Apr 10, 2017 03:37 UTC
  • Jumatatu, 10 Aprili, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe 12 Rajab 1438 Hijria sawa na 10 Aprili 2017.

Siku kama ya leo miaka 1406 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Abbas bin Abdul Muttalib, ami yake Bwana Mtume Muhammad SAW na mmoja wa shakhsia wakubwa wa Kikuraishi. Alijulikana kwa tabia njema, mwenendo mzuri, busara na maarifa ya hali ya juu. Baadhi ya wanahistoria wanaamini kwamba, Abbas bin Abdul Muttalib aliukubali Uislamu kwa siri kabla ya Bwana Mtume kuhamia Madina na alikuwa akimpelekea Mtume habari za harakati za washirikina mjini Makka. Mwaka wa 8 Hijria Abbas bin Abdul Muttalib aliungana na Waislamu na baada ya Fat'hu Makka aliteuliwa na Bwana Mtume kuchukua jukumu la kutoa huduma ya maji kwa watu wanaozuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al-Kaaba.

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, aliuawa Emiliano Zapata mwanamapinduzi mashuhuri wa nchini Mexico kupitia njama maalumu dhidi yake. Wahindi Wekundu wa Mexico wanamfahamu Zapata kama mrekebishaji wa jamii na mwokozi wao. Tangu mwishoni mwa mwaka 1910 Miladia sanjari na kutoa nara za kupigania uhuru, alibeba pia silaha na kuwaongoza Wahindi Wekundu katika kupambana na wavamizi na kufanikiwa kuzikomboa ardhi za nchi hiyo zilizokuwa zimeporwa. 

Emiliano Zapata

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 10 Aprili 1946, kundi la mwisho la wanajeshi wa Ufaransa liliondoka huko Lebanon. Ufaransa ilizikalia kwa mabavu Lebanon na Syria wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Lebanon ilipata uhuru mwaka 1945 na mwaka huo huo ikatia saini makubaliano ya kuondoka askari wa Uingereza na Ufaransa katika ardhi ya nchi hiyo ambayo yalianza kutekelezwa Aprili 1946. 

Bendera ya Lebanon

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita yaani sawa na tarehe 10 Aprili 1973, makachero wa Shirika la Ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD waliwaua maafisa watatu wa Palestina huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Katika kuendeleza jinai zake dhidi ya Wapalestina, miaka kumi baadaye utawala wa Kizayuni wa Israel yaani tarehe 10 Aprili 1983, ulimuuwa huko Ureno, Isam Sartawi aliyekuwa mshauri wa Yassir Arafat kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO). Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitumia mauaji ya kigaidi dhidi ya viongozi wa mapambano ya ukombozi wa Palestina kwa ajili ya kuendelea kujipanua na kuzima mapambano ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina. 

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, inayosadifiana na 21 Farvardin 1367 Hijria Shamsia, ndege za kivita za Iraq ziliushambulia mji wa Marivan magharibi mwa Iran na kukilenga kijiji kimoja kwa mabomu ya kemikali. Raia kadhaa waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika jinai hiyo ya utawala wa Saddam Hussein. Jamii ya kimataifa na hasa nchi za Magharibi zilinyamazia kimya jinai hiyo na badala yake zilitoa misaada zaidi ya silaha za kemikali kwa nchi hiyo.

Wahanga wa mashambulizi ya silaha za kemikali z a Saddam Hussein wanaendelea kuteseka

Miaka 18 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 21 Farvardin 1378 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Meja Jenerali Ali Sayyad Shirazi, Kaimu Kamanda Mkuu wa majeshi yote na mmoja kati ya makamanda shupavu wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu, baada ya kufyatuliwa risasi na vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqiin mjini Tehran. Meja Jenerali Shirazi alikuwa mwanaharakati wa mapinduzi, na alitupwa gerezani mara kadhaa wakati wa utawala wa Shah, na hatimaye aliachiliwa huru baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu. Meja Jenerali Sayyad Shirazi aliwahi kuwa Kamanda wa Jeshi la nchi kavu wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran.

Meja Jenerali Ali Sayyad Shirazi

Na siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, alifariki dunia Joseph-Louis Lagrange, mwanahisabati maarufu wa Ufaransa. Lagrange alizaliwa mwaka 1736 Miladia huko mjini Turin, Italia. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni pamoja na kitabu cha 'Uchunguzi wa Umekanika' ambacho alikiandika kwa kipindi cha miaka 25.

Joseph-Louis Lagrange

 

Tags