Hadithi ya Uongofu (76)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na ni matumaini yangu kuwa hamjambo popote pale mlipo. Tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia sifa mbaya ya kupenda jaha na uongozi. Tulisema kuwa, kupenda jaha maana yake ni kuwa na mapenzi ya kupindukia ya uongozi na cheo kiasi kwamba, katika mazingira kama haya, mtu wa aina hii awe yuko tayari kufikia lengo hilo kwa thamani yoyote ile.
Kupenda jaha na uongozi ni miongoni mwa mambo hatari mno ambayo sio tu hutoa pigo kwa mtu katika upande wa kimaanawi, bali kwa mtazamo wa kijamii humfanya mtu huyo achukiwe na kutengwa.
Hali hii ya kupenda mno jaha na uongozi hupelekea kupatikana nifaki katika moyo wa mwanadamu. Mtume Muhammad saw amenukuliwa akisema kuwa, kupenda jaha na uongozi ni mithili ya maji ambayo hupelekea kukua majani, basi ndivyo ambavyo pia nifaki hukua na kustawi katika moyo wa mwanadamu. Dini tukufu ya Kiislamu imekemea mno suala la mtu kupenda jaha na uongozi. Moyo ambao unapiga na kudunda kutokana na kupenda kukuza jina hauwezi kuwazingatia watu bali huwa mtumwa wa hilo unalolihangaikia.
Watu wanaopenda jaha na uongozi daima hufanya hima ya kuhifadhi na kulinda uongozi wao usiwatoke na daima hufanya juhudi kadiri wawezavyo ili kuhakikisha kwamba, vyeo walivyonavyo wanaendelea kuwa navyo kwa thamani yoyote ile. Mtu wa namna hii huugua na kupata maradhi mara anapopoteza cheo au uongozi alionao. Watu wa aina hii husononeka na kupata maradhi ya nafsi mara wanapopokonywa vyeo na madaraka walionayo.
Katika sehemu hii ya 76 ya mfululizo huu tutazungumzia moja ya tabia mbaya na ambayo imekemewa mno na dini Tukufu ya Kiislamu nayo ni ile ya mtu kufurahia msiba, matatizo na masaibu ya mtu mwingine. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo.
Mtu kufurahia matatizo na masaibu ya mwenzake ni miongoni mwa vitendo ambavyo havichukiwi na dini tu bali hata akili ya kila mwanadamu inalichukia jambo hilo. Akili na roho ya mwanadamu kikawaida ni yenye kutaka urafiki, mahaba na mahusiano mazuri na watu wengine. Urafiki huu huongeza hali ya kuwa pamoja na watu wengine katika masaibu na matatizo yanayowakumbwa. Hata fitra na maumbile safi ya mwanadamu sio tu kwamba, inachukia hali ya mtu kuonyesha furaha kwa sababu ya balaa na ghamu iliyowapata watu wengine, bali inalikemea jambo hilo. Maimamu watoharifu as waliitambua furaha hiyo kuwa miongoni mwa mambo mabaya na waliwakataza wafuasi wao kuonyesha furaha kwa matatizo na msaibu ya wengine.
Mtume Muhammad saw amenukuliwa akisema kuwa: Usionyeshe furaha kwa matatizo ya ndugu yao, kwani Mwenyezi Mungu atampatia rehema mtu kama huyo na atakupatia balaa wewe. Kwa hakika kama zilivyo mbaya tabia nyingine kama husuda, kusengenya, kusema uongo na kuchunguza aibu za wengine na kadhalika, vivyo hivyo kuonyesha furaha kwa matatizo ya wengine ni maradhi ambayo yanahitajia tiba. Hali hii hutokana na ujahili na ujinga kuhusiana na hekima ya Mwenyezi Mungu katika mambo mbalimbali. Hii ni kutokana na kuwa, katika mambo mengi Mwenyezi Mungu akiwa na lengo la kufidia makosa ya huko nyuma ya mtu au akiwa na nia ya kumkweza daraja mja wake, basi humtia katika majaribu na mitihani kwa kumshushia balaa na kumtia katika matatizo na masaibu. Tukirejea kisa cha Nabii Ayyub as tunaona kuwa, baada ya Mwenyezi Mungu kumtia katika balaa na masaibu makubwa, mja mwema huyo alisubiri. Hata hivyo baadhi ya watu wakawa wakionyesha furaha na hata kumlaumu kutokana masaibu hayo hali iliyomfanya Mtume huyo wa Allah kupata maudhi. Nabii Ayyub as alimuomba Mwenyezi Mungu amuokoe kutokana na hilo. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 41 ya Surat Saad: Na mkumbuke mja wetu Ayubu alipo mwita Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika Shet'ani amenifikishia udhia na adhabu.
Baada ya Nabii Ayyub as kufanikiwa kupita salama na kushinda masaibu na majaribu yote ya Mwenyezi Mungu, mmoja wa masahaba na watu wake wa karibu alimuuliza: Ni kipi kilichokuwa kigumu zaidi kwako wakati ulipokumbwa na mitihani na majaribu ya Mwenyezi Mungu? Nabii Ayyub as alijibu kwa kusema: Kilichokuwa kigumu kwangu ni furaha ya marafiki na maadui kwa masaibu na majaribu niliyokuwa nayo.
Kuonyesha furaha kwa mtihani na masaibu ya wengine kuna matokeo mabaya kwa mhusika hapa duniani na kesho Akhera. Moja ya athari mbaya za kitendo hicho hapa duniani ni mtu kukumbwa na mitihani na masaibu yale yale yaliyomkumba mwenzake na yeye akawa ni mwenye kuyafurahia.
Imam Ja’afar Swadiq as anasema: Kila mtu ambaye ataonyesha furaha kwa matatizo na mitihani iliyompata ndugu yake, hataondoka katika dunia hii (hatafiriki dunia) isipokuwa atatiwa katika majaribu na mitihani ile ile; na huko Akhera Mwenyezi Mungu hatazungumza naye. Hii ni kutokana na kuwa, imepokelewa katika Hadith al-Quds ya kwamba Allah amesema: Mwenye kumuudhi mja wangu muumini, ametangaza vita na mimi.
Aidha Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa, mwenye kumuudhi muumini ameniudhi mimi na mwenye kuniudhi mimi amemuudhi Mwenyezi Mungu na mwenye kumuudhi Mwenyezi Mungu amelaaniwa. Kadhalika katika kitabu cha Man la Yahdhuruh al-Faqih cha Sheikh Saduuq imepokewa kuwa, Mtume saw alimwambia Imam Ali as: Ewe Ali! Muumini ana alama tatu: Swala, Zaka na Saumu. Na mtu ambaye anayafanya maisha yake kuwa magumu na yenye mashaka ana alama tatu: Mosi, anajipendekeza mbele ya mtu, na mtu huyo anapokuwa hayupo anamsengenya na anapopatwa na masaibu na matatizo hufurahia hilo. Nukta ambayo tunapaswa kuiashiria hapa ni hii kwamba, mtu anayefurahia mitihani na masaibu ya mwenzake kikawaida huwa hatambui kwamba, kufanya hivyo ni kumkosoa Mwenyezi Mungu SWT. Hii ni kutokana na kuwa, katika baadhi ya mambo Mwenyezi Mungu humtia majaribuni mtu fulani kutokana na hekima fulani ambapo majaribu na mitihani hiyo sio kwa sababu ya matendo yake ya huko nyuma, bali ni kutokana na hekima fulani anayoijua yeye Mola Muumba.
Mtume Muhammad saw amenukuliwa akisema kuwa: Unapowaona watu wenye matatizo na masaibu mshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna ambayo hawatasikia yaani mshukuru Allah taratibu, kwani kinyume na hivyo watakuwa watu wa huzuni na ghamu.
Tab’ani katika ulimwengu wa leo daima kuna watu ambao huwalaumu watu wengine na kufurahia taabu na mitihani waliopata na hata kuonyesha kwamba, wamekumbwa na hayo kwa kujitakia. Kwa muktadha huo mtu anapaswa kufanya mambo yake kwa kutumia akili na kwa mujibu wa sheria za Mwenyezi Mungu na hivyo kutoathirika na furaha au hata lawama za wale wanaofurahia masaibu ya wengine na hivyo kusonga mbele katika njia ya haki.
Katika aya ya 54 ya Surat al-Maidah Mwenyezi Mungu anawazungumzia watu anaowapenda kwa kusema:
Enyi mlio amini! Atakaye iacha miongoni mwenu Dini yake, basi Mwenyezi Mungu atakuja leta watu anao wapenda nao wanampenda, wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu juu ya makafiri, wanapigania Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama ya anaye laumu.
Kwa leo tunakomea hapa wapenzi wasikilizaji nikitaraji kuwa, mtakuwa nami juma lijalo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Ahsanteni na kwaherini….