Aug 14, 2017 08:05 UTC
  • Michezo, Agosti 14

Huu ni mkusayiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita.....

Voliboli: Iran yatinga Mashindano ya Mabingwa wa Dunia 2018

Timu ya taifa ya voliboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejikatia tiketi ya kushiriki Mashindano ya Dunia ya Mabingwa wa Voliboli ya Wanaume mwaka ujao 2018. Hii ni baada ya kuichachafya Kazakhstan seti 3-0 za (25-18, 25-17, 25-16) katika mchezo wa kuwania kutinga mashindano hayo ya kimataifa siku ya Jumapili katika Ukumbi wa Hossein Rezazadeh mjini Ardabil, kaskazini magharibi mwa nchi. Awali vijana wa Iran waliwakung'uta Wachina seti 3-0 za (25-21, 29-27 and 25-20), ikiwa ni mechi nyingine ya Kundi A. Mchezaji Milad Ebadipour ndiye aliyekuwa nyota wa Iran katika mashindano hayo kwa kufunga pointi 14. Vijana hao wa mkufunzi Igor Kolaković kabla ya hapo waliwapelekea mchakamchaka Korea Kusini kwa kuwalaza (25-10, 27-25, 25-18) na mchezo kati yake na Qatar siku ya Jumatatu hautakuwa na taathira kubwa kwao, kwani tayari wana tiketi mfukoni. Mashindano ya kimataifa ya voliboli hapo mwakani yanayojulikana kama 2018 FIVB Volleyball Men’s World Championship yatafanyika katika nchi za Italia na Bulgaria. Bingwa mtetezi Poland amepata tiketi ya moja kwa moja ya bwerere sawa na timu wenyeji. Timu nyingine zilizofuzu katika mashindano hayo ya dunia ni Ufaransa, Uholanzi, Slovenia, Serbia, Finland naUbelgiji kutoka bara Uropa huku Iran, Japan, na Australia zikitazamiwa kuliwakilisha bara Asia katika mashindano hayo.

Mieleka: Vijana wa Iran watwaa ubingwa wa Asia

Timu ya taifa ya mieleka ya vijana ya Iran imetwaa ubingwa wa Duru ya 5 ya Mashindano ya Mabingwa wa Mieleka Mtindo wa Kurash barani Asia.

Wanamieleka chipukizi wa Iran ya Kiislamu wameibuka kidedea baada ya kuzoa medali 3 za dhahabu, fedha 4 na shaba 4. Timu ya Uzbekistan ya mchezo huo imeibuka ya pili baada ya kuzoa medali 3 za dhahabu na fedha 1 ikifuatiwa na Turkeministan ambayo imefunga orodha ya tatu bora kwa kutwaa dhahabu 1 na shaba 8. Mashindano hayo ya kieneo yalifanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Azadi katika mji wa Bojnord, yapata kilomita 701 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Tehran.

Mwanamieleka wa Kiirani akipambana

Dhahabu za Iran ziliztwaliwa na Javad Moradi, Ghasem Baghcheghi na Hamed Rashidi katika kitengo cha mieleka ya vijana wenye chini ya kilo 81, kilo 90 na kilo 100 kwa usanjari huo. Mashindano hayo yanayofahamika kama Asian Junior Under-20 Kurash Championships yalianza Agosti 9, na kufunga pazia lake Agosti 12.

TFF yapata mkuu mpya

Wallace Karia ndiye Mkuu mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania TFF. Karia ameteuliwa katika wadhifa huo baada ya kuzoa kura 95 (asilimia 74.22) katika uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa juma. Karia alikuwa Makamu wa Rais kwenye uongozi uliopita ambao ulikuwa unaongozwa na Jamali Malinzi, aliye enguliwa kwenye uchaguzi huo kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za TFF, yeye na Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa. Karia ameibuka mshindi katika nafasi ya Rais, baada ya kuwashinda wapinzani wake Ally Mayayi na Shija Richard ambao wote walipata kura tisa. Iman Madega alipata kura nane, Fredrick Mwakalebela kura tatu na Emmanuel Kimbe akaondoka na kura moja tu. Katika nafasi ya Makamu wa Rais  aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania FAT sasa TFF, Richard Wambura alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura 85 ( asilimia 66.4) na kuwabwaga wapinzani wake Mulami Nghambi aliyepata kura 25, Mtemi Ramadhani kura 14 na Robart Selasela aliyeambulia kura mbili.

Mkuu mpya wa TFF

Baada ya kuapishwa Rais Mpya wa TFF, Karia alitoa hutuba fupi ambapo aliitaka Kamati yake kuchapa kazi kwa bidii ili kurudisha imani ya Watanzania katika mchezo huo ambao unaongoza kwa kuwa na mashabiki wengi nchini. Karia alianza kwa kuwashukuru wajumbe kwa kuonyesha imani kubwa kwake hata kumchagua yeye kuwa kiongozi mkuu wa TFF, na kuahidi kuwatumikia kwa nguvu zake zote ili kufika kule ambako wamekusudia.

Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza

Baada ya mapumziko, Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza imeanza kwa kishindo na kasi ya juu, huku baadhi ya timu zikianza kwa mguu wa kulia na nyingine zikiangukia pua. Kiungo Romelu Lukaku ambaye alisainiwa klabu ya Manchester United hivi karibuni kwa kima cha Yuro milioni 75 alidhihirisha thamani na umbuji wake baada ya kucheka na nyavu mara mbili katika mchuano dhidi ya West Ham siku ya Jumapili. Man U iliigaragaraza West Ham mabao 4-0 ikiwa ni mchuano wa ufunguzi wa Ligi ya Premier kwa timu mbili hizo. Wakiupiga nyumbani Old Trafford, Mashetani Wekundu waliupa maana msemo usemao mcheza kwao hutuzwa. Lukaku alifunga mabao yake katika dakika za 33 na 52. Kiungo Anthony Martial aliipa Man U bao la tatu kunako dakika ya 87 na dakika 3 baadaye, ikiwa zimesalia dakika za majeruhu, kiuno mwingine alisainiwa Man U kwa donge kubwa Paul Pogba akipiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la West Ham.

Katika mchuano mwingine wa aina yake siku ya Jumamosi, klabu ya Watsford ilipiga Liverpool breki na kuilamizisha sare ya 3-3 katika mechi ya ufunguzi mjini Watford.

Kwengineko Mchezaji wa ziada Olivier Giroud alifunga kichwa kizuri katika ushindi wa kushangaza baada ya Arsenal kutoka nyuma na kuilaza Leicester 4-3 katika mechi kali ya ufunguzi wa ligi ya Uingereza. The Gunners walikuwa nyuma 3-2 huku ikiwa imesalia dakika saba kabla ya Aaron Ramsey na Giroud kuingia na kufunga mabao hayo mawili yalioipatia Arsenal ushindi huo. Alexandre Lacazette aliiweka kifua mbele Arsenal sekunde 94 baada ya kuanzishwa kabla ya Shinji Okazaki kusawazisha dakika mbili baadaye. Vardy baadaye aliwaweka mbele wageni hao kufuatia krosi muruwa iliopigwa na Albrighton, kabla ya Danny Welbeck kusawazisha dakika za lala salama katika kipindi cha kwanza. Leicester ilichukua tena uongozi baada ya Vardy kufunga kona iliopigwa na Mahrez hatua iliomlazimu Wenger kufanya mabadiliko yaliozaa matunda. Mchezaji wa ziada Ramsey alifunga akiwa karibu na goli kutoka kona iliopigwa na Mesut Ozil kabla ya Giroud kufunga kichwa chengine kupitia kona iliopigwa na Granit Xhaka.

......................................TAMATI...............................