May 24, 2017 02:16 UTC
  • Jumatano, 24 Mei, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 27 Shaaban 1438 Hijria sawa na tarehe 24 Mei mwaka 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 612 iliyopita  Ibn Araqi fakihi na kadhi wa Kiislamu wa Misri aliaga dunia katika mji wa Makka. Alizaliwa mwaka 762 na alihudhuria darsa na masomo ya wanazuoni mashuhuri wa zama hizo katika elimu ya hadithi. Ibn Araqi baada ya kunufaika na elimu ya walimu wa zama hizo alifanikiwa kuingia katika faharasa ya maulama mashuhuri  na kuanza kufundisha elimu za fikihi na hadithi.  Msomi huyo ameandika vitabu kadhaa kwa lugha ya Kiarabu.***

Ibn Araqi

Katika siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, nchi ya Eritrea iliyoko kaskazini mashariki mwa bara la Afrika ilipata uhuru kutoka kwa Ethiopia. Mwaka 1936 Italia iliikalia kwa mabavu Eritrea iliyokuwa ikihesabiwa katika zama hizo kuwa sehemu ya ardhi ya Ethiopia. Mwaka 1953, Italia iliirejeshea Ethiopia ardhi hiyo. Hata hivyo wananchi wengi wa nchi hiyo waliokuwa wakitaka uhuru walianzisha harakati za ukombozi dhidi ya serikali ya Ethiopia. Mwaka 1991, Harakati ya Ukombozi wa Eritrea ikisaidiana na wanamapinduzi wa Ethiopia walihitimisha utawala wa kidikteta wa Mengistu Haile Mariam, na wakakubaliana kuanishwa mustakbali wa Eritrea mwaka 1993 kupitia kura ya maoni. Washiriki wengi wa kura hiyo ya maoni walipiga kura ya kutaka kujitawala Eritrea. ***

Eritrea

Miaka 17 iliyopita katika siku kama ya leo, vikosi vya utawala dhalimu wa Israel vililazimika kuondoka kwa madhila katika eneo la kusini mwa Lebanon baada ya kulikalia kwa mabavu eneo hilo kwa muda wa miaka 22. Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na mapambano ya wananchi wa kusini mwa Lebanon. Mwaka 1982, majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yalishambulia Lebanon na kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut. Hata hivyo kutokana na wananchi hao kuathirika na mafunzo ya kutokubali dhulma hasa baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, nchini Lebanon kulianzishwa harakati za mapambano ya Kiislamu dhidi ya majeshi vamizi ya utawala haramu wa Israel. Chama cha Hizbullah kilikuwa na nafasi muhimu na ya kuzingatiwa mno katika kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon toka katika makucha ya utawala dhalimu wa Israel.***

Lebanon

Na miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo, mji wa Khorramshahr wa Iran ulikombolewa na wapiganaji wa Kiislamu na ukaondoka katika uvamizi wa majeshi vamizi ya Iraq. Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo  ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu mwaka mmoja na miezi minane. Uvamizi dhidi ya mji huo ulijiri mwanzoni mwa vita vya miaka minane vya kulazimishwa Iran na Iraq. Siku hii inajulikana katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuwa, "Siku ya Muqawama na Ushindi". 

Kukombolewa mji wa Khorramshahr

 

Tags