Apr 10, 2017 11:30 UTC

Sura ya Luqman, aya ya 7-11 (Darsa ya 731)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 731 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 31 ya Luqman. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya saba ambayo inasema:

وَإِذَا تُتْلَى عَلَيْهِ آيَاتُنَا وَلَّى مُسْتَكْبِرًا كَأَن لَّمْ يَسْمَعْهَا كَأَنَّ فِي أُذُنَيْهِ وَقْرًا فَبَشِّرْهُ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ

Na (mtu kama huyo) anapo somewa Aya zetu huzipa mgongo kwa kujivuna, kama kwamba hakuzisikia, kama kwamba masikioni mwake mna uziwi. Basi mbashirie kuwa atapata adhabu chungu.

Katika aya ya mwisho tuliyoisoma katika darsa iliyopita Quráni tukufu ilisema baadhi ya watu wanaeneza maneno batili na yasiyo na maana ili kuwaburudisha na kuwapumbaza watu kwa lengo la kuwafanya wasiusikilize na kuukubali wito wa maneno ya haki. Baada ya maelezo hayo aya tuliyosoma inasema: Watu wa aina hiyo huwa hawako tayari hata kuzisikiliza aya za Quráni, seuze kuzitafakari, ili kama watabaini kuwa ni za mantiki waziamini. Bila ya shaka chanzo cha ukengeukaji huo na kuipa mgongo haki ni kiburi na majivuno. Kwani watu hao wanajiona wabora na wenye hadhi ya juu zaidi kuliko Bwana Mtume SAW na waumini; na kwa sababu hiyo hawako tayari kusikiliza maneno yao.

Ni wazi kwamba hulka ya aina hiyo inamporomosha mtu na kumfanya afikwe na adhabu na ikabu ya Allah. Kwa sababu ukafiri na ukanushaji wake unatokana na kiburi na ghururi, si ujinga na kutokuwa na uelewa wa aya za Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba hulka ya kutakabari huizuia nafsi isiikubali haki na kumfanya mtu aselelee kwenye upotofu na maangamizi. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kusikiliza maneno ya batili na ya pumbao humwondolea mtu utayari wa kuyakubali maneno ya haki.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya nane na ya tisa ambazo zinasema:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ جَنَّاتُ النَّعِيمِ

Hakika walio amini na wakatenda mema watakuwa na Bustani za neema.

خَالِدِينَ فِيهَا وَعْدَ اللَّهِ حَقًّا وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

Watadumu humo - ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kweli. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Tumeeleza kwamba kuna watu ambao badala ya kufuata maneno ya haki wanayaendea maneno ya batili. Watu kama hao wanaeneza ukafiri na hivyo kuishia kufikwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Lakini kinyume na watu hao, kuna watu ambao kutokana na imani yao juu ya asili ya uumbwaji wao na maadi, yaani kufufuliwa kwao, wanafanya amali njema na hivyo kupata malipo makubwa ya thawabu kwa Mola. Hao ni watu ambao husoma na kusikiliza aya za Quráni kwa makini, wakazitafakari na kuziamini kwa njia ya ufahamu na uelewa. Badala ya kutakabari mbele ya Muumba wa ulimwengu, wanasalimu amri mbele yake Yeye Allah na kuyasikiliza maamrisho yake matukufu na kuamiliana na waja wake kwa unyenyekevu na uraufu. Allah amewaahidi waja kama hao Pepo yake ya milele; na ni hakika kwamba ahadi hiyo itathibiti, kwa sababu Yeye Allah ni mwenye nguvu na mwenye hekima. Si mwenye kushindwa kutimiza ahadi anayotoa au mwenye kuahidi jambo bila ya kupanga na kufikiria. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba imani peke yake au amali njema peke yake haiwezi kumfikisha mtu peponi. Ni imani inayoambatana na amali njema ndiyo yenye tija ya kumfikisha mtu kwenye saada ya milele. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Pepo ni maskani ya anuai za neema za Allah, za kimaada na kimaanawi. Kwa hivyo katika ulimwengu huo, mtu hatojihisi kuchoka, kukirihishwa wala kuhuzunishwa na jambo. Kadhalika aya hizi zinatutaka tuamini ahadi na malipo ambayo Allah SW atakwenda kutupa huko akhera; na wala tusilinganishe ahadi ya Mola na za wengineo ambazo ima huwa za uongo au watoaji wake hawana uwezo wa kuzitimiza.

Darsa ya 731 ya Quráni inahatimishwa na aya ya 10 na 11 ambazo zinasema:

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا وَأَلْقَى فِي الأَرْضِ رَوَاسِيَ أَن تَمِيدَ بِكُمْ وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَابَّةٍ وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاء مَاء فَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ كَرِيمٍ

Ameziumba mbingu bila ya nguzo mnazo ziona; na ameweka katika ardhi milima ili ardhi isikuyumbisheni; na ametawanya humo kila namna ya wanyama; na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha katika ardhi mimea mizuri ya kila namna.

هَذَا خَلْقُ اللَّهِ فَأَرُونِي مَاذَا خَلَقَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ بَلِ الظَّالِمُونَ فِي ضَلالٍ مُّبِينٍ

Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni wameumba nini hao wasio kuwa Yeye! Lakini madhaalimu wamo katika upotevu ulio dhaahiri.

Aya hizi tulizosoma zimeashiria mifano mitano ya ishara za nguvu na uwezo wa Allah SW katika uumbaji.  Ya kwanza ni uimara wa mfumo adhimu wa mbingu na nyota zake ambayo imesimama bila ya kuwa na nguzo au mhimili wowote unaoonekana. Ya pili ni milima yenye adhama, inayoifanya ardhi itulie na kuwa thabiti. Ishara ya tatu ni ya uumbaji wa viumbe mbalimbali hai walioko nchi kavu, baharini na angani. Ya nne ni rehma ya kunyesha mvua; na ya tano ni uotaji wa anuai za mimea na miti. Yote hayo yanaashiria na kuthibitisha kitu kimoja tu ambacho ni nguvu na uwezo usio na ukomo wa Muumba wa ulimwengu, ambaye hakuna mtu wala kitu chochote kilichokuwa mshirika wake katika uumbaji wa vitu hivyo. Katika aya hizi zimeashiriwa nguzo na mihimili isiyoonekana inayozifanya sayari na maumbo ya angani yapite kwenye mizingo yao inayodumisha hali ya mlingano baina yao. Aidha katika aya hizi imeashiriwa nafasi muhimu ya milima katika kuifanya ardhi ibaki kuwa thabiti pasina kuyumba. Hii ni mifano michache tu ya miujiza ya kielimu na kisayansi ya Qur'ani. Ni ajabu kwamba mambo hayo yalizungumziwa katika zama ambazo mwanadamu hakuwa akijua chochote kuhusu masuala hayo.

Hata hivyo pamoja na kuwepo ishara za wazi kabisa katika ulimwengu wa maumbile juu ya kuwepo Mwenyezi Mungu, kwa masikitiko ni kwamba kwa sababu ya kutokuwa na uelewa au kutokana na imani potofu, baadhi ya watu wamewaweka wanadamu wenzao au vitu katika daraja ya uungu kwa kudhani kwamba watu au vitu hivyo vina taathira katika hatima na majaaliwa yao. Ni kama kwamba sehemu moja ya ulimwengu huu wa maumbile wamekabidhiwa washirika hao; na ni wao, badala ya Allah, ndio wanaoshughulikia uendeshaji wake. Kutokana na kuwepo imani hiyo, aya zinaendelea kuwahutubu watu hao kwa kuhoji: Wale ambao nyinyi mnawafanya washirika wa Mwenyezi Mungu, walishirikiana na Yeye Mola katika uumbaji wa kipi kati ya vitu vya ulimwengu wa maumbile? Hawana uwezo wa kuumba hata nzi au mbu sembuse mbingu na mimea. Kisha aya zinamalizia kwa kueleza kwamba fikra na imani ya aina hii ni dhulma kwa nafsi yake mtu mwenyewe na dhulma kwa Mwenyezi Mungu, kwa mtu kukifanya kiumbe kilichoumbwa na Yeye Allah kuwa mshirika wake Yeye Mola; na badala ya Mwenyezi Mungu, kwenda kumwabudu mwingine asiyekuwa Yeye. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuning'inia mbinguni mabilioni ya nyota, sayari na maumbo ya angani ni ishara ya nguvu na uwezo wa Allah na pia ni hoja ya kuthibitisha muujiza wa Qur'ani ambayo imelinasibisha jambo hilo na uwepo wa mihimili isiyoonekana, ambayo leo hii inaelezewa kuwa ni Kani ya Mvutano, kwa kimombo Force of Gravity. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa maji, udongo, mimea na maumbile kwa jumla ni vitu vyenye thamani mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwanadamu naye anapaswa ajue kwamba mazingira ni kitu chenye thamani hivyo aitunze amana hiyo kubwa aliyokabidhiwa na Mola kama inavyostahiki. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba njia mojawapo ya kumjua Mwenyezi Mungu ni kulinganisha nguvu na uwezo wake Yeye na uwezo wa wasiokuwa Yeye. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba watu wanaomwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu wanatenda dhulma inayowafanya waishie kwenye upotofu. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 731 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuzidishie elimu na ujuzi wa kuzitambua ishara zake utakaozijaza nyoyo zetu imani thabiti juu yake. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags