Jumamosi, Juni 8, 2017
Leo ni Jumamosi tarehe 8 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1438 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 3 Juni mwaka 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 763 iliyopita, alifariki dunia Najmuddin Ali Dabiran maarufu kwa jina la Katibi ambaye alikuwa mwanafalsafa na mnajimu mkubwa wa Kiirani. Hakuna maandiko yanayoashiria historia ya kipindi cha awali cha maisha ya msomi huyu lakini maisha yake yanaonesha kuwa Khaja Nasiruddin Tusi alimtaka Katibi kumsaidia katika kituo chake cha elimu ya nujumu huko Maraghe. Najmuddin Ali Dabiran au Katibi kama anavyojulikana zaidi ameandika vitabu kadhaa kama "Jamiud Daqaiq" na "Hikmatul Ain". ***
Katika siku kama ya leo miaka 515 Vasco da Gama baharia wa Kireno alifanya mauaji ya umati huko Calicut, mji ambao hivi sasa umepewa jina la Kozhikode, ni bandari iliyoko huko Madras kusini mwa India. Bandari hiyo ilikuwa eneo la kwanza alipofikia baharia Vasco da Gama mwaka 1498 Miladia na baadaye kulikalia kwa mabavu eneo hilo. Vasco da Gama kama walivyo wakoloni wengine, alidai kuwa mmiliki halisi wa India. Vasco da Gama alitoa amri ya kukatwa, masikio na pua za mabaharia wa Kiarabu wakati walipowasili katika bandari ya Calicut kwa ajili ya kufanya biashara ya mchele. Pia aliwauwa kwa umati wafanyabiashara hao wa Kiarabu baada ya kuzichoma moto meli zao. ***
Miaka 350 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa mara ya kwanza katika historia ya tiba na upasuaji, kitendo cha kuongezwa damu katika mwili wa binadamu kilifanyika. Damu hiyo iliwekwa kwa mwanadamu na tabibu wa Kifaransa aliyeitwa Jean Baptiste Denis. Utiaji damu huo kwa wagonjwa, ulihesabiwa kuwa tukio na mafanikio makubwa katika sayansi ya tiba. Hii ni kwa sababu zama hizo wagonjwa wengi walipoteza maisha yao kutokana na kuvuja damu nyingi na ukosefu wa damu. Katika jaribio lake la kwanza, tabibu huyo wa Kifaransa alichukua damu ya kondoo na kuitia katika mwili wa mwanadamu, na baadaye akawa akiwaongeza wagonjwa damu ya wanadamu. ***
Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, alifariki dunia Nazim Hikmet malenga mashuhuri wa Kituruki. Alizaliwa mwaka 1902 na kuanza kutunga mashairi akiwa na umri wa miaka 12. Malenga huyo wa Kituruki alijiunga na jeshi la nchi hiyo baada ya kuhitimu masomo yake ya shule ya upili. Lakini mwaka 1920, Nazim Hikmet alijiondoa jeshini kutokana na misimamo yake ya kisiasa. Kisha alielekea Moscow mji mkuu wa Urusi ya zamani kwa ajili ya kuendelea na masomo yake na baadaye akarejea Uturuki baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu katika fani ya uchumi wa kisiasa. Baada ya hapo, Nazim Hikmet akaanza kutunga mashairi ya kimapinduzi dhidi ya ufashisti, yaliyokuwa yakiukosoa utawala wa kidikteta wa Ataturk, rais wa kwanza wa Uturuki. ***
Na miaka 54 iliyopita Imam Khomeini (M.A), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa hotuba kali ya kihistoria dhidi ya utawala wa kitwaguti wa Iran, kwa mnasaba wa Ashura ya Imam Husseini (A.S). Imam Khomeini alitoa hotuba hiyo mbele ya hadhara kubwa ya wananchi na wanazuoni katika Madrasa ya Faidhiya katika mji mtakatifu wa Qum hapa nchini, licha ya vizuizi na vitisho vya utawala wa Shah. Imam alikosoa vikali usaliti wa utawala wa Shah na vibaraka wake na kukosoa usaliti wa utawala huo dhidi ya wananchi Waislamu wa Iran. Sehemu ya hotuba ya Imam Khomeini ilisema hivi kama ninavyomnukuu: "Watu hao wanapinga Uislamu na wanazuoni na wana nia ya kuutokomeza. Enyi wananchi, dini yetu ya Kiislamu na nchi yetu viko hatarini na tuna wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Iran," mwisho wa kunukuu.