Apr 08, 2017 04:15 UTC
  • Jumamosi  8 Aprili 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 10 Rajab 1438 Hijria sawa na 8 Aprili 2017

Katika siku kama ya leo miaka 1378, iliyopita tarehe 10 Rajab mwaka 60 Hijria Qamaria, alizaliwa Abdullah bin Hassan, maarufu kama Ali Asghar , mtoto mdogo zaidi wa Imam Hussein AS, Mjukuu wa Mtume Muhammad SAW. Wakati wa kuzaliwa kwake, Yazid bin Muawiya ndio mwanzo alikuwa ameingia madarakani na katika kipindi hicho alikuwa akimtisha na kumshinikiza Imam Hussein AS ambai. Lakini Imamu hakufanya hivyo kwani alimtazama Yazid kama mtu fisadi asiyestahiki kubaiwa. Ni kwa sababu hii ndio takribani siku 18 baada ya kuzaliwa  Ali Asghar, Imam Hussein AS aliondoka Madina akiwa na watu wa nyumba yake. Wakati wa vita vya Karbala baina ya majeshi ya Yazid na Imam Hussein AS na wafuasi wake, Ali Asghar alikuwepo pia katika medani ya vita. Pale wafuasi wote watiifu wa Imam Hussein As walipouawa shahidi, mwanae alikuwa na kiu sana kutokana na maadui kukata maji. Hapo Imam Hussein AS aliinua mikono yake juu akiwataka wampe maji lakini Harmaleh-Ibn-Kahel Asadi aliyekuwa kati ya wanajeshi katili  wa Yazid alimlenga Ali Ashgar kwa mkuki na kumdunga koo lake na mtoto huyo mchanga akafa shahidi katika hali hiyo.

Siku kama ya leo miaka 1243 iliyopita sawa na 10 Rajab 195 Hijria, alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina, Imam Muhammad Taqi mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume SAW. Imam Taqi AS alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ridha AS Mtukufu huyo alikuwa maarufu kwa lakabu ya 'Jawad' yenye maana ya mtu mkarimu mno, kutokana na ukarimu wake mkubwa. Nyumba ya Imam Jawad ilikuwa kimbilio la wahitaji waliokuwa wamekata tamaa na walitaraji Imam huyo awakidhie shida na mahitaji yao ya dharura. Sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa uzao huo, tunakunukulieni maneno ya hekima ya Imam Muhammad Taqi AS ambaye amesema: "Kila mwenye kuwa na imani na Mwenyezi Mungu, basi Allah humuokoa na kila baya na kumhifadhi na kila uadui."

Ssiku kama ya leo miaka 47 iliyopita, ndege za kijeshi za utawala haramu wa Israel ziliishambulia shule ya msingi ya Bahrul Baqr iliyoko umbali wa kilomita 80 kaskazini mwa mji wa Cairo. Katika mashambulizi hayo ya kutisha watoto 46 waliokuwa shuleni hapo waliuawa. Mashambulizi hayo ya kikatili yaliibua hasira ya watu katika nchi mbalimbali duniani. Kwa muda wa miezi mitatu ya awali ya mwaka 1970 ndege za utawala haramu wa Israel ziliyashambulia maeneo ya kiraia huko kaskazini mashariki mwa Misri. Tarehe 12 Februari mwaka huohuo Wazayuni pia walikishambulia kiwanda kimoja katika eneo hilo na kuua pamoja na kuwajeruhi wafanyakazi 168. Kadhalika Wazayuni waliwaua watu 12 katika mashambulizi dhidi ya mji wa al-Mansura ulio kaskazini mashariki mwa nchi hiyo tarehe 31 mwezi Machi mwaka huohuo wa 1970.

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita utawala wa Baathi nchini Iraq uliwaua Shahidi Sayyid Muhammad Baqir-Sadr na dada yake, Bintul Huda. Sayyid Sadr alijifunza Qur'ani Tukufu na elimu nyingine za kidini akiwa mdogo na kupata daraja ya ijtihadi akiwa kijana. Alikuwa mmoja wa walimu wakubwa wa chuo cha kidini mjini Najaf, Iraq kiasi kwamba nadharia zake katika elimu ya usul fiqhi zilipewa umuhimu mkubwa na wasomi wengine wa Kiislamu. Msomi huyu aliyekuwa na uelewa na uwezo wa hali ya juu wa kielimu, aliuarifisha Uislamu kwa njia sahihi. Kwa kipindi kifupi Ayatullah Sadr aligeuka na kuwa kiongozi wa kifikra na kisiasa wa wananchi wa Iraq na kuyapa mwelekeo mpya mapambano ya wananchi wa nchi hiyo. Baada ya muda fulani utawala wa nchi hiyo ambao ulihisi hatari kutokana na harakati za Ayatullahi Sadr ulimtia mbaroni na kisha kumuua shahidi mwanazuoni huyo mashuhuri pamoja na dada yake, licha ya malalamiko makubwa ya maulama na wananchi Waislamu wa Iraq. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na kitabu cha "Uchumi Wetu", "Hamasa ya Nuru", "Falsafa Yetu", "Mwanadamu wa Leo na Matatizo ya Kijamii", na "Ukhalifa wa Mwanadamu na Ushuhuda wa Mitume."

Sayyed Baqeri Sadr