Hadithi ya Uongofu (73)
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami tena juma hili katika sehemu nyingine ya mfululizo wa kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu ambacho hujadili na kuzungumzia masuala mbalimbali ya kijamii, kidini, kimaadili na kadhalika na kukunukulieni hadithi na maneno ya hekima kuhusiana na maudhui hizo kutoka kwa Bwana Mtume saw, Ahlul Baiti wake watoharifu as na waja wema wa Mwenyezi Mungu.
Kipindi chetu kilichopita kilikunukulieni baadhi ya hadithi zinazohusiana na maudhui ya kuchunguza na kutaja aibu za wengine na tuliona jinsi tabia hiyo ilivyokemewa na kukatazwa na mafundisho ya Kiislamu. Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 73 ya mfululizo huu kitajadili na kuzungumzia suala la kujiweka mbali na dhambi na mambo machafu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hili ili muweze kunufaika na yale niliyokuandalieni kwa juma hili. Karibuni.
Dhambi ina athari mbaya kwa maisha ya watu. Athari ya kwanza ya dhambi ni Mwenyezi Mungu kumtia katika mabalaa na misiba katika maisha yule anayetenda dhambi ili azinduke na kukumbuka. Imam Ja'far Swadiq as anasema: Kila balaa na na masaibu na hata kuumwa na kichwa na maradhi anayokumbwa nayo mwanadamu ni athari ya dhambi. Ushahidi wa hilo ni aya ya 30 ya Surat al-Shuura ambapo Mwenyezi Mungu anasema: Na misiba inayokusibuni ni kwa sababu ya vitendo vya mikono yenu. Naye anasamehe mengi.
Tab’an inapasa kufahamu kuwa, masaibu na mabala yaliyowapata baadhi ya Manabii na Mawalii wa Mwenyezi Mungu yalikuwa ni kwa ajili ya kuwapandisha daraja au kuwatia majaribuni. Aidha baadhi ya matatizo na mitihani inayowakumba watu ambao sio Maasumina ina engo mbili. Engo ya kwanza ni ya mtihani na kutiwa katika majaribu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 155 ya Surat al-Baqarah kwamba: Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya hofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanaosubiri.
Engo ya pili ni kwamba, wakati mwingine matatizo na mabalaa hayo chimbuko lake mo uzembe na kutopata ushauri mtu katika masuala hayo ambapo natija ya kawaida ya kutokuwa makini si nyingine ghairi ya hii yaani ya kukumbwa na balaa na masaibu.
Wakati mwingine nia ya dhambi fulani hupelekea mtu kunyimwa baadhi ya riziki. Riziki haiishii tu katika masuala ya kimaada kama chakula na kadhalika, bali ni kila kitu ambacho mtu ananufaika nacho iwe ni cha kimaada au cha kimaanawi. Imani na tawfiqi ya kufanya ibada nayo ni riziki na kunyimwa na kutopata tawfiki ya hilo mara nyingi hutokana na kutenda dhambi. Imam Ja’afar Swadiq as anasema kuwa: Kuna wakati mtu anasema uongo, na uongo huo kumpelekea akose tawfiki ya kuswali Sala za usiku. Wakati anaponyimwa tawfiki ya kuswali Sala za Usiku hunyimwa pia riziki yaani kipaji cha kimaada na kimaanawi.
Kwa hakika kutenda dhambi humfanya mtu akengeuke njia nyoofu na hivyo kuwa mbali kabisa na haki. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Mtume saw na Maimamu watoharifu as wamesisitiza mno juu ya kujiweka mbali na madhambi. Imekuja katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume saw kwamba: Mtu mwenye kuabudu zaidi miongoni mwa watu ni yule anayetekeleza mambo ya wajibu na mwenye hima na idili zaidi ni yule ambaye anajiweka mbali na dhambi. Imam Muhammad Baqir as amenukuliwa akisema: Inashangaza kuwa, watu wanachukua tahadhari katika ulaji wa vyakula kwa kuhofia kupata maradhi; lakini hawajiweki mbali na madhambi kwa hofu ya moto wa Jahanamu.
Kwa hakika kadiri mtu anavyokuwa karibu zaidi na fitra ya Mwenyezi Mungu, kujiweka mbali na dhambi kwake huwa ni jambo jepesi zaidi, kinyume na hivyo kujiweka mbali na dhambi huwa ni jambo gumu mno kwake.
Kwa hakika kujiweka mbali na madhambi na kutenda amali njema ni miongoni mwa sifa za wazi za watu wanaoshikamana na imani. Mtume saw anasema katika kuwasifia waumini kwamba: Moyo wa Muumini uko safi kunako mambo machafu ya kimaadili. Kwa upande wake Imam Ali bin Hussein al-Sajjad as anasema kuwa: Moja ya ishara za muumini ni kujiweka mbali na dhambi hata akiwa faraghani. Ukweli ni kuwa, kadiri imani ya mtu inavyokuwa dhaifu, basi mtu huyo huwa na ujeuri na kiburi cha kufanya dhambi kuliko mtu mwingine.
Imam Ali as amenukuliwa katika hadithi moja akiwataka waumini wapambane na matamanio ya nafsi zao kabla nafsi hizo hazijazoea na kupindukia katika mambo hayo; kwani kama ukengeukaji huo utaimarika na kupata nguvu utakuwa ndio kiongozi wa mtu na hivyo kumpeleka mtu popote utakapo na natija ya hilo ni mtu kupoteza nguvu ya kupambana na matamanio ya nafsi.
Katika sehemu nyingine Imam Ali bin Abi Twalib as anawataka waumini wapambane na nafasi zao katika kuacha dhambi ili kujivuta kuelekea upande wa uja na ibada liwe ni jambo rahisi na jepesi.
Siku moja Bwana Mtume saw alimwambia Swahaba wake Abdullah bin Mas'ud kwamba" Ewe mwana wa Mas'ud! Jihadhari na kulewa dhambi, kwani dhambi pia ni kama pombe, huleweshwa bali ulevi wa dhambi ni mkubwa na shadidi zaidi. Kisha Mtume saw akasoma aya ya 18 iliyoko katika Surat al-Baqara inayosema:
"Viziwi, mabubu, vipofu; kwa hivyo hawatarejea."
Pombe hulewesha mtu; na mtu aliyelewa huwa hafahamu anachokifanya, hupayuka na kusema ovyo, hutukana, hufanya mambo yasiyo na heshima na adabu na hata wakati mwingine huvua nguo na kufanya mambo ya kumvunjia heshima na staha. Hii ni kutokana na kuwa, amelewa na hajui alitendalo. Mambo anayoyafanya akiwa amelewa hawezi kuyafanya kabla ya kulewa au baada ya pombe kumtoka kichwani. Kwa maneno mengine ni kuwa, mtu aliyelewa, akili si yake yaani hayuko katika hali yake ya kawaida. Hii kwamba, Bwana Mtume saw anasema, ulevi wa dhambi ni mbaya na shadidi zaidi ya ulevi wa pombe ni kutokana na kuwa, ulevi hubakia katika akili ya mtu kwa masaa kadhaa na kisha humtoka. Lakini ulevi wa dhambi, huleta mazoea ya kutenda dhambi na mtendaji dhambi huwa mraibu wa kutenda dhambi; hivyo huwa ni kama kipofu asiyeona na na kiziwi asiyesikia.
Imam Muhammad Baqir as anasema, hakuna mja isipokuwa katika moyo wake kuna sehemu ambayo ni nyeupe. Kila anapotenda dhambi katika sehemu ile hujitokeza doa jeusi. Endapo atatubu, doa lile jeusi hufutika na kuondoka. Lakini kama ataendelea kutenda dhambi, doa lile jeusi mduara wake hupanuka na kuwa mkubwa mpaka likafunika sehemu yote ile na yote kuwa nyeusi. Wakati sehemu ile nyeupe inapobadilika na kuwa nyeusi yote, mwenye moyo ule katu hawezi kuona ukweli na uhakika. Maneno haya yanaungwa mkono na aya ya 14 ya Surat al-Mutaffifiin inayosema:
"Hasha! Bali yametia kutu juu ya nyoyo zao hao walio kuwa wakiyachuma."
Wapenzi wasikilizaji kwa aya hiyo ndio tunahitimisha kipindi chetu cha juma hilo basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo ninakuageni nikimuomba Mwenyezi Mungu atujaalie na kutupa tawfiki ya kujitenga mbali na dhambi na tufanye yale yenye ridhaa Yake ili tuweze kupata saada na mafanikio hapa duniani na kesho akhera.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.