri.
Kadhalika Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa: Miongoni mwa sifa ambazo zinapelekea nikudhaminieni pepo ni kuchunga insafu mnapoamiliana na watu.
Imam Ali as anasema kuwa, Muumini humfanyia insafu hata mtu ambaye yeye haamiliani naye kwa insafu.
Insafu imegawanyika katika sehemu kadhaa. Moja ya sehemu hiyo ni insafu katika mazungumzo. Mtu anapaswa kuwathamini watu wengine anapozungumza nao kama anavyothamini maneno yake na awatetee kama anavyotetea maneno yake. Kwa maneno mengine ni kuwa, awe ni mwenye kufuatilia maneno ya haki na ayakubali hayo kutoka kwa yeyote na popote pale. Hata kama msemaji wa neno hilo la haki atakuwa mtu wa kawaida sana na msikilizaji ni msomi na alimu mkubwa.
Katika maisha yetu tunayoishi kuna watu huwa hawathamini maneno ya haki kutoka kwa wengine kwa sababu tu kwa mtazamo wao msemaji huyo ni duni kuliko wao au hana daraja yao kielimu au kihali hna mali. Hili ni jambo ambalo linakemewa na mafundisho matukufu ya Kiislamu ambayo yanasisitiza kusikiliza na kupokea neno haki kutoka kwa mtu yeyote yule bila kujali tofauti za kimataba au za kielimu.
Imam Ja’far Swadiq as anasema kuwa: Watu wa aina tatu Siku ya Kiyama watakuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu. Mosi, mtu ambaye mwenye nguvu ambaye katika hali ya ghadhabu hawadhulumu walioko chini yake. Pili mtu ambaye wakati anapotoa hukumu baina ya watu wawili hutoa kwa usawa pasina kuegemea upande cwowote. Na tatu ni mtu ambaye anasema haki, bila kujali ni kwa manufaa yake au kwa madhara yake.
Aidha Bwana Mtume saw anasema kuhusiana na suala la kuchunga insafu na uadilifu katika kuipokea haki kwamba: Mcha Mungu zaidi miongoni mwa watu ni yule anayesema haki iwe ni kwa faida au kwa madhara yake. Aidha hadithi ifuatayo inayopatika katika kitabu cha Kanzul Ummal Mtume saw amenukuliwa akisema: Ikubali haki iliyoletwa kwako na mtu yeyote yule, iwe kubwa au ndogo au hata kama ni adui yako; na mrejeshee mwenyewe aliyeileta batili iwe ndogo au kubwa hata kama aliyeileta ni rafiki yako.
Kwa hakika kuchunga insafu na uadilifu kuna marhala ambapo kila mtu anapaswa kulichunga hilo kulingana na nafasi aliyopo. Kutochunga hilo humfanya mwanadamu aharibu dunia na akhera yake.
Katika nasaha zake kwa mmoja wa marafiki zake, Imam Ja’far Swadiq as alisema: Je unataka nikujulishe moja ya wajibu muhimu zaidi za Mwenyezi Mungu? Basi amiliana kwa insafu na watu. Mshirikishe ndugu yako katika dini katika njia ya Mwenyezi Mungu na katika mali yako, na mtaje Mwenyezi Mungu katika kila hali kiasi kwamba, kama utapatiwa jambo la taa basi lifanye na kama utapatiwa jambo la maasi achana nalo.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia tamati. Ninakushukuruni kwa kunitegea sikio na ninakuageni nikukitakieni kila la kheri maishani.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh