Jumatano 05, Aprili, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 7 Rajab 1438 Hijria sawa na 5 Aprili 2017
Siku kama ya leo miaka 1133 iliyopita alizaliwa Ibn Tarrar mpokezi wa hadithi na mwandishi wa fasihi wa Kiislamu huko Iraq. Bin Tarrar ambaye ni jina lake ni Abul Fat'h Muafi bin Zakaria bin Yahya alikuwa miongoni mwa maulama wa Kishafii na alitabahari katika elimu za fiqhi, hadithi na fasihi. Msomi huyo wa Kiislamu aliandika vitabu vingi katika uwanja wa fiqhi. Vilevile aliandika vitabu katika taaluma ya fasihi ya lugha ya Kiarabu kikiwemo kile alichokiita "al Jalisu Wal Aniis".Bin tarrar alifariki dunia mwaka 390 Hijria mjini Baghdad akiwa na umri wa miaka 85.
Siku kama ya leo miaka 432 iliyoyopita yaani 5 Aprili 1585, yalifanyika mauaji ya halaiki katika mji wa Harlem nchini Uholanzi, ambacho kilikuwa kitovu cha wapigania uhuru nchini humo. Mauaji hayo yalifanyika kwa amri ya Mfalme wa Uhispania. Jumla ya watu elfu sita wanaaminika kuwa waliuawa kwenye shambulio hilo. Hatimaye Uholanzi ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Uhispania hapo mwaka 1609.
Tarehe 5 Aprili 223 iliyopita, aliuawa Georges Danton mmoja kati ya viongozi wa mapinduzi ya Ufaransa. Danton licha ya kusomea taaluma ya sheria, alikuwa mhamasishaji mzuri katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa. Danton alikuwa akiamini kuwa, sanjari na kuzuia machafuko na maafa ya kibinadamu, utawala wa kifalme nchini Ufaransa ulipaswa kutokomezwa. Amma Robes Pierre mmoja kati ya vinara wakubwa wa mapinduzi ya Ufaransa ambaye pia alikuwa mshindani wa Danton alichukua uamuzi wa kimtia mbaroni Danton na hatimaye kumuuwa.
Na siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Aprili 1956, yalimalizika mashambulizi ya kinyama ya majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza. Majeshi hayo, tarehe 4 Aprili, yalianza kufanya mashambulio makubwa na kuwauwa watu 56 na kuwajeruhi wengine 30 wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee katika kipindi cha siku mbili. Nchi za Magharibi na jamii ya kimataifa hazikutoa radiamali yoyote kuhusiana na jinai hizo za Wazayuni.