Jul 31, 2017 04:26 UTC
  • Jumatatu tarehe 31 Julai, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe 7 Dhulqaada 1438 Hijria sawa na Julai 31, 2017.

Tarehe 31 Julai miaka 211 iliyopita ardhi ya Cape huko kusini mwa bara la Afrika ilivamiwa na wanajeshi wa Uingereza. Ardhi ya Cape au mji wa Cape Town ni sehemu ya kusini ya nchi ya Afrika Kusini iliyoko pembeni ya Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) ambayo ipo kati ya Bahari za Atlantic na Hindi. Eneo hilo lina utajiri mkubwa wa dhahabu na almasi na ni kwa sababu hiyo ndiyo maana daima wakoloni wakawa wanalikodolea jicho la tamaa.

Ardhi ya Cape, Afrika Kuisini

Miaka 131 iliyopita aliaga dunia Franz Liszt mtunzi wa nyimbo wa Hungary. Franz alizaliwa mwaka 1811. Franz Liszt pia alikuwa na kipawa na maarifa makubwa katika utungaji wa nyimbo. Nyimbo Hungarian Rhapsodies na shairi la Symphony ni miongoni mwa kazi za utunzi wa Franz Liszt. 

Franz Liszt

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita aliaga dunia Antoine de Saint-Exupery mwandishi na mwanaanga wa Kifaransa katika Vita vya Pili vya Dunia baada ya ndege yake kuanguka. Exupery alizaliwa mwaka 1900 katika mji wa Lyon nchini Ufaransa. Mwandishi Antoine de Saint Exupery alijishughulisha na masuala ya kusafiri angani kutokana na kupenda sana fani hiyo. Alijiunga na jeshi la Ufaransa katika Vita vya Pili vya Dunia na kuwa afisa wa masuala ya usafirishaji wa posta. Siku hiyo Antoine de Saint Exupery alirusha ndege hewani akiwa katika kazi zake za kawaida, lakini ndege yake ilitoweka na mabaki ya mwili wake na ndege hiyo hazijaonekana hadi leo hii. Mwandishi huyo ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwao ni "The Little Prince", "Southern Mail" na "Night Flight."

Antoine de Saint Exupery

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita kiongozi wa Waislamu weusi wa Marekani, Elijah Muhammad alitoa wito wa kuundwa dola la watu weusi nchini Marekani chini ya usimamizi wa serikali ya Federali ya nchi hiyo. Lengo la kutolewa fikra hiyo lilikuwa kukomboa Wamarekani weusi kutoka kwenye siasa za ubaguzi wa kimbari na kizazi nchini Marekani. Elijah Muhammad mwenyewe ambaye aliathiriwa na kiongozi mwingine wa Waislamu weusi wa Marekani kwa jina la la Wallace Fard Muhammad na kuwa Muislamu, alikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa na taathira kubwa katika harakati hiyo ya kudai dola la Wamarekani weusi. Elija Muhammad aliasisi chama cha Umma wa Uislamu (Nation of Islam) na kujenga misikiti na vituo kadhaa kwa ajili ya Waislamu wa Marekani. Hata hivyo baadhi ya wanachama wa harakati hiyo ya Waislamu weusi wa Marekani kama Malcolm X walikataa na kupinga baadhi ya itikadi za kidini na siasa za Elijah Muhammad.

Elijah Muhammad

Tarehe 9 Mordad mwaka 1366 Hijria Shamsia yaani siku kama hii ya leo miaka 30 iliyopita kulitokea tukio la kusikitisha la Ijumaa ya Damu mjini Makka. Siku hiyo mamia ya mahujaji wa Irani na mahujaji wa nchi nyinginezo wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu waliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa serikali ya Kiwahabi ya Saudi Arabia, walipokuwa wakitekeleza faradhi ya kujibari na kujiweka mbali na washirikina ndani ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu hutekeleza ibada hiyo kila mwaka wakati wa Hija, kutokana na mafunzo ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo sambamba na kutoa wito wa umoja na mshikamano baina ya Waislamu, hutoa tangazo la kujiweka mbali na maadui wa Uislamu hasa Marekani na utawala ghasibu wa Israel. Siku hiyo askari wa Kiwahabi wa Saudia walishambulia mahujaji hao kwa risasi na kuua mahujaji 400 wa Kiirani na kujeruhi wengine zaidi ya elfu moja.

Picha ya tukio la Ijumaa ya Damu, Makkah

Miaka 722 iliyopita  siku kama ya leo alifariki dunia Ibn Baswis mtaalamu wa kaligrafia aliyeliwa maarufu kwa jina la Damashki. Alizaliwa mwaka 651 Hijiria katika mji wa Damascus na kwa muda wa miaka 50 alijishughulisha kufundisha hati na wakaazi wa mji huo walistafidi kwa elimu na sanaa kutoka kwake. Ibn Baswis aliandika hati kwa mitindo tofauti ya kupendeza na katika umri wake wa uzeeni aliandika nakala ya Qur'ani Tukufu kwa kutumia maji ya dhahabu na kwa hati nzuri na za kuvutia. Qur'ani hiyo pamoja na athari nyingine za Ibn Basis bado ziko hadi leo.

ابن بصیص

 

Tags