Hadithi ya Uongofu (71)
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 71 ya mfululizo huu kitatupia jicho moja ya tabia mbaya nayo ni kuchunguza na kupekua aibu za watu wengine. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 10 hadi ya 12 za Surat al-Hujuraat:
Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe. Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini. Na wasio tubu, hao ndio wenye kudhulumu. Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.
Aya zilizotangulia zinazitaja tabia kama za mtu kumdharua mwenzake, kuvunjiana heshima, kuitana majina ya kejeli, kuwa na dhana nyingi, kupeleleza na kupekua mambo ya watu, kusengenya na mengineyo kwamba, ni sababu ya kuondoka hali ya mshikamano na maelewano baina ya watu.
Kwa hakika ni jukumu la Mwislamu pindi anapoona aibu au mapungufu ya ndugu yake katika dini, basi amueleze kwa siri yaani kando na watu wengine na kwa njia nzuri na ya kujenga badala ya kutumia maneno ambayo badala ya kujenga utabomoa.
Kwa hakika kutafuta na kuchunguza aibu na mapungufu ya watu ni moja ya maradhi ya kimaadili na kiakhlaqi ambayo hupelekea kuondoka na kuporomoka heshima ya watu wengine. Wapekuaji wa aibu za watu kwa kitendo chao hicho kilicho dhidi ya maadili, huharibu heshima na thamani ya watu na hivyo kupelekea kuweko hali ya kudhaniana vibaya baina ya watu, suala ambalo hatimaye hupelekea kuibuka ufisadi. Sifa na tabia hii mbaya inatambuliwa na kioo cha mafundisho ya Uislamu kuwa ni katika madhambi makubwa. Maradhi haya ya kimaadili chimbuko lake ni ghururi, kujiona, kuwa na hisia ya kupenda jaha na husuda. Wenye kuchunguza aibu za wengine ni watu ambao kutokana na kutofahamu uhalisia wa hali yao, hutembea kiguu na njia kutafuta makosa na mapungufu ya wengine na hivyo kufunua pazia la aibu na makosa ya watu wengine. Hapana shaka kuwa, kama mtu atazingatia na kuangalia aibu na mapungufu alionayo na akafanya hima na juhudi za kujirekebisha, basi hatakuwa ni mwenye kuzingatia na kufuata kupekua aibu na mapungufu ya watu wengine.
Mtume saw amenukuliwa akisema: Msichunguze na kutafuta aibu za Waislamu. Kila ambaye atafuatilia aibu za ndugu yake, Mwenyezi Mungu atafuatilia aibu zake. Na kila ambaye Mwenyezi Mungu atafuatilia aibu zake humuumbua hata kama atakuwa ndani ya nyumba yake.
Kwa hakika akthari ya matatizo ya jamii hutokea pale kila mtu anapoamua kuingilia maisha ya mwengine na kuchunguza aibu na mapungufu ya mwenziwe. Hapana shaka kuwa, mtu anapoamua kupekua na kupeleleza aibu za mwengine hatoishia tu katika kufahamu mapungufu na aibu za mwenzake huyo, bali hatua itakayofuata ni kusengenya na kutoa tuhuma, jambo ambalo lenyewe hilo ni kutenda dhambi kubwa.
Moja ya mambo ambayo yameusiwa na kutiliwa mkazo na dini Tukufu ya Kiislamu ni kuficha na kusitiri aibu za waja wa Mwenyezi Mungu. Kusitiri aibu kinyume na kupeleleza na kufichua aibu za watu jambo ambalo hupelekea kuibuka ugomvi, mivutano na utengano, lenyewe huwa chimbuko la kuimarika urafiki, huba na kuongezeka hali ya kuaminiana baina ya watu. Imam Ali bin Abi Twalib AS amenukuliwa akisema kuwa: Funika na kusitiri aibu za watu kadiri inavyowezekana, kama unavyopenda Mwenyezi Mungu afunike na kustiri aibu zako mbele ya macho ya watu.
Mtume Muhammad SAW ambaye ni mwanadamu mkamilifu kabisa na mbora wa viumbe alijipamba na suala la kufunika na kutofichua aibu za wengine na alikuwa akiwausia wafuasi wake kwa kuwaambia: Kila ambaye ataficha na kufunika aibu ya ndugu yake Mwislamu na kutomuumbua, basi Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama atazistiri aibu zake.
Nukta muhimu ya kuzingatia hapa ni hii kwamba, makusudio ya kufunika na kutotaja aibu za mtu ni kutofichua mapungufu aliyonayo mtu huyo. Pamoja na hayo jukumu la kuamrishana mema na kukatazana maovu linalazimu mtu kumueleza ndugu yake Mwislamu aibu na mapungufu aliyonayo, lakini hilo kama tulivyoashiria katika kipindi chetu cha juma lililopita ni jambo ambalo linapaswa kufanyika kwa siri na njia bora na yenye maneno mazuri na ya kuvutia kiasi cha kutomfanya mlengwa achukie.
Viongozi wakubwa wa Uislamu wametoa nasaha zenye thamani kubwa mno kuhusiana na kufunika aibu za watu hususan viongozi kusitiri aibu za raia. Tunasoma katika sehemu ya barua ya Imam Ali bin Abi Twalib AS kwa Malik al-Ashtar kwamba:
"Baina ya watu kuna aibu na mapungufu yaliyojificha, hivyo usiondoe pazia lake. Mwenyezi Mungu mwenyewe anahukumu kuhusiana na mambo ya siri. Ficha na usitiri aibu na mapungufu kadiri unavyoweza ili Mwenyezi Mungu naye asitiri na kuficha aibu zako ambazo unapenda zibakie kuwa ni siri.”
Katika sehemu nyingine ya nasaha zake kwa viongozi, Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema:
“Wasiwahesabie raia mambo madogo madogo bali fumbia macho mambo mabaya na ongeza kiwango cha thamani yako.”
Moja ya sifa mbaya za kimaadili na kiakhlaqi ni mtu kutoona aibu zake na badala yake kuzingatia aibu za wengine. Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa Imam Ali bin Abi Twalib AS ni kuwa;
Aibu na mapungufu makubwa zaidi ni kushughulishwa na aibu za wengine ilihali aibu hizo hizo na wewe unazo.
Wanadamu wakubwa na wacha Mungu badala ya kutafuta na kuchunguza aibu za wengine hujichunguza wao na kuangalia aibu na mapungufu waliyonayo na kufanya hima ya kujirekebisha.
Imam Ali AS amenukuliwa akisema kuwa, hongera zimuendee mtu ambaye anazingatia aibu zake na anajizuia kufuatilia na kuchunguza aibu za wengine. Tukirejea mafundisho na ya Uislamu na hadithi tunapata kuwa imesisitizwa na kutiliwa mkazo juu ya suala la mtu kuangalia aibu na mapungufu yake kabla ya kuangalia aibu za wengine. Imam Ali AS anasema: Mtu anayetazama aibu za watu anapaswa kuanza na aibu zake.
Aidha Mtume SAW amenukuliwa katika hadithi mashuhuri akisema kuwa, ukitaka kutaja aibu za mwanzako kwanza kumbuka aibu zako.
Ukweli wa mambo ni kuwa, kuna watu katika jamii ni mahodari mno wa kukosoa watu wengine na kuona aibu na mapungufu ya wenzao lakini mapungufu na aibu hizo hizo na wao wanazo. Hivyo basi mtu huyu kabla ya kutaja aibu za wengine anapaswa kukumbuka kwanza aibu zake.
Kwa leo tunakomea hapa kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki. Tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Hadiyhi ya Uongofu.