May 09, 2017 04:19 UTC
  • Jumanne 9 Mei 2017

Leo ni Jumanne 12 Shaaban 1438 Hijria, sawa na Mei 9, 2017.

Siku kama ya leo miaka 364 iliyopita, kazi ya ujenzi wa jengo la Taj Mahal linalohesabiwa kuwa miongoni mwa majengo ya kuvutia zaidi duniani na moja kati ya mifano bora zaidi ya usanifu majengo wa Kiislamu huko India ilimalizika baada ya miaka 22. Ujenzi wa jengo la Taj Mahal ulianza baada ya kufariki dunia mke wa Shah Jahan, mfalme wa India huko katika jimbo la Agra. Jengo hilo lilijengwa kwa kutegemea ramani iliyochorwa na msanifu majengo mashuhuri wa Iran, Issa Isfahani. Kwa upande wa nje, jengo la Taj Mahal limenakshiwa kwa ustadi kwa rangi mbalimbali huku kuta zake zikiwa zimeandikwa maandishi ya Kiarabu yenye aya za Qur'ani Tukufu. Ndani ya jengo hilo kuna makaburi mawili ya mfalme Shah Jahan na mkewe, Nur Jahan.

Taj Mahal

Miaka 101 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 9 Mei, mkataba wa kihistoria wa Sykes-Picot ulitiwa saini na wawakilishi wa Uingereza, Ufaransa na Urusi ya zamani. Hata hivyo Umoja wa Kisovieti baadaye ulijitoa kwenye makubaliano hayo baada ya mapinduzi ya Bolshevik. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, tawala za Uingereza na Ufaransa ziligawana nchi za Kiarabu zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Kiothmania. Kwa msingi huo Iraq na Jordan zikawa chini ya udhibiti wa Uingereza huku Syria na Lebanon zikitawaliwa na Ufaransa.

Sykes na Picot

Miaka 90 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 19 Ordibehesht mwaka 1306 Hijria Shamsia, sheria ya "Capitulation' ilifutwa na Bunge la Kitaifa la Iran. Kimsingi sheria hii ilikuwa na lengo la kuwapa kinga ya kutoshtakiwa raia wa kigeni waliopatikana na hatia ya kufanya uhalifu nchini Iran. Haki ya  'Capitulation' ilitumika mara ya kwanza nchini Iran baada ya mapatano ya Torkmanche ya mwaka 1206 wakati wa utawala wa Fath-Ali Shah ambapo Warusi walipata kinga hiyo na baada ya hapo serikali zingine za kigeni nazo ziliweza kupata haki hiyo ya raia wao kutoshtakiwa nchini Iran. Hata hivyo sheria hiyo ilipitishwa tena na bunge la kitaifa la Iran mwaka 1343 kwa lengo la kuwapa kinga Wamarekani. Imam Khomeini MA alipinga vikali sheria hiyo na utawala wa Shah ulikasirishwa sana na malalamiko hayo na ukachukua uamuzi wa kumbaidisha Imam nchini Uturuki. Hatimaye, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, sheria ya 'Capitulation' ilifutwa daima nchini Iran.

Capitulation

Tarehe 9 Mei miaka 212 iliyopita aliaga dunia mwandishi, malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kijerumani kwa jina la Johann Christoph Friedrich von Schiller akiwa na umri wa miaka 46. Von Schiller alipenda sana masuala ya uandishi tangu utotoni mwake. Friedrich Von Schiller alikuwa hodari katika fasihi ya Kijerumani na anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waandishi mahiri wa Kijerumani katika uga wa fasihi.

 

 

Tags